Haki na usawa katika Uislamu
 
Na Haura Shamte

MWANAMKE kama binadamu ana haki ya kupata mahitaji yote muhimu ya binadamu kama vile chakula, mavazi na pahali pa kuishi. Ana haki ya kupiga na kupigiwa kura na ni mtu huru anayeweza kwenda anakotaka, kuamini dini anayotaka na kusema anachotaka ili mradi havunji sheria zilizowekwa na jamii husika.

Kama alivyo binadamu mwingine yeyote mwanamke anahitaji matunzo na kujaliwa. Ana haki ya kupata elimu, kumiliki mali na kurithi na pia ana haki ya uamuzi.

Hizo ndizo haki za binadamu ambazo kimsingi hazipingani na haki zilizoainishwa katika Qur'an ambazo ni stahili kwa mwanamke na mwanaume.

Haki za mwanamke katika Uislamu

Mwanamke na mwanaume katika Uislamu wana haki sawa katika mambo yote ya msingi wa ubinadamu, lakini usawa huo ni kama sarafu iliyo na pande mbili.

Kimantiki ni vigumu kumlinganisha mwanamke na mwanaume kuwa wako sawa mia kwa mia kwa sababu ya tofauti ya maumbile. Ingawa tofauti hiyo si sababu ya kumdhalilisha kiumbe mmoja juu ya mwenzake bali ina lengo la kutofautisha baadhi ya majukumu ya kimaumbile tu.

Kwa mfano kazi mojawapo ya maumbile ya mwanamke ni kubeba mimba jukumu ambalo mwanaume akipewa hatalimudu. Kwa hiyo ni sawa kabisa kusema kuwa mwanamke na mwanaume ni sawa sawa katika utu wao lakini ni tofauti kimaumbile. Na kwa hivyo haki zao zitalingana na kutofautiana kwa mujibu wa maumbile yao.

Haki za Kiitikadi

Mwanamke sawa na mtu mwingine yeyote ana haki ya kuwa na mawazo yake binafsi au kufuata mawazo ya mtu mwingine kwa hiari yake mwenyewe ili mradi mawazo hayo hayaathiri mwenendo na taratibu zilizowekwa. Kwa Waislamu kinachozungumziwa ni mwenendo na taratibu zilizoainishwa katika Qur'an na Sunnah (Hadithi na matendo ya Mtume Muhammad (s.a.w.)).

Mwenyezi Mungu (s.w.) anasema katika sura ya 18 aya ya 29 ya Qur'an tukufu kuwa: "Waambie huu Uislamu ni (ukweli) uliotoka kwa Mola wenu. Anayetaka na aamini, na asiyetaka na akanushe".

Pia Allah (s.w.) anasema katika sura ya 2 aya ya 256: "Hakuna kulazimishana (mtu) kukubali dini. Uongofu upo bayana na upotofu kadhalika".

Haki hiyo inampa mtu awe mwanamke au mwanaume uhuru na maamuzi katika kuchagua dini au dhehebu analotaka au hata kufuata itikadi ya kisiasa aipendayo.

Haki za kiuchumi

Uislamu pia umempa mwanamke haki ya kumiliki mali yoyote na kiasi chochote mradi tu iwe ni halali.

Kwa msingi huo Uislamu umempa ruhusa mwanamke kutafuta mali kwa nguvu zake na ana hiari ya kutumia mali yake apendavyo. Kwa mujibu wa Uislamu wanaume ndio wenye dhamana ya kukimu na kutunza familia lakini bado Uislamu haumkatazi mwanamke kujishughulisha na shughuli zenye kumpatia kipato cha halali.

Aidha, ukiwa kuna mali iliyochumwa pamoja kati ya mke na mume, basi kile alichokiingiza mwanamke katika mali ile na kikathibitika kuwa ni chake, kitabaki kwa sheria kuwa ni chake pamoja na kilichozalishwa kutokana na mali ile. Hiyo ina maana ya kuwa mwanamke baada ya kuruhusiwa na kupewa haki ya kiuchumi, pia anayo haki ya kumiliki mali inayohamishika na isiyohamishika.

Haki za kisheria

Uislamu umeweka usawa wa kisheria baina ya mwanamke na mwanaume na umeelezwa bayana katika Qur'an endapo mmoja wao atatenda kosa. Kosa la mauaji: Aya ya 45 sura ya 5: "Na mtu (mwanaume/mwanamke) auawe kwa kuuwa mtu mwingine".

Kosa la kuzini; sura ya 24 aya 2: "Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamke wapigeni viboko mia moja pindi mkiwakamata... na isiwashike huruma juu yao".

Kosa la wizi; sura ya 5 aya ya 39: "Mwizi mwanaume na mwizi mwanamke wakateni mikono yao kila mmoja".

Haki ya kurithi

Mwanamke wa Kiislamu ni haki yake kurithi endapo atafiwa na baba yake, mama yake, mume wake na kadhalika.

Sheria ya mirathi katika Uislamu ni yenye ustawi wa familia na majukumu ya kila mmoja katika familia.

Itaendelea wiki ijayo.
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook