'Waislamu msijidhalilishe'
 

WAISLAMU wote duniani hawapaswi kufikiri kuwa watapata mafanikio kwa kujidhalilisha kwa Mayahudi na Wakristo.

Hayo yamesemwa na mmoja wa wahadhiri maarufu jijini hapa Sheikh Hilal Shaweji.

Akifafanua maelezo yake hayo maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam alisema, "Hawa ni wenzetu ki-asili tu yaani wote ni wana wa Adam, hatufanani kiimani, hivyo Waislamu wasifikiri watapata mafanikio kwa kufuata itikadi zao.

Sheikh Hilal aliyerejea hivi karibuni toka Rufiji sehemu ya Ikwiriri alieleza hatua iliyofikiwa na Waislamu kuunda UWAWARU huku akirejea aya nzima ya Qur'an (2) sura ya (120) inayosema Hawatakuwa radhi juu yako Mayahudi wala Wakristo mpaka ufuate mila yao. Sema: "Hakika uongozi wa Mwenyezi Mungu ndio uongozi (khasa). Na kama ukifuata matamanio yao baada ya yale yaliyo kufikia ya ujuzi (wa kweli) hutapata msaidizi yoyote wala mlinzi kwa Mwenyezi Mungu. Na kuongeza kuwa "Jambo lolote la Ibada hatuna ushirikiano wowote na wasio kuwa Waislamu", alisema Sheikh Hilal.

Umoja wa Waislamu na Wakristo Rufiji (UWAWARU) uliasisiwa mapema mwaka jana na wamisheni waliofika wilayani hapo (Rufiji) kwa kushirikiana na mheshimiwa Bakari Bonde.

Malengo ya umoja huo yameelezwa ni kujenga mahusiano mema miongoni mwa wananchi wilayani Rufiji.

Sheikh Hilal ambaye ni Mndengereko na mzaliwa wa Rufiji, alieleza kuwa kihistoria hakuna Mndengereko Mkristo na asilimia kubwa ni Waislamu.

Aliendelea kueleza kuwa wilaya ya Rufiji ni miongoni mwa wilaya zilizonyuma kimaendeleo nchini Tanzania bara.

Akielezea ni sababu zipi zinapelekea wilaya hiyo kuwa nyuma kimaendeleo alieleza kuwa ni udini na ubaguzi; "Kwa sababu Rufiji kuna Waislamu wengi, na kwa sababu hawakubali kugeuka ndio maana wanaachwa kama walivyo", alisema Sheikh Hilal.

Pia Sheikh huyo alishangazwa kuwa Rufiji nzima ni kijiji kimoja tu chenye umeme tena Ikwiriri, hivyo wana Rufiji hawana budi kujiuliza, "iko siri penye UWAWARU ndio penye umeme, sehemu alipozaliwa Waziri Mbonde hapana umeme, Mbunge Profesa Mikidadi hapana umeme kwa nini?" alihoji Sheikh Hilal.

Aidha, aliilezea Rufiji kuwa kuna Rufiji bara na visiwani na kwa ujumla ni sehemu yenye utajiri mkubwa. "Visiwani alipozaliwa Profesa (Mbunge) Juma Mikidadi Mtupa hupatikana kamba, mbao, boriti, chumvi hata meno ya tembo hupatikana huko", alisema Sheikh Hilal.

Akikamilisha maelezo yake aliwaasa wanachuoni wa Kiislamu watupie macho sehemu zenye Waislamu wengi na kuelezea kuwa Mtume (s.a.w.) alikuwa akiongea na wakubwa wa Kikuraishi waitwao (Sanaadii Quraysh) baadaye akatokea Sahaba (kipofu) Bw. Abdallah bin Umm Makhtum, akamwambia Mtume ee Mjumbe wa Mwenyezi Mungu nifundishe katika alichokufundisha Mwenyezi Mungu, lakini Mtume alimkunjia uso na kugeuka, Mwenyezi Mungu akaleta sura iitwayo Abbasa, hali ya kuwa anamlaumu Mtume wake kwamba amjali yule aliyekuwa Muislamu kuliko yule ambaye anamtarajia kusilimu.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook