Kwa ukaribu aliokuwa nao na Mwalimu Nyerere katika siasa ilitarajiwa awe miongoni mwa watu waliokwishatuma salamu.
Baadhi ya watu walioongea na gazeti hili wamekuwa wakiuliza aliko mwanasiasa huyo mkongwe. Aidha, imekuwa ikiulizwa kipi kimemsibu hata asitume salamu zake za rambirambi. Watu waliokuwa wakifuatilia kwa karibu matangazo ya vyombo vya habari toka msiba wa hayati Mwalimu Nyerere utokee; wameeleza kuwa hawakuwahi kusikia salamu kutoka kwa Bw. Milton Obote.
"Mwalimu alitoa muhanga roho za Watanzania na uchumi wao kumpiga Idi Amin ndani ya Uganda. Jambo ambalo hatimaye lilimrejesha Bw. Obote madarakani hadi alipopinduliwa tena na Bw. Okello. Vipi Bwana huyu ashindwe hata kutuma salamu", Bw. Joseph Zablon alisema wakati akiongea na gazeti hili.
Aidha, alisema kuwa katika hali ya kawaida vita vingekoma baada ya majeshi ya Amini yaliyodaiwa kuvamia ardhi ya Tanzania kutolewa.
Hata hivyo, akasema kuwa Mwalimu aliwahimiza Watanzania kujitoa muhanga zaidi kupigana ndani ya Uganda ili kuuondoa madarakani utawala wa Idd Amin. Jambo lililowaacha Watanzania wakifunga mikanda.
"Huo ni urafiki, ujirani mwema na udugu wa aina yake. Pamoja na yote yaliyokuja kutokea baadae katika siasa za Uganda bado Bw. Milton Obote angepaswa kutambua mchango huo japo kwa kutuma salamu za rambirambi", alisema Bw. Joseph.
Juzi gazeti hili liliwasiliana na Idara ya Itifaki (Protocal) Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutaka kujua ukweli wa jambo hili.
Afisa mmoja katika Idara hiyo ambaye hakutaja jina lake, alikiri kuwa hazijapokelewa salamu kutoka kwa Bw. Milton Obote.
Afisa huyo alisema kuwa kama zitakuwa zimekuja salamu labda amezituma moja kwa moja kwa familia ya Mwalimu.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanasema kuwa kushiriki kwa Rais Museven kumetosheleza kuwawakilisha Waganda wote. Lakini wengine wamekuwa pia na maoni tofauti wakisema kuwa Rais Museven ana uhusiano wa pekee kwa Mwalimu Nyerere usiomuhusu Obote.
Bw. Milton Obote alikuwa Rais wa kwanza wa Uganda na alikuwa karibu na Mwalimu katika Shirikisho la Afrika ya Mashariki.
Alipinduliwa na Idd Amin mwaka 1971 na kukimbilia Tanzania. Baada ya vita vya Kagera mwaka 1979 majeshi ya Tanzania yaliingia Uganda ambapo Idd Amin aliikimbia nchi.
Baada ya Marais Yusuf Lule na Godfrey Binaisa, Bw. Milton Obote alirejea katika Urais Uganda hata hivyo akapinduliwa tena na Tiko Okello.
Rais Yoweri Kaguta Museven alishika madaraka baada ya kupigana na kumshinda Okello.
|
|