MMOJA wa washitakiwa katika kesi zinazokabili Waislamu kuhusiana na kadhia ya Mwembechai, amefariki dunia.
Hamad Salum (23) aliyekuwa mkazi wa Manzese jijini alifariki na kuzikwa eneo hilo hivi karibuni.
Kwa mujibu wa jamaa wa karibu, marehemu kabla ya kifo chake alianza kuugua mara tu baada ya kutoka rumande.
Yeye na watuhumiwa wengine 11 katika kesi Na. 192/1998 waliwekwa mahabusu miezi kadhaa katika gereza la Segerea.
Kifo cha kijana huyo kinafanya idadi ya watuhumiwa waliofariki baada ya kutoka gerezani kuwa wawili hadi sasa.
Awali alifariki aliyekuwa Imamu wa Msikiti wa Mtambani marehemu Mzee Chata Abdallah Kidagaa ambaye naye aliwekwa mahabusu gereza hilo.
Mshitakiwa Salum ni miongoni mwa watu waliokamatwa katika msako maalum ulioendeshwa na polisi siku chache baada ya tukio la Mwembechai.
Wakati huo huo kesi Na. 192/1998 inayowakabili Waislamu 12 katika shauri la Mwembechai imeahirishwa hadi Novemba 29, mwaka huu.
Kesi hiyo ambayo sasa imebakiwa na washitakiwa 11 baada ya mmoja kufariki dunia ilifunguliwa na Jamhuri mwaka wa jana katika mahakama ya Kisutu Jijini.
Tangu wakati huo imekuwa ikitajwa na kuahirishwa inakaribia kufikia miaka miwili sasa.
Mbali ya kesi hiyo, kesi nyingine mbili kuhusiana na tukio hilo hilo nazo halidhalika zimeendelea kupigwa tarehe mara kwa mara.
|
|