"Hawaangalii kwa Muislamu udugu wala ahadi, basi hao ndio wapitao mipaka". (4:10)
Haya ni maelezo ya Qur'an kutoka Surat At-Tawba juu ya mahusiano na wasiokuwa Waislamu.
Ilivyo, pamoja na tofauti za kiimani watu katika jamii wanatakiwa waishi kwa amani, waelewane na wasidhulumiane.
Pamoja na uhuru wa dini, watu wasionewe na haki zao za msingi zisihujumiwe.
Maadhali hayo yanapatikana katika jamii ni wajibu wa kidini kwa Waislamu kuheshimu, kutii na kufuata makubaliano na taratibu zilizowekwa ili kukidhi haja ya kuishi wote kwa amani.
Hata hivyo wapo watu wanapopata uongozi na madaraka katika jamii husahau kanuni hii na hutawaliwa na chuki za kidini dhidi ya wengine.
Inapotokea hali hiyo ni wazi wapo watu watakaoonewa na kudhulumiwa haki zao kinyume cha katiba na sheria.
Kwa muda mrefu sasa Waislamu wamekuwa wakieleza kuwa kuna kila ushahidi kuthibitisha kuwa walioshikilia madaraka ya serikali katika ngazi mbalimbali ambao wengi wao ni Wakristo wamekuwa si waadilifu.
Wanakiuka kanuni za kuishi pamoja kwa amani.
Kwa bahati mbaya malalamiko ya Waislamu yamekuwa yakishukia sikio la uziwi.
Hata pale ambapo kwa wazi kabisa Waislamu wamehujumiwa kama kuuliwa pale Mwembechai, serikali haielekei kujali. Utadhani waliouliwa si watu au hakuna katiba inayolinda haki ya uhai kwa wananchi.
Hii tafsiri yake nini? Je, Waislamu waamini kuwa walioshikilia madaraka nchini hapa ni sawa na wale wanaotajwa katika aya ya nane na kumi na At-Tawba?
Na kama itasibu kuwa hivyo, nini mustakbali wa nchi hii?
Waislamu wanadhima kubwa kuichambua na kuielewa vizuri jamii hii ya Watanzania na kuangalia Qur'an inawapa mwongozo gani.
|
|