Sheikh wa Butiama atakiwa kueleza
 

KAULI ya Imamu wa Kijiji cha Butiama iliyoripotiwa na vyombo vya habari kuwa Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa Muislamu kimatendo imezua mijadala jijini wiki hii.

Baadhi ya watu, wengi wao wakiwa Waislamu walimtaka Sheikh huyo afafanue aina ya Uislamu aliokuwa nao Nyerere.

Bwana Abu Hafsa wa Magomeni ambaye hufanyia shughuli zake mitaa ya Kariakoo akishiriki moja ya mijadala hiyo eneo la Kariakoo, alidai hadhani kama Sheikh aliyetoa kauli hiyo ana ufahamu vizuri Uislamu.

Huku akinukuu aya ya Qur'an isemayo wema '(Uislamu) si kuamirisha Misikiti, kuelekea kibla au kuwahudumia mahujaji, bali kuwa na imani ya kamili juu ya Uislamu, Bwana Abu alisema Mwalimu kushiriki ujenzi wa Msikiti kijijini au kushirikiana na Waislamu haiwezi kuwa sababu ya yeye kunasibishwa na Uislamu.

"Kama alifanya hivyo kwa nia njema ichukuliwe ni mahusiano ya kawaida baina ya watu walioamua kuishi kama jirani au taifa moja, Uislamu una misingi, kanuni na vigezo vyake", alisisitiza Bwana huyo.

Hata hivyo watu wengine walioongelea suala hili walisifu moyo huo wa Mwalimu ambao walidai unaonesha jinsi alivyokuwa si mbaguzi wa dini.

"Wale wanaosema Mwalimu alikuwa na udini waseme sasa vipi asaidie kujenga Msikiti wakati yeye ni Mkatoliki", alidai mkereketwa mmoja wa CCM wa eneo la Kariakoo ambaye jina lake halikufahamika.

Kutoka Kinondoni Mwandishi Wetu anaripoti kuwa baadhi ya Waislamu wa eneo hilo wameshutumu hatua ya waumini wa Butiama kupokea pesa kutoka kwa mtu asiye Muislamu kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti.

"Waumini hao walipaswa kuchangishana au kupeleka maombi kwa waumini wenzao sehemu nyingine badala ya kujidhalilisha kwa wasio Waislamu", amedai Ustadh Yahya mkazi wa Mwananyamala.

Katikati ya wiki hii gazeti moja la kila siku katika ukurasa wa mbele lilimripoti Imamu wa Butiama Sheikh Mbaraka Lusheke akidai ya kwamba Waislamu wa kijiji hicho wanamtambua hayati Mwalimu Nyerere kuwa alikuwa Muislamu mwenzao kwa matendo na kuvaa kwake kofia (baraghashia).

Sheikh huyo alisisitiza kuwa Msikiti wanaotumia hivi sasa walijenga kwa msaada mkubwa kutoka kwa Mwalimu Nyerere.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu Mtume (s.a.w.) alikatazwa kuswalia Msikiti uliopata kujengwa mjini Madina na Waislamu ambao imani yao ilikuwa ikiyumba.
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook