Ziko faida nyingi katika utaratibu wa kukata rufaa.
Kwanza mrufani anapata nafasi adhimu ya kupinga uamuzi, hukumu au adhabu ya mahakama inayohusika katika masuala ya ushahidi, pia sheria. Mfano mzuri ni shauri la Awadh Nayopa v. R. (Shauri la Jinai la Rufani Na. 116. 1978. Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam (Hijachapishwa) ambapo mrufani alitiwa hatiani kwa wizi akiwa mtumishi kinyume na fungu la 271 na 265 la Kanuni la Adhabu (Sura ya 16, Sheria za Tanzania) na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani. Hati yake ya rufani, ambayo ilitayarishwa na wakili wake, pamoja na sababu nyingine, ilikuwa na hoja zifuatazo:
1. Kwanza msomi Hakimu alikosea kisheria kumtia hatiani mrufani kwa kosa la wizi akiwa mtumishi bila kuzingatia vipengele vya kosa linalohusika.
2. Kwamba msomi Hakimu alikosea kisheria kukubali nakala za stakabadhi hizo zilipotea.
3. Kwamba msomi Hakimu alikosea kuukubali na kuutilia maanani ushahidi wa kuambiwa.
4 Kwamba kulikuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha shtaka dhidi ya mrufani.
Itaonekana kuwa sababu tatu za kwanza ni za kisheria ambapo ile ya nne ni ya kiushahidi.
Faida ya pili ya rufani ni ule uwezo ambao mahakama ya rufani yanao kuweza kuchukua ushahidi wa nyongeza. Wakati mwingine ili haki itendeke inabidi kumwita au kuwaita mashahidi wa nyongeza na kupata ushahidi wa lazima kufikia uamuzi sahihi kisheria. Hali hii inatokea wakati ambapo mahakama ya awali yalishindwa kufanya hivyo.
Ziko namna mbili ambazo ushahidi wa nyongeza unaweza kuchukuliwa: Mahakama ya rufani kuamuru mahakama ya awali kufanya hivyo au, mahakama ya rufani kuchukua ushahidi huo wenyewe (F. 369 (1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Kwa bahati mbaya uwezo wa mahakama hautumiwi sana penginepo hata pale inapobidi kufanya hivyo. Aghalabu jambo hilo husababisa haki kutotendeka ipasavyo. Mathalan katika shauri la Wibert Mushi v. R (Shauri la Jinai la Rufani Na. 31, 1980, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mbeya (Haijachapishwa), mahakama ya awali yaliacha kumwita shahidi muhimu mno kwa upande wa mashitaka. Pamoja na makosa hayo mahakama yaliridhika kuwa kulikuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani mshitakiwa kwa kosa la kupokea rushwa. Katika kusikiliza rufani iliyokatwa na Wilbert Mushi, Mahakama Kuu yaligusia kosa la kutoitwa shaurini shahidi huyo wa lazima - Erick Nonyoma. Badala ya kutumia uwezo wake wa kufanya hivyo, au kuyataka mahakama ya awali kuchukua ushahidi wa Erick Nonyoma, Mahakama Kuu yalitumia kasoro hiyo kuiruhusu rufani.
Tatu, daima mrufani, ana haki ya kuwepo mahakamani kubishania rufani yake. Anaweza kuwepo mwenyewe au kuwakilishwa na wakili wake. Haki ya kuwakilishwa na Wakili inatambulikana kisheria (F. 310, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j) na ilisisitizwa zaidi katika shauri la Alimasi Kalumbeta v. R (Shauri la Jinai la Rufani Na. 1979, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mbeya (Haijachapishwa).. Katika shauri hilo Hakimu na mahakama ya awali alikimbilia kusikiliza na kuamua shauri lenyewe wakati ambapo mrufani alieleza haja ya kuweka wakili.
Kuwepo mahakamani, iwe kwa mrufani binafsi au wakili wake, kuna faida kubwa sana kwa mrufani kwa vile huweza kuelezea kwa nafasi sababu yake pamoja na kuzijibu hoja zote dhidi ya sababu alizokwishatoa. Kwa bahati mbaya warufani wengi Tanzania hawatetewi na mawakili na aghalabu hawataki kuwepo mahakamani kuelezea sababu za rufani zao. Jambo hilo huyapa taabu mahakama kuweza kuelewa hasa sababu za rufani hizo kwani, kama tulivyoona, hati za rufani nyingi ambazo zimetayarishwa na warufani wasio na mawakili ni ndefu mno na hazieleweki vizuri.
Hivyo hapana shaka yoyote kwamba haki ya kutetewa na wakili ni jambo zuri katika uendeshaji wa mashauri ya jinai na utoaji haki katika mfumo wowote wa sheria unaojidai umekomaa. Hata hivyo, haina maana kuwa na haki isiyoweza kupatikana. Hadi leo hivi, kwa walio wengi hapa nchini, kuajiri wakili (achilia mbali bora ambaye aghalabu hutoza ada kubwa zaidi) ni mithili ya ndoto. Shauri la Martha Wejja v. Kitwana Kondo (Shauri maalum la Madai Na. 1, 1980 Mahakam Kuu, Dar es Salaam) kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa ubunge wilaya ya Ilala, Dar es Salaam ni ithibati ya haja ya kuwa na wakili katika utekelezaji haki.
Matatizo katika ukataji wa rufaa
KUKATA rufani kuna matatizo yafuatayo ambavyo ni vipingamizi vinavyohitaji kutiliwa maanani wakati wote. Kwanza, ukomo wa muda wa kukata rufaa. Ukiachilia rufaa zote kutoka Mahakama ya Mwanzo kwenda mahakama ya Wilaya kuna muda ambao, kama ambavyo imekwishaelezwa awali, unaowekwa kumtaka mrufani awasilishe taarifa ya kukata rufaa na baadaye hati yenyewe ya rufaa. Tatizo ni kuwa mara nyingi watu wengi, hasa wasio na mawakili, hawaelewi masharti na umuhimu wa muda uliowekwa kufanya mambo hayo mawili. Ni kweli kwamba mahakama yanatakiwa kumfahamisha aliyetiwa hatiani haki yake ya kukata rufaani. Vile vile ni kuona kwamba kwa jumla mahakama hutekeleza wajibu wake huo. Isipokuwa mahakimu wengi hawawafahamishi wahusika muda unaotakiwa kutoa taarifa zao za kukata rufaa. Bahati mbaya sheria haitoi sharti la kuwataka wafanye hivyo. Lakini, hata kama mahakimu wote wangeweza kuwaelezea wahusika muda unaotakiwa kufanya mambo hayo mawili, bado kuna matatizo kadhaa yanayofanya taarifa hiyo isikidhi haja. Moja ya sababu kubwa ni kughafilika kwa wahusika. Baada ya fazaa za kuhukumiwa kifungo wahusika wengi huchanganyikiwa na kupotewa na fahamu ya muda wanaotakiwa kutoa taarifa zao za kukata rufaa na baadaye kukata rufaa yenyewe.
Pili woga. Uamuzi wa kukata rufaa, kwa baadhi ya wahusika, huchukua muda mrefu kufikiwa. Mhusika anaweza kuamini kwamba ametiwa hatiani kwa makosa lakini bado hapo hapo, akazingirwa na hofu ya kushindwa kujieleza na kushinda rufani katika mahakama ya juu. Pengine ni imani kwamba endapo rufani yake itatupiliwa mbali basi kifungo chake kitaongezwa. Kutokana na sababu hizo wale ambao rufani zao zingekuwa na uwezakano mkubwa wa kukubaliwa wanabaki kutumikia kifungo. Hatimaye wanatoka gerezani na kumbukumbu ya kufungwa. Na kwa wale ambao walikuwa wameajiriwa kabla ya vifungo hivyo wanakosa mishahara, kiinua mgongo na akiba ya uzeeni.
La kuudhi zaidi ni kuwa mtu huwa ametumikia adhabu ambayo, pengine, hakuistahili kisheria.
Ucheleweshaji wa nakala za mwenendo wa shauri ni tatizo jingine kubwa kwani kila hati ya kukata rufaa, isipokuwa pale endapo Mahakama Kuu yameagiza vingine, lazima iambatane na nakala ya hukumu au amri inayopingwa (F. 362(a), Sheria ya Mwenendo wa Jinai i.h.j). Kukosekana au upungufu mkubwa wa vifaa vya kutayarishia nakala hizo kama vile karatasi, wino na kadhalika ni moja ya sababu za ucheleweshaji wenyewe. Tatizo huwa kubwa zaidi shauri linalokatiwa rufani ikiwa ni refu sana hivyo kuhitaji karatasi nyingi vile vile.
Utayarishaji wa hati za rufani aidha sio jambo rahisi kama ilivyokwishagusiwa hapo awali. Ugumu wake uko katika kuuchambua ushahidi uliotolewa awali kisha kugundua masuala ya kubishaniwa. Katika mashauri marefu zaidi suala hilo hujitokeza na kutatanisha kupita ilivyo kwenye mashauri mafupi. Licha ya hayo idadi kuwa ya warufani hawajui kusoma wala kuandika wachilia mbali kuweza kutafautisha masuala ya sheria na ushahidi. Hivyo inabidi waandikiwe au waandike wenyewe, ikiwa wanajua kusoma na kuandika, wakababaisha tu juu ya sababu za rufani zao.
Inapokuja kwenye kusikiliza rufaa yenyewe uwezo wa kujieleza vizuri huwasumbua warufani wengi. Kwenye shauri la Moffat Kajange v. R., (Shauri la Jinai la Rufani Na. 180, 1979, Mahakama ya Rufani Tanzania Mbeya (Haijachapishwa) mrufani alikataa kupinga hukumu ya kifo iliyotolewa na Mahakama Kuu dhidi yake. Wakati wa kusikilizwa rufani aliamua kumkataa wakili wake aliyemtetea awali kwa sababu hakuridhika naye, akaomba ajitetee mwenyewe. Mahakama ya Rufani, baada ya kutaka ushauri wa wakili wa mrufani, ambaye baadaye alijitoa kwenye shauri hilo, yaliyakubali maombi ya mrufani. Mrufani alianza kusoma kwenye karatasi alizokuja nazo. Alichukua muda mrefu mno, kama saa moja na robo. Isipokuwa aliloweza kufanya ni kulalamika bila ya sababu za maana, kwamba ameonewa na kusingiziwa. Aliendelea kurudia rudia hoja hizo hizo mpaka alipotakiwa amalize maelezo yake. Akachukua tena nusu saa nzima kurudia, kwa jumla, yale yale, ingawa kwa namna ya maneno tofauti. Haikuwa vigumu, kwa umati uliofurika ndani ya Mahakama Kuu Mbeya kuelewa nini litakalotokea. Matokeo yake rufani ilikataliwa na hukumu ilisomwa pale pale bila ya kuahirisha kikao.
Ingawa sio kweli kwamba bingwa
wa kuzungumza mahakamani hushinda rufani yake daima, ila dhahiri uwezo
huo ni silaha kubwa mno kwa mrufani.
--
|
|