Uandikishaji kura serikali za mitaa haufai - Wananchi
 

BAADHI ya wakazi Jijini wameelezea kuwa zoezi la uandikishaji kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa kuwa halifai.

Wakiongea na mwandishi kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam, wakazi hao wameeleza dosari katika zoezi zima la uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Bw. Mohamed Naringa mkazi wa Kigiragira ameeleza kuwa utaratibu uliowekwa na serikali wa waandikishaji kupita majumbani nyakati za mchana wakati watu wengi wako katika pilikapilika za kutafuta mahitaji yao muhimu, una lengo la kuzuia baadhi ya watu kwa maslahi ya chama fulani.

"Utaratibu huu unawakosesha wengi haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowahitaji", alisema Bw. Mohamed.

Nae Bwana John Mtupa wa Kinondoni amehoji mantiki ya serikali kuendesha zoezi hili kwa kuwapitia watu majumbani.

"Serikali inakusudia nini katika zoezi hili, kama wamekusudia kutupitia majumbani mwetu waje basi usiku ili watukute nyumbani kuliko kupita mchana wakati tuko makazini", alisema Bw. Mtupa.

Bw. Mohamed Naringa ambaye mpaka sasa hajajiandikisha kutokana na mizunguko yake, anaeleza kuwa kuna uwezekano wa watu wengi kutoandikishwa kwa ajili ya uchaguzi huo.

Wakazi hao wameeleza kuwa serikali isione uzito kuweka vituo vya kuandikisha wapiga kura ili kila mtu (mwananchi) apate haki yake ya kuchagua viongozi wanaowataka.

"Serikali iweke vituo vya kuandikisha wapiga kura ili kila mwananchi kwa wakati wake aweze kujiandikisha, kuliko kuendelea na zoezi lililopo hivi sasa kwani watu wengi hawajajiandikisha kwa kutokuwepo nyumbani", alisema dada mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwajuma mkazi wa Mbagala Kizuiani.

Zoezi la uandikishaji lilianza mapema mwezi Oktoba, baadaye kuahirishwa kufuatia kifo cha Mwalimu Nyerere.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook