Mashairi
 

Ujamaa!

Ya kale tulosomewa, tukingali darasani,
Mahubiri ya usawa, jinsia na zote dini,
Bongo zetu zikalewa, maneno tukaamini,
Hukumbuka nikacheka, hekaya za Ujamaa!

Ilani ilinadiwa, kwisha kwenda mkolini,
Hayuko wa kuonewa, wala kujihisi duni,
Tumebakia wazawa, tushike vyema sukani,
Hukumbuka nikacheka, hekaya za Ujamaa!

Arusha kulikaliwa, Azimio kusaini,
Ubepari kuondowa, ujamaa kuamini,
Wenye mali wakaporwa, mashamba na marosheni,
Hukumbuka nikacheka, hekaya za Ujamaa!

Lengo wote tuwe sawa, wasiwepo wa kukhini,
Kusoma na kutibiwa, na madaraka ya ndani,
Dira tukaichukuwa, Uchina na Urusini,
Hukumbuka nikacheka, hekaya za Ujamaa!

Ujenzi umelemewa, ujamaa uko chini,
Lengo halikufikiwa, tumetehemu njiani,
Si mambo ya kuambiwa, inaona kila mboni,
Hukumbuka nikacheka, hekaya za Ujamaa!

Shule zinalaumiwa, kufunza elimu duni,
“Wajamaa” tunachekwa, wala haya hatuoni,
Wana wa watu “wakubwa”, wanasomeshwa Londoni,
Hukumbuka nikacheka, hekaya za Ujamaa!

Hata tunakotibiwa, dawa hazipatikani,
Muhimbili yakimbiwa, watu wenda “Uropani”,
Hakika tumezidiwa, kwa maoni ya kichwani,
Hukumbuka nikacheka, hekaya za Ujamaa!

Wajifunze wasofunzwa, uungu wanotamani,
Kutaka kuabudiwa, kwa maoni ya kichwani,
Kina Mao wameachwa, watu hawaulizani,
Hukumbuka nikacheka, hekaya za Ujamaa!

Kaditamati makiwa, ujamaa kitu duni,
Hadharani umetupwa, wala hatuna huzuni,
Mwenye kufaa kuigwa, ni mjumbe wa Manani,
Hukumbuka nikacheka, hekaya za Ujamaa!

Jihad  Saballa,
Box 347,
Shinyanga.



Leo ninaunguruma!

Leo ninaunguruma, Kiko mithili ya simba,
Uwanjani nasimama, nasema tukaze kamba,
Sikizeni nchi nzima, Bara, Unguja na Pemba,
'Mmm' 'mmm' amkeni, oneni hii dhuluma.

Nanguruma asubuhi, enyi macho mlofumba,
Oneni Muembe chai, wameuwa kwa kutamba,
Kwa hasira kama  chui, pongezi wakajigamba,
'Mmm' 'mmm' amkeni, oneni hii dhuluma.

Leo ninaunguruma, nasema tukaze kamba,
Umekubuhu unyama, utu hawendi sambamba,
Haki tupinge hujuma, tusibaki ombaomba,
'Mmm' 'mmm' amkeni, oneni hii dhuluma.

Oneni hii dhuluma, simaneno ya kupamba,
Paroko alituchoma, kupitia kwa Makamba,
Watoto akina mama, wakapigwa na kuvimba,
'Mmm' 'mmm' amkeni, oneni hii dhuluma.

Leo ninaunguruma, nasema tukaze kamba,
Ikulu tuliyatuma, madai haki kuyumba,
Haki ipewe heshima, dhuluma yavunja nyumba,
'Mmm' 'mmm' amkeni, oneni hii dhuluma.

Kimya hiki cha dola, cha haki ama kasumba,
Ushindweje utawala, kuwafikisha kizimba,
Walopiga kama swala, Chuki shaba ikachimba,
'Mmm' 'mmm' amkeni, oneni hii dhuluma.

Hapa mwisho kaditama, ujumbe tukaze kamba,
Pamoja tukisimama, utafutika umwamba,
Twende tusirudi nyuma, zetu haki wameramba,
'Mmm' 'mmm' amkeni, oneni hii dhuluma.

Idd Kikong'ona,
Morogoro.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook