KATIKA mfululizo wa makala hizi za wajibu wa kila mmoja wetu katika kusimamisha Uislamu. Katika makala yaliyopita tuliweza kuona nini wajibu wa wanafunzi katika kuendeleza Uislamu mashuleni. Na nia yetu makala ya leo iweze kufahamisha kwa uchache tu wajibu wa msingi wa wazazi na walezi katika kuhakikisha kuwa tunaandaa mazingira ya ksimamisha ukhalifa katika ardhi. Kama ambavyo Allah (s.w.) alivyobainisha lengo la kuumbwa kwetu. (Qur'an 2:30). Mwandishi wa makala haya SUKE KILAKALA anaeleza zaidi.
WAZAZI na walezi wa wanafunzi Waislamu wanawajibika kuufanya Uislamu ndio lengo la maisha yao. Wazazi na walezi wahakikishe kuwa wanarithisha lengo hili kwa hao wanaowalea. Mtume (s.a.w.) amesema kila mmoja ni mchunga na kila mchunga ataulizwa kutokana na lile analolichunga.
Kwa Hadith hii ya Mtume (s.a.w.) wale wote wenye jukumu la kuwalea watoto wa Kiislamu kama wazazi au walezi hawana budi kuwarithisha wale wanaowachunga Uislamu ili wasalimike mbele ya Allah (s.w.) siku ya kiyama.
Kwa kufanya Uislamu ndio lengo la maisha kutasaidia watoto kuendelea hivyo na hatimaye kukua wakijua nini cha kufanya hapa duniani. Tukifanya kinyume chake na kuishi kama wanyama, bila kujali hadhi yetu watoto wataiga na tutakuwa mas-uli mbele ya Allah (s.w.).
Wazazi wanatakiwa kujenga mazingira ya wanafunzi hawa kuishi Kiislamu toka nyumbani. Kinyume chake hivi kutokana na wazazi kutotekeleza wajibu wao wapo ambao Uislamu unakuwa ni miongoni mwa misamiati inayokita shuleni iwe ya Kiislamu au zile za serikali zenye walimu. Ni vipi tutajenga mazingira ya watoto kuishi Kiislamu toka majumbani kabla ya shule. Kwanza ni kwa wazazi au walezi wenyewe kujipamba na vipengele vya tabia njema, kutoruhusu mambo ya laghwi kufanyika nyumbani, kwa kudhibiti TV, radio na magazeti ya kitwaghuti. Kupendelea kuswali sunnah mbalimbali nyumbani na kuwahimiza watoto kuswali, kuhimizwa suala la kusoma Qur'an kwa mazingitio na kuhimiza utekelezaji wake hapo nyumbani. Maisha ya majumba yetu yawe yanaongozwa na Qur'an na Sunnah.
Wazazi wa wanafunzi Waislamu hawana budi kujenga tabia ya kufuatilia mienendo ya watoto wao kuanzia nyumbani mpaka shuleni wanakosoma. Kujua marafiki na watu gani ana uhusiano nao na kwa nini wawe na uhusiano. Mwanafunzi akionesha tabia mbaya aonywe mara moja bila kumchekea. Sambamba na hilo wazazi hawana budi kufuatilia maendeleo ya wanafunzi katika masomo shuleni na kuhakikisha kuwa akifanya vizuri kuwapongeza na kuwapa moyo na kuwarekebisha wanapofanya vibaya.
Walezi na wazazi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wao wanafundishwa elimu ya Kiislamu shuleni. Hili linaweza kufanywa kwa kuwatafutia mwalimu na pia kuwapatia vitabu vya kujisomea. Wahakikishe wanafundishwa kwa kutumia muhtasari na wanafanyiwa mtihani.
Wanafunzi wapewe huduma muhimu kama vile ya chakula iwapo shule ni ya kutwa na nauli ili kuepuka vishawishi ambavyo vinaweza kuwatoa katika maadili mema.
Mwisho ni wajibu wa wazazi na walezi
wa wanafunzi Waislamu kuwaenzi na kuwahifadhi walimu wa dini mashuleni.
Kwa ujumla kuwepo na utaratibu utakaowahakikishia waalimu wanaojitolea
kuhifadhiwa si kwa kuwasaidia bali kama ni wajibu wao wazazi ili watoto
wao walelewe Kiisalmu hata huko shuleni, iwe ni shule ya kutwa au ya bweni.
--
|
|