Utaratibu wa maombolezo ubadilishwe - Wananchi

SERIKALI imeshauriwa kubadili utaratibu wa maombolezo unaoendelea hivi sasa katika vyombo vya habari ambapo hutumika kwaya za kidini na hutuba za hayati mwalimu Nyerere alizozitoa baada ya kustaafu Urais.

Badala yake imependekezwa zitumike nyimbo za zamani zinazotoa nasaha kwa jamii, au hotuba za viongozi mbali mbali miaka ya sitini na sabini sambamba na kuwahoji watu mbali mbali kuhusiana na hali ya nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Aidha zihusishwe nyimbo za "brass band" za jeshi la wananchi, polisi na magereza kama ilivyokuwa wakati wa msiba wa hayati Edward Moringe Sokoine 1984 au wakati wa vita vya Kagera mwaka 1978-79.

Hayo ni baadhi ya maoni yaliyotolewa na wananchi mbalimbali waliohojiwa na gazeti hili kuhusiana na msiba ambao nchi inaomboleza hivi sasa.

Imedaiwa kuwa kwa serikali kufanya hivyo kutaleta hisia za utaifa na mshikamano zaidi katika kipindi hiki muhimu katika historia ya nchi yetu.

Wakitoa maoni yao kupitia gazeti hili wananchi kadhaa wamelaumu utaratibu uliopo ambao wameueleza kuwa unamuelekeo wa kidini zaidi kuliko utaifa.

Mama Mage wa Kinondoni akizungumzia suala hilo, alisema uombolezaji wa aina hiyo unaweza kuwafanya baadhi ya watanzania wadhani hii imekuwa fursa kwa chama fulani na baadhi ya viongozi wake kujijenga kwa wananchi au baadhi ya madhehebu ya dini kueneza imani yao.

Mzee Shaabani Ndombaki mkazi wa Sinza ameshauri nafasi ya kwaya za kidini ichukuliwe na hotuba za viongozi mbali mbali wakihusishwa na wale wa vyama vya upinzani kuhimiza maendeleo na mshikamano wa utaifa.

Wengine waliotoa maoni yao wamelaumu ahadi zinazotolewa na viongozi wakuu kusimamia yote yaliyoachwa na hayati Mwalimu Nyerere kwa madai ya kuenzi jitihada zake.

"Mwalimu ni mwanaadamu wa kawaida, yapo mazuri aliyoyafanya na yapo mengi aliyokosea, wajibu wetu siyo kung'angania kibubusa kuendelezwa yaliyoachwa bali kutafakari na kujadili namna nzuri zaidi ya kuboresha umoja na mshikamano wetu", amesema mzee Ndombaki.

Naye bwana Abdallah Musa wa Buguruni alitahadharisha juu ya michango ya nguvu inayosemekana kuendeshwa na baadhi ya vyombo vya umma.

Alisema kuwakaba wananchi wachangie rambi rambi wakati hali zao ni ngumu huenda kukazua mtafaruku.

"Ni kweli familia ya Mwalimu inahitaji kuhudumiwa lakini sisi tunaokabwa kutoa michango hali zetu ni mbaya kuliko tanaotakiwa kuwahudumia", alilalamika bwana Abdallah ambaye alidai kuwa ni mfanyakazi katika moja ya mashirika ya umma ambalo alidai hivi karibuni lilikata sehemu ya pesa kutoka mshahara wa kila mfanyakazi kwa ajili hiyo.

Aidha, Bwana Shakir wa Mabibo Jijini akizungumzia uchangishaji huo alisema desturi za waungwana wanapofiwa huwekwa sinia ambalo huwa ni hiyari kwa mtu kutoa au kutotoa kiasi chochote kile kwa ajili ya wafiwa.

"Rambirambi gani hii ya kulazimishana?", alihoji Bwana Shakir.

Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa rais mstaafu wa awamu ya kwanza, alifariki dunia katika hospitali ya St. Thomas mjini London ambako alikwenda kutibiwa ugonjwa wa kansa ya damu.

Mwasisi huyo wa CCM alizikwa Jumamosi iliyopita kijijini kwake Butiama katika mazishi yaliyohudhuriwa na maelfu ya watanzania wakiongozwa na Rais Benjamin Mkapa ambaye alifuatana na viongozi wengine wa ndani na nje ya nchi.


Madaraka si kipimo cha utukufu - Sheikh Zuberi
 

IMAM wa Masjid Sunni (Nunge) mjini Dodoma, Sheikh Ahmed Zuberi ameuambia uma wa Waislamu waliohudhuria swala ya Ijumaa hivi karibuni kuwa kipimo cha utukufu mbele ya Allah (s.w.) ni kumcha Mungu, aidha madaraka, vyeo na utajiri usioambatana na kufuata amri za Allah (s.w.) si vigezo vya utukufu.

Sheikh Zuberi alisema kwa mujibu wa mafunzo ya Qur'an, Waislamu wamefundishwa kuwa; "Kwa hakika mbora mbele ya Allah (s.w.) ni yule aliye mcha Mungu".

Akitoa nasaha zake kabla ya swala ya Ijumaa, Sheikh Zuberi aliwasisitiza Waislamu kuwa waangalifu kwa kuutumia umri vizuri katika twaa ya Allah (s.w.).

Alisema mtu kupewa umri mrefu wenye kuambatana na kuafnya maaswi ni hasara kubwa hapa duniani na akhera, aidha pia alisisitiza kuwa mtu kupewa umri mfupi wenye kuambatana na matendo mazuri yenye kumridhisha Allah (s.w.) ni aula (bora) zaidi.

Aidha, Sheikh Zuberi amewakumbusha Waslamu juu ya wajibu wao wa kuyaimarisha majumba (Misikiti) ya Allah (s.w.). Alisema kuwa kujenga Misikiti kwa ajili ya Allah (s.w.) ni kujijengea majumba makubwa na ya fakhari huko peponi, sambamba na waadhi kwake huo Sheikh huyo aliwataka Waislamu kuonesha mshikamano katika ujenzi na upanuzi wa Msikiti wa Nunge.

Alisema, hatua iliyofikiwa inahitaji mshikamano, pia aliwashukuru wale wote waliotoa misaada kwa ajili ya upanuzi wa Msikiti huo.
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook