UMOJA wa Mataifa ulipitisha mkataba wa haki za watoto ambao haki zilizoanishwa ni zaidi ya ishirini ili kumlinda mtoto asinyanyaswe na kukoseshwa haki zake za msingi kama vile kupata elimu, matunzo na kadhalika.
Hata hivyo umri wa mtu anayeitwa mtoto kisheria unatofautiana kutokana na mahali na mazingira, lakini tunaweza kukubaliana kuwa mtoto ni kuanzia umri 0 hadi 18.
Lakini tunapokubali kwamba mtu fulani ni mtoto pia kimsingi tunakubali kwamba anastahili kuhudumiwa kichakula, kimavazi na kadhalika.
Inapotokea mtoto mazingira yakamlazimisha kumfanya yeye ndiye mtafutaji riziki bado ukweli utaendelea kubaki kuwa mtoto huyo amekosa haki yake ya kutunzwa.
Ajira ya watoto ni tatizo sugu la nchi nyingi zinazoendelea, sababu kubwa ni kipato duni cha familia.
Katika jamii ambazo wakubwa wameathiriwa na ugonjwa wa ukimwi, watoto ndio wahudumiaji maalum wa familia hizo.
Katika familia ambazo wazazi wameangamizwa na vita, watoto wanapaswa kubeba majukumu.
Na mara nyingine hata katika familia za kawaida tu, watoto hulazimika kufanya kazi ili kuongeza pato la familia.
Naweza kusema kuwa mara nyingine si hiari ya wazazi kuwaruhusu watoto wao kufanya kazi bali mazingira huwalazimisha kufanya hivyo.
Mtoto Amina (12) mkazi wa Manzese kwa Mfuga Mbwa analazimika kila siku baada ya masomo kubeba kikapu cha karanga. Mama Amina, Bi. Sikudhani Ramadhani ana watoto sita, Amina akiwa ndiye mkubwa na wote wanamtegemea yeye kwani mumewe alimtekeleza na watoto baada ya kupata kimwana mwingine Kichinchiri.
Bi Sikudhani kila siku huamka saa 10 alfajili kwa ajili ya kuchoma maandazi ambayo faida yake kwa siku ni shilingi 500 tu na siku nyingine humdodea.
Amina anaporudi shule hulazimika kumsaidia mama yake kuuza karanga ili angalau kuongeza kipato cha familia yao.
Katika mazingira kama hayo tutamlaumu vipi mama Amina kwa kumtumikisha mtoto?
Ya Amina angalau ni kazi nyepesi kuna watoto wanaofanya kazi migodini kwa ujira mdogo, kuna watoto wanaolazimika kushika nyundo na kupasua mawe ili wapate senti mbili tatu za kuwasaidia wao na familia zao baada ya kuuza kokoto.
Watoto kama hao wanaofanya kazi za sulubu zenye ujira mdogo tatizo lao si dogo kiasi cha kuliegemeza katika ngazi ya familia tu bali tatizo la watoto kama hao linapaswa kushughulikiwa kitaifa.
Wakati wa sera za elimu bila malipo tatizo la ajira za watoto na watoto wa mitaani lilikuwa halijajitokeza kiasi cha kukera lakini katika zama hizi za uchangiaji wa huduma zote muhimu kama vile elimu, afya na maji safi, watoto wengi hulazimika kujiingiza katika ajira ndogo ndogo ili wajipatie chochote.
Enzi za elimu bila malipo si aghalabu kumkuta mtoto nyakati za kwenda shule ananing'ia kwenye daladala akipiga debe na kujipatia shilingi 100 kwa kila basi atakalolijaza.
Zama za elimu ya kujitegemea watoto walikuwa wakipewa ujuzi wa mikono ili waweze kujitegemea wamalizapo elimu ya msingi.
Tunapowakebehi watoto ombaomba mabarabarani huwa tunamkebehi nani? Bila shaka huwa tunajikebehi sisi wenyewe na tunalikebehi taifa,
Baada ya kukosa cha kufanya (kwa kuwa hawaendi tena shule kwa sababu mbalimbali) watoto hulazimika kutafuta kazi ya kufanya ili angalau waweze kupata kijio chao na cha familia zao, hapo huwa liwalo na liwe ama awe mpiga debe, muuza karanga, ombaomba, wizi wa mifukoni na hata uasherati. Je, hilo bado ni la kufumbia macho?
Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Watoto, wanawake wanataka kuona vitendo na wala si maneno!
|
|