Viongozi waliokopeshwa mamilioni Pakistan kufikishwa mahakamani
 

Islamabad

SERIKALI ya kijeshi ya Pakistan inatazamia kuwafikisha mahakamani viongozi wa serikali iliyopinduliwa nchini humo kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma, rushwa na uendeshaji mbaya wa nchi.

Hatua hiyo inafuatia viongozi hao kushindwa kulipa madeni yanayotokana na mikopo waliyojikopesha wakiwa madarakani katika muda maalum uliowekwa na serikali hiyo ya kijeshi.

Habari kutoka nchini humo zinaeleza kuwa operesheni ya kuwakamata watuhumiwa iliendeshwa katika miji ya Islamabad, Pushawar, Punjap na Karachi.

Viongozi kadhaa wa serikali iliyopinduliwa akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Bwana Nawaz Sharrif wako mbaroni hivi sasa kufuatia ubadhilifu ambao imedaiwa umeisababisha Pakistan kuwa katika hali ngumu kiuchumi.

Aliyekuwa Waziri Mkuu kabla ya Bwana Sharrif, Bibi Benazir Bhuto ni miongoni mwa watu wanaotakiwa kujibu mashitaka hayo.

Hata hivyo, Bibi Bhuto hivi sasa yuko uhamishoni nchini Uingereza.

Serikali ya kiraia ya Pakistan ilipinduliwa mwanzoni mwa mwezi uliopita kufuatia kutoelewana kati ya Waziri Mkuu na jeshi la nchi hiyo.

Kutoelewana huko kulisababishwa na mambo kadhaa yakiwemo ya uendeshaji mbaya wa nchi na suala la Kashmir.

Mkuu wa nchi hiyo ambaye ndiye kiongozi wa mapinduzi hayo Jenerali Parwez Musharraf amemlaumu Bwana Nawaz kwa kuangusha uchumi wa Pakistan na kuwa msimamo unaoyumba kuhusu suala la Kashmir.

Bwana Musharraf ana msimamo unaoelekea kuwasaidia Waislamu wa Kashmir dhidi ya unyama unaofanywa na serikali ya India.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook