ZIMWI bandia limeundwa kuwatisha watu kuwa amani ipo hatarini kwa ubaguzi. Lakini huenda matokeo yake yakawa kinyume chake.
Wananchi wanalazimishwa kuamini kuwa ukabila na udini lilikuwa ni tatizo kubwa. Tatizo lililokuja kupigwa vita baada ya uhuru.
Sehemu ya wimbo mmoja mashuhuri unaopigwa radioni katika kipindi hiki cha maombolezo inasema: Kabla ya TANU kuundwa hali ilitisha, migongano ya dini hata ukabila, TANU iligundua hapa Tanganyika hitilafu zizikwe liundwe Taifa"
Wazee waliokuwepo zama hizo wameeleza kushangazwa kwao na kauli kama hizo.
Mzee Shaaban Gonga anaeleza kuwa nchi hii haijawa na tatizo hilo katika medani za kisiasa na maisha ya kijamii.
Akiongea na gazeti hili juzi Mzee Gonga amesema kwamba udini ni istilahi iliyozushwa baada ya uhuru ili kufifisha mchango na kazi kubwa iliyofanywa na baadhi ya wazee wazalendo wa nchi hii.
Amesema kuwa waanzilishi wa harakati za ukombozi walikuwa wa makabila mbalimbali na dini tofauti na walifanya kazi pamoja.
"Akina Sykes ni Wazulu. Dossa Azizi Mdigo, Mzee Jumbe Tambaza Mzaramo, Sheikh Mohammed Ramia Mmanyema na Sheikh Haidar Mwinyimvua Mzaramo.
"Wengine ni Ali Mwinyi Tambwe Mngazija, Idd Tulio Mzaramo, Bibi Titi Mndengereko, Tewa Said Tewa Mmakua, Saadan Kandoro Mmanyema (Mbwari) na Max Mbwana Mzaramo, John Rupia Msukuma, Japhet Kirilo Mmeru, Cecil Matola Myao.
Wote hawa walianzisha harakati za kudai uhuru bila kubaguana kabila zao hata kabla ya Nyerere kuungana nao", alisema Mzee Gonga ambaye ni Mzaramo na kuongeza kuwa hata Mwalimu alivyojiunga na harakati hakubaguliwa si kwa dini yake wala kabila lake.
Ni kwa ajili hiyo amesema Mzee Gonga, Mwalimu alipoacha kazi alipewa chumba aishi katika nyumba ya Mzee Ramadhani Jongo (Mzaramo) kona ya mtaa wa Masasi na Likoma, Kariakoo.
Mzee Gonga amesema watu walioingia katika serikali na TANU wakati wa 'Africanization' ndio waliokuja kuua moyo wa upendo wa TANU.
Amesema watu hao walionja ladha ya kushika madaraka walianzisha ubaguzi wa aina yao. Waliingiza watu katika serikali na uongozi wa chama kwa kigezo cha "huyu tutasikilizana zaidi".
Katika hali hiyo amesema kuwa wengi wa walioshiriki mapambano wakatupwa nje.
Sambamba na hali hiyo amesema kuwa yaliundwa mazingira ya kukemea udini ambao haukuwepo lakini kama mbinu kuzuia madai ya baadhi ya watu na kuifuta historia ya nyuma ionekane hakuna kilichofanyika.
Kuhusu moyo wa upendo wa TANU ambao ndio ulioleta mafanikio katika kujenga taifa hili, Mzee Gonga ameonesha wasiwasi wake kuwa hautarudi tena.
Amesema kuwa walioonja ladha ya madaraka wanataka kudumu wao na ndugu zao katika dini wanaodhani ndio watakaosikilizana.
Hata hivyo akasema watu hao ndio wanaowakemea wenzao kwa udini, wakifanya hivyo kuwazuia watu wasihoji.
"Kuunda hofu isiyokuwepo kwa wananchi bali zao la viongozi wenyewe walioonja utamu wa madaraka ni dalili kuwa ule moyo wa TANU haurejei", alisema Mzee Gonga.
Mzee Shaaban Gonga aliingia katika siasa wakati wa chama cha TAA. Kuanzia mwaka 1956 hadi 1958 alikuwa Katibu wa TANU eneo la Kariakoo na mwaka 1959 akawa Katibu wa Wodi Kariakoo chini ya DC.
Alikuwa Diwani wa Kata ya Kariakoo toka mwaka 1962 hadi 1967.
Hivi sasa Mzee Shaaban Gonga ni Mwenyekiti wa Chama cha UKUTA kwa Dar es Salaam na Pwani. Halidhalika Mjumbe wa Halmashauri wa Chama hicho.
UKUTA ni Chama cha Washairi kilichoundwa mwaka 1965 baada ya kile kilichojulikana kama Tanganyika Poetry Association kilichokuwa kimewaunganisha washairi mashuhuri kama 'Jitu Kali' Mathias Mnyampala na Shaaban Robert ambaye ndiye aliyeandaa Katiba ya chama hicho.
Wakati huo huo, Imamu msaidizi wa Msikiti wa Mtambani, Ustadh Ramadhani ameripotiwa kukamatwa na polisi juzi asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na watu walio karibu naye, polisi ambao hawakuelezwa wametoka kituo gani, walifika nyumba anayoishi Imamu huyo eneo la Kinondoni (Mwananyamala) ambapo baada ya kumhoji walimchukua hadi kituo cha polisi ambako aliwekwa mahabusu hadi jana.
Katika upekuzi, polisi walichukua kanda moja ya radio (radio kassette).
Haikufahamika Imamu huyo anatuhumiwa kuhusika na kosa gani.
Hata hivyo gazeti hili lilipowasiliana na Kamanda wa polisi mkoa wa Dar es Salaam kwa njia ya simu, alisema hana taarifa za tukio hilo.
Imamu wa Mtambani amekamatwa katika kipindi cha maombolezo ambacho viongozi wa nchi wamekuwa wakiwaasa watu kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuvuruga amani.
Kwa upande mwingine viongozi hao wamekuwa wakitoa kauli kuwaonya watendaji ambao utendaji wao huenda ukaigawa jamii katika misingi ya kidini au kikabila.
Ili kulinda amani ya nchi
baada ya kufariki Mwalimu Nyerere, Rais Benjamin Mkapa ametishia kuwa wale
wote watakaothubutu kuyaharibu yale yaliyoachwa na mwasisi huyo watakandamizwa
na jinamizi lake. Mara nyingi imeelezwa kuwa Mwalimu Nyerere hakuwa mkandamizaji.
--
|
|