IMAMU wa Msikiti wa Manyema Jijini Sheikh Jongo na aliyekuwa Katibu wa Bakwata Bwana Adamu Nasibu wamejikuta wakiwa katika wakati mgumu mjini Kigoma baada ya makundi ya vijana kuwazomea mitaani.
Mabwana hao ambao walifanya ziara isiyo rasmi mjini hapa hivi karibuni, walikabiliwa na mkasa huo kufuatia hotuba ya Sheikh Jongo katika Msikiti wa Shauri Moyo eneo la Mwanga.
Katika hotuba yake, imedaiwa Sheikh Jongo alidai kuwa serikali haiwachukii Waislamu isipokuwa Waislamu ndio wanaowachukia viongozi wa serikali.
Aidha, alidai kuwa Masheikh na viongozi wa Kiislamu wanaokamatwa hawakamatwi kwa sababu ya Uislamu wao bali kwa chuki zao dhidi ya viongozi wa serikali.
Kauli hiyo iliibua maswali kadhaa miongoni mwa waumini waliokuwa wakimsikiliza ambapo baadae muumini mmoja alisimama na kuwaambia wengine kuwa huyo aliyekuwa akiongea ndiye Sheikh Hamid Jongo wa Msikiti wa Manyema Dar es Salaam.
Kufuatia tukio hilo taarifa za kuwepo kwao hapa zilizagaa mji mzima hali iliyopelekea makundi ya vijana kufuatilia mizunguko yao huku wakiwazomea.
Imeelezwa kuwa baadhi ya mambo waliyoshulikia wakiwa mjini hapa ni pamoja na kulitangaza Baraza la Maimamu na kujaribu kuwasuluhisha Masheikh maarufu mjini.
Ziara ya viongozi hao iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa kampeni za Ubunge za CCM uliofanywa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, imezua maswali kadhaa miongoni mwa waumini na Masheikh.
Baadhi ya waumini wamedai kuwa huenda
hayo ni maandalizi kuelekea ucahguzi mkuu mwaka 2000.
--
|
|