Malipo ya wazee wastaafu mashakani
 

WAZEE wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameitaka serikali iwape haki zao badala ya kuendelea kuwazungusha.

Wazee hao wamesema malipo hayo si hisani ya serikali bali jasho lao ambalo kuendelea kulizulia ni dhulma.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ilivunjika mwaka 1977 baada ya viongozi wakuu wa nchi husika kutofautiana kisiasa.

Mashirika yaliyokuwa chini ya Jumuiya hiyo ni pamoja na Reli, Bandari na Ndege.

Nchi zilizounda umoja huo ni Tanzania, Kenya na Uganda ambapo makao yake makuu yalikuwa Nairobi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wastaafu wa jumuiya hiyo upande wa Tanzania wameshutumu "danadana" wanayopigwa na serikali wakati wenzao wa Kenya na Uganda walishalipwa mara tu baada ya kuvunjika kwa jumuiya.

Mzee Ramadhani Abdallah aliyekuwa mfanyakazi wa Bandari Dar es Salaam ametuhumu kuwa huenda kinachoifanya serikali izuie haki yao ni kuona kuwa wastaafu wengi ni Waislamu.

Aidha, Mzee alidai kuwa kila wanapofuatilia haki yao hiyo haumbiwa wao ni wafuasi wa chama cha CUF kwa hiyo wasitegemee kupata chochote. Hata hivyo hakueleza ofisa gani katoa madai hayo.

Mzee Abdallah aliyasema hayo Jumapili iliyopita katika Msikiti wa Mtambani wakati akielezea historia ya uhuru wa Tanganyika.

Naye Mzee Ali Abbas mkazi wa Kariakoo amesema inashangaza kusikia serikali inawaheshimu wazee wakati ambapo inaendelea kuwalaghai kuhusu malipo yao.

"Huku ndiko kuwaheshimu wazee haya si yale yale yanayofanyika Shinyanga tofauti hawa wanawaongopea kwa njoo kesho wale wanawaua", alizungumza kwa hasira mzee huyo maarufu jijini.

Kutoka Morogoro mwandishi wetu anaripoti kuwa baadhi ya wazee wastaafu wa jumuiya hiyo wameingiwa na wasiwasi juu ya uwezekano wa kulipwa haki zao.

Mzee Hussein Swaleh aliyekuwa mfanyakazi wa shirika la Reli ameliambia AN-NUUR kuwa tangu yatoke majina ya watakaolipwa wamekuwa wakifuatilia malipo yao bila ya mafanikio.

Mzee huyo ambaye alistaafu mwaka 1988 baada ya kufanya kazi katika Shirika hilo kwa miaka 35, amesema mara zote wamekuwa wakiambiwa hundi zao zinatayarishwa na kwamba wangefahamishwa baadae.

"Huu ni mwezi wa sita sasa tangu tuanze kufuatilia, sasa watueleze nini wanachokusudia kuhusu malipo yetu haya", alilalamika mzee huyo.

Wakati akihojiwa na chombo kimoja cha habari cha nje, msemaji wa Hazina alisema mpaka sasa ofisi yake imeshawalipa wastaafu wasiopungua 700 na kwamba zoezi hilo linaendelea.

Baadhi ya watu Jijini Dar es Salaam wameitaka serikali iwalipe wazee hao ili kuiepusha nchi na majanga yanayoweza kusababishwa na kudhulumu haki za watu.
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook