VYAKULA tunavyokula kila siku na namna tunavyokula vyakula hivyo, ni mambo ambayo yanaweza kuleta afya nzuri au afya mbaya kwa mtu anayehusika. Katika makala haya tutazama dhana ya kula kwa wakati na kiasi maalum inavyoweza kuwa neema au balaa kwa mtu anayekula.
Kula chakula pasipo kufuata saa maalum (iliyopangwa) ni moja ya mambo yanayoleta magonjwa kadhaa ya tumbo.
Leo unawahi, na kesho unachelewa kula chakula, baadhi ya nyakati unashikwa na njaa kwa muda mrefu, baadhi ya nyakati unajaza tumbo kupita kiasi, hali kama hiyo ikiendelea kwa muda mrefu, uwezo wa kufanya kazi wa tumbo lako utafifia na kusababisha magonjwa ya tumbo.
Kwa hiyo, kinachotakiwa mtu awe na muda maalum wa kula chakula. Chakula hicho kiwe cha asubuhi, mchana au cha usiku lazima kiliwe kwa wakati maalum.
Sambamba na tatizo la watu kutokula kwa wakati maalum, kuna baadhi ya watu hawana uwezo wa kujizuia wakiona chakula kinono, wanakula kingi kupindukia, hasa katika sikukuu (au sherehe fulani). Tabia hii ni mbaya na ni rahisi kusababisha magonjwa.
Tumbo la mtu ni kama mpira ambao una uwezo wa kupanuka. Lakini uwezo huo una kikomo chake. Ukila chakula kingi huongeza mzigo wa tumbo na kuliumiza. Kwa hivyo, usile chakula kupita kiasi, bali kula kiasi ulichozoea.
Dhana ya kula kwa wakati na kiasi maalum ni jambo ambalo pia limekokotezwa sana katika vitabu vya dini. Kwa mfano katika kitabu Sahihi Bukhari na cha Sahihi Muslim (vitabu vya dini ya Kiislamu), Mtume Muhammad (s.a.w.) anasema: "Sisi ni watu wastaarabu hatuli mpaka tuwe na njaa. Na tunapokula hatushibi kupita kiasi".
Hata hivyo wananchi hawana budi kutengeneza mazingira ya kijamii yatakayomhakikishia kila mtu kupata mahitaji ya lazima kama chakula kwa urahisi.
Ni lazima kupambana na yeyote
yule anayezuia, kwa njia yoyote ile, kupatikana haki hiyo ya waja wa Mwenyezi
Mungu.
--
|
|