Tusije tukamtumia Mwalimu Nyerere kama nembo ya kuhalalisha ukandamizaji
 
 
Na Yusuf Ng'ombo
 

SIKU ya Alhamisi ya Oktoba 14, 1999 itabaki katika historia ya Watanzania. Rais Benjamin Mkapa mnamo majira ya saa sita kasoro dakika tano alitangaza rasmi kifo cha Mwalimu Nyerere na kutangaza siku 30 za maombolezo. Watu walijawa na majonzi mioyoni mwao, radio na televisheni zilipiga nyimbo za maombolezo pamoja na kuweka na kuonesha kumbukumbu za zamani za Mwalimu Nyerere.

MWALIMU Nyerere katika uhai wake amehusishwa na ukombozi na mpigania uhuru wa nchi, pia alisaidia kupata uhuru kwa nchi jirani, pia aliruhusu nchi yetu kuwa kimbilio la wapigania uhuru wa baadhi ya nchi za Afrika.

Mwalimu pia amehusishwa na amani ya nchi nzima, kuwa yeye ndiye aliyeleta amani nchini na kufanikiwa kuyaunganisha makabila yote ya Tanzania na kuleta umoja wa kitaifa.

Baada ya kifo cha MwaLimu baadhi ya wananchi wamepata wasiwasi, wameingiwa hofu, kwamba amani ya nchi itavunjika kwakuwa tu Mwalimu amekufa, kwa madai kuwa yeye ndiye aliyeleta amani, sasa amekufa na nchi itaparaganyika.

Viongozi wakubwa wa nchi nao wamekuwa wakihofu, hivyo na kusisitiza kila wanapozungumzia msiba wa Mwalimu wanasisitizia umoja na amani na kuwaomba wananchi watulie wakati huu wa maombolezo na kutoa ahadi za kupambana na yeyote atakayeleta chokochoko wakati huu.

Lakini hofu hii inatoka wapi hasa, kitu gani alichokuwa nacho Mwalimu Nyerere kimezuia amani isichafuke wakati wa uhai wake na kwanini amani itoweke wakati huu ambao Mwalimu ametoweka.

Kwani nini kinafanya amani iwepo au kipi kinasababisha amani isiwepo mpaka tuingiwe na hofu kubwa kiasi cha kuihusisha amani ya nchi na Mwalimu Nyerere.

Hali hii yote haikutokea kwa bahati mbaya, hii ni kazi ya mikono yetu wenyewe kwa kuipotosha historia halisi ya nchi yetu. Historia ya nchi imepotoshwa kwa manufaa ya watu wachache, baadhi ya watu wamepewa mizigo ya sifa wasiyoweza kuzibeba. Mwisho wake ndio leo tunajisulubu wenyewe mioyoni mwetu. Tumejawa hofu na wasiwasi.

Katika historia ya nchi yetu pamoja na kuwa na ufahamu mdogo wa historia, lakini historia haioneshi kama nchi yetu ilipatikana na machafuko mpaka apatikane mtu wa kuondoa machafuko na kuleta amani.

Pia katika historia ya kupigania uhuru wa Tanzania tumegundua kwamba si Mwalimu Nyerere pekee aliyeleta uhuru bali walikuwepo wazee wa Dar es Salaam "Waislamu" wa wakati huo waliokwishaanza kupigania uhuru kwa kuanzisha vyama vyao. Baadaye walimkaribisha Mwalimu Nyerere bila kujali kama ni Mkristo au anatoka kijijini.

Wazee wa Dar es Salaam "Waislamu" bila kujali tofauti za kidini na sehemu wanazotoka, walimkaribisha Mwalimu mjini na baadaye walimpa uongozi katika vyama vyao walivyokwishavianzisha vya kupigania uhuru.

Ingawa katika historia tuliyofundishwa mashuleni hayamo haya lakini yamegundulika baada ya kifo chake, katika kumbukumbu za hotuba zake ambazo zimesikika redioni mara kwa mara.

Katika hotuba yake aliyoitoa Novemba 2, 1985 katika ukumbi wa Diamond Jubilee wakati akiwaaga wazee wa Dar es Salaam baada ya kung'atuka Urais, Mwalimu alisema.

"Nimekuja natoka Ulaya tena msomi, msomi ninakuja, nimetoka Ulaya nimesoma muda mfupi tu, jamaa hawa wa mjini Dar es Salaam kwa kweli sijapata kuishi mjini, lakini jamaa hawa mara wakaniamini haraka haraka sana. Wakaniamini haraka sana."

"Katika muda wa miezi mitatu wakanichagua President wa African Association. Tanganyika African Association... Ndipo tukaanza sasa shughuli za kujaribu kuandika katiba mpya ya TAA kusudi tuipe madhumuni ya shahaba ya kuleta uhuru."

"Mwaka uliofuata 1954 ndio tuka, kwa kweli mimi nilidhani tutachukua katiba tu wenzangu wakasema hapana, tukibadili katiba tubadili na jina".

"Tukahaingaika sana kupata jina na hao hao kina Abdul Sykes, jina lile hatukuligundua. Wao walikuwa wamelifikiria zamani wakina Abdul Sykes hao. Walikuwa Burma alikuwa askari na kule waliwahi kufikiria kuanzisha chama...

"Kusema kweli wao waliwahi kufikiria kabisa Tanganyika African National Union.

"Kwa hiyo wakati tunahangaika hangaika pale tuchukuwe jina gani tuchukue Tanganyika African Union wakasema hali itafanana na Kenya African Union. Watadhani nao ni Maumau. Tunataka kuanzisha Maumau yetu. Ndio wakina Abdul Sykes wakakumbuka jina lao walilokuwa wameliunda walipokuwa Burma, wakasema tuite Tanganyika African National Union, ndio tukaanzisha..."

"Wazee wa Dar es Salaam wakaniamini upesi sana, kijana mdogo nikawa na uhusiano mkubwa sana na wazee wa Dar es Salaam. Mkubwa sana, watu wazima, mimi mdogo. Wadogo wenzangu wengine walikuwa ni hao Abdul Sykes kina Abbas Sykes wakina Dossa. Lakini wengine wote walikuwa watu wazima...".

"...Mimi Mkristu, wazee wangu Waislamu wale, lakini tulikuwa tunaelewana sana na wazee wangu. Wazee wengine wanakumbuka. Tumekwenda Bagamoyo kule na wazee wangu. Labda Mkristo mimi peke yangu au wakati mwingine John Rupia anakuja. La sivyo wazee wangu wale Waislamu na mimi mtoto wao. Tunakwenda kuomba dua huko baadhi yetu mtakumbuka...".

Kama nilivyosema hapo juu vichwa cha wananchi vimechafuliwa na akili zao zimejazwa propaganda hizi na zile kuanzia mashuleni, mitaani, kwenye mikutano ya siasa, radioni mpaka kwenye nyimbo watu wamefutwa kumbukumbu ya mambo (memory) vichwani mwao.

Viongozi wa nchi wamewajenga wananchi kumtukuza mtu au kikundi cha watu fulani kuwa ndio bora zaidi kuliko wengine.

Mwalimu Nyerere anastahili sifa nyingi sana, tena alikuwa na kipaji cha kuongea, hekima na busara, lakini asipewe sifa kupindukia kiasi cha kumkufuru Mwenyezi Mungu.

Ilifikia wakati watu walimuhofu Mwalimu na kujenga imani kubwa sana kuwa afanyalo ndilo sawa na asemalo ndilo lifaalo. Mwalimu akimchukia mtu au kikundi cha watu basi jamii iwachukie na iwasuse moja kwa moja bila ya kuhoji, mradi fulani kasema.

Imani hiyo hiyo ndio iliyowafanya wananchi waamini amani ni Nyerere na Nyerere ndiye amani mpaka wakajenga hofu hivi sasa wakati Mwalimu hayupo tena.

Imani hiyo imewafanya watu wamkufuru Mwenyezi Mungu kwa kumwita Mwalimu ni Nabii. Wapo waliodai Mwalimu ni nusu Mungu au Mungu. Wengine waliridiki kusema fimbo yake ni ya miujiza, ya uchawi, pia matajiri waliodiriki hata kutaka kuinunua fimbo yake kwa imani za kishirikina.

Sasa kwa imani hizi ni wazi kuwa watu waliojengwa na imani hii vichwani mwao, watahofu, watalia kupindukia, watapagawa na kupata homa na kuamini "Baba ametutoka... hatumwoni tena... amani aliyoijenga itatoweka... nani ataziba pengo... nani atatushauri!!!"

Katika kuuenzi mchango wa Mwalimu na kudumisha amani hatuna budi kuwaunganisha wananchi kuwa kitu kimoja bila ya kuwanyanyasa hawa na kuwanyongesha wengine kwa rangi zao, dini zao, vyama vyao vya kisiasa au maeneo wanayotoka, tufanye hayo kwa vitendo yaonekane hadharani.

Kitu cha ajabu hata viongozi wakubwa wa nchi wameingiwa na woga na hofu ya kuvurugika amani na katika hotuba zao mara kwa mara wamekuwa wakiimba amani ... amani... amani!!!.

Ni kweli!! Kama tukiamini Mwalimu amekufa na amani itakufa, tutafarakana wenyewe kwa wenyewe, itakuwa kweli tutatafutana, lakini kama kama tukiamini amani hii si kwa ajili yake basi tutaendelea na amani yetu tena maradufu.

Tusijinyongeshe kwa imani za ajabu ajabu tulizojengewa nchini muda mrefu sasa, kila kitu kinakwenda kwa muda maalum na wakati maalum. Mwendeshaji wa mambo yote ni Mungu. Yeye ndiye mwenye uwezo wote.

Pamoja na yote hayo baada ya maombolezo ningependa kuwaomba viongozi wanaoimba amani wadumishe misingi ya amani iliyoachwa na wazee wetu, asibuguliwe mtu kwa sababu ya kabila lake, dini yake au jinsia, asinyanyaswe yeyote kwa shinikizo la mtu au watu fulani wakubwa au wadogo.

Viongozi wote wa vyama vya siasa, wa dini na madhehebu mbalimbali wapewe hadhi na fursa sawa na heshima isibague watu katika nafasi zao.

Vyombo vya dola vitumie sheria katika kazi zao, viache kutumia jazba na chuki binafsi katika kushughulikia matatizo ya makundi ya watu na wachukuliwe hatua za kisheria wakibainika na makosa.

Haki itawale katika shughuli za kiserikali za kila siku ndio amani itadumu, wasinyimwe watu haki yao kwa wingi wao ama kwa uchache wao ilimradi haki yao wapewe na atakayezuia achukuliwe hatua ili kuepusha vurugu.

Serikali isitumie propaganda za kufa kwa Mwalimu Nyerere kama kinga ya kuwaogopesha wanaodai haki zao wasidai kwa kuwahusisha na machafuko ya nchi.

Serikali isihofishe watu na kuwakandamiza kwa kuwa tu Mwalimu ametoweka na kuwatangaza vibaya kwa wengine kuwa wanataka kuvuruga amani ili ipate kuwakandamiza kwa manufaa yao wenyewe.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook