CHUKI Athumani ameomba aonewe huruma na kusaidiwa.
Akiwa bado na imani ya kupona anahisi akipatiwa matibabu stahiki anaweza kutembea.
"Nimekuwa mpweke sana na najiona kama nimetengwa na jamii; hasa Waislamu. Kwa jinsi ninavyopata maumivu kwa kweli nahisi kuwa Waislamu mmenitupa mkono", amesema Chuki katika barua yake kwa Amir wa Shura ya Maimamu, Sheikh Juma Mbukuzi.
"Siwezi kuamini kama ndivyo Waislamu tulivyo", aliongeza.
Kuhusu hali yake amesema kuwa uchunguzi wa daktari umeonesha kuwa anaweza kupona lakini serikali haijaonesha azma ya kumpeleka nje kwa matibabu.
Alisema kwenda nje kwa matibabu kuna gharimu fedha nyingi ambazo familia yake haiwezi kumudu.
Katika hali hiyo amewataka Waislamu wamsaidie kwani uwezo huo wanao.
Aidha, amemuomba Sheikh Juma Mbukuzi Amir wa Shura awe anamtembelea ili ajue maendeleo ya hali yake.
Gazeti hili liliwasiliana na Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu juu ya jambo hili ambapo limeahidi kulifuatilia.
Kaimu Katibu wa Baraza hilo Sheikh Samatta amesema kuwa Baraza litafanya vikao hivi karibuni na kutizama lipi laweza kufanyika.
Chuki Athumani (18) ni miongoni mwa waathirika wa Mwembechai.
Alipigwa risasi Februari 13, 1998. Risasi iliathiri sehemu ya mishipa ya fahamu katika uti wa mgongo.
Alifungwa pingu kitandani bila ya matibabu hadi akapooza. Hivi sasa miguu yake haifanyi kazi.
Ni katika tukio hilo ambapo Waislamu kadhaa waliuliwa na wengine kufia mikononi mwa polisi.
Aidha wapo walioathirika afya zao wakiwa ndani kama mzee Chatta na kufa muda mfupi baada ya kuachiwa.
Mpaka hivi sasa serikali haijaonesha dalili yoyote ya kukubali kuundwa kwa tume ya kulishughulikia suala hili, na kuwafikisha wauaji mahakamani.
|
|