Alisema kwamba kama Watanzania wataendelea na tabia yao ya kufurahishwa na kila jambo linalofanywa na viongozi wao, wakitanabahi watakuta nchi yao imeuzwa na wao wakitabasamu.
"Watanzania mtakasirika lini?", alihoji Mhe. Cheyo, akishangaa wananchi kukaa kimya huku mali ya umma na kodi zao zikihujumiwa.
Alitaja tukio la hivi karibuni ambapo Taasisi moja isiyo ya kiserikali (NGO) imejiingiza katika biashara isivyo halali na kwa kutumia fedha ya umma.
Taasisi hiyo inayoitwa Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote inaongozwa na Mke wa Rais, mama Anna Mkapa.
"Ilikuwaje chama kisicho cha kiserikali kinachojiita fursa sawa kwa wote (EOTF) ambacho kisheria si chama cha kujipatia faida kikawa kinafanya biashara ya kupangisha nyumba iliyo mali ya Benki ya Taifa ya Biashara", alihoji.
Bw. Cheyo alimtaka Mhe. Rais alieleze Taifa juu ya jambo hili.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa mfuko wa fursa sawa kwa wote (Equal Opportunities for All Trust Fund) unaoongozwa na Mama Anna Mkapa umeuziwa jengo la NBC.
Lakini kabla ya kukamilisha malipo kwa NBC, mfuko huo ukalikodisha jengo hilo kwa National Bureau de Change (taasisi ya umma).
Imedaiwa kuwa tayari taasisi ya Mama Anna Mkapa imelipwa shilingi 481.2 milioni kama ada ya pango.
Hayo yanafanyika wakati jengo hilo bado kisheria ni mali ya NBC Holding Corporation.
Katika hali ya kushangaa, Mhe. Cheyo alihoji vipi hujuma zinazofanyika leo hazisemwi wakati Mama Sitti Mwinyi aliandamwa, bila hata hayo makosa yake kuthibiti.
Kuhusu mchango wa Wabunge wa upinzani kuwatetea wananchi, Mhe. Cheyo alieleza kuwa nguvu ya Wabunge hao ipo kwa wananchi. Kama wananchi wenyewe wamelala mchango wa Wabunge hausaidii.
Akifafanua alisema lau wananchi wanajitokeza kwa maelfu kudai haki zao serikali haiwezi kuwakwaza.
Akitoa mfano wa wafanyakazi wa iliyokuwa
Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaodai mafao yao alisema alitarajia wafurike
kwa maelfu katika ukumbi wa Bunge suala lao lilipokuwa linazungumzwa, lakini
badala yake walikuwepo watu watano tu.
--
|
|