Huwezi kuingia peponi kwa kuzikwa na watu wengi
Ndugu Mhariri
NATOA masikitiko yangu juu ya kauli ya Rais Mkapa kugawa pepo kama vyeo vya kiserikali.
Hayo yalifanyika siku ya kumaliza maombolezo ya msiba wa Mwalimu Nyerere. Alisema kuwa "Nimeambiwa katika Qur'an kuwa mtu akizikwa na kuombewa na watu wengi ataingia peponi". Maneno hayo siyo ya kweli kwani hakuna aya ndani ya Qur'an inayosema hivyo.
Jingine ni kwamba kwa mujibu wa Uislamu kuzika ni jambo linalokusanya matendo manne; kuoshwa maiti, kisha kukafiniwa (kuvikwa sanda), baadae kusaliwa na hatimaye kulazwa kaburini kwa utaratibu ulioelekezwa. Mkusanyiko wa haya yote ndiyo huzaa istilahi ya "kuzika". Kinyume na utaratibu huo nje ya dharura za kisheria, maiti huwa imefukiwa.
Ni lazima Rais afahamu kuwa Uislamu ni tofauti na dini zingine, kwani Uislamu hauendi kwa matakwa ya mtu au fikra za mtu kama dini zingine zilivyo.
Jumanne Mussa,
Mwanza.
Ndugu Mhariri
NACHUKUA fursa hii kuzungumzia mapesa yaliyochangwa na wananchi yakikusudiwa kuwa ni rambirambi kwa hayati Mwalimu Nyerere.
Baadhi ya viongozi wametamka kuwa pesa hizo zitajengwa minara ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere. Ninahakika kuwa mia kwa mia, huku ni kufuja pesa za wananchi. Ni minara mingapi iliyojengwa wakati Mwalimu Nyerere mwenyewe yuko hai ambayo hadi sasa ina hali nzuri? Kuna uhuru, kuna ya Azimio la Arusha, nikitaja michache. Je, mmeiona baadhi yake ilivyo sasa hivi?
Pendekezo langu ni kwamba pesa hizi ambazo zitafikia mabilioni iwapo hesabu zitatolewa kwa usahihi, kwani kufa kufaana, zitumiwe kujengea vituo vya huduma kwa jina Mwalimu Nyerere. Nchi inahitaji hospitali bora kama ya Mtakatifu Thomas. Nchi inahitaji vyuo vikuu vizuri kama cha Edingburg. Tunahitaji madaraja ya kuunganisha kijiji hadi kijiji kama Moi Bridge-Mombasa.
Tunahitaji viwanja vizuri kama Jomo Kenyatta International Airport, tunahitaji barabara za kisasa kutoka Amboni hadi Horohoro - barabara hii madaraja yake yote mabovu.
Daraja la Choba - Pangani tangu mvua za El-Nino mpaka leo halijafanyiwa ukarabati. Tunahitaji barabara za kisasa kutoka Kibiti hadi Utete, kutoka Utete hadi Kilwa kupitia Nyamwage. Zote hizi ziitwe Nyerere.
Hapo ndipo wananchi watakuwa na kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ya milele. Mfano mzuri wa kumbukumbu yenye faida kwa wananchi ni Sokoine University of Argriculture - Morogoro.
Hassan B. Kisuwah,
S.L.B. 1542,
TANGA.
Ndugu Mhariri
HAKIKA hali iliyo katika Jiji la Dar es Salaam ni ya kusikitisha sana, kwani kila kona unayokatisha katika Jiji hili inanuka pombe. Kila mtaa haukosi Baa au Groceries.
Na wakati huo huo mabarabara na mitaa mbalimbali imepambwa kwa mabango yanayotangaza aina mbalimbali za pombe na sifa zake, kwa kweli Jiji hili limechafuka na linanuka! Kutokana na hali hii Tanzania inavifundisha nini vizazi vijavyo na watoto wadogo wanaoinukia?
Sasa kimefika kipindi ambacho mtoto anakuwa katika mazingira yanayomuonesha kuwa hakuna kitu kizuri kama pombe, kwa sababu kila apitapo anaona pombe imepambwa kwa sifa nzuri sana kuliko vyote anavyoviona.
Kwa kweli mazingira ya namna hi yatawapelekea watoto wetu kutumbukia katika ulevi wa kupindukia.
Na matokeo ya haya yote ni nchi kukosa muelekeo, kwa sababu walevi watupu ndio watakaokuwa madarakani.
Ndugu Mhariri
NAOMBA usinitie kapuni ili nami niwajibike katika kuosha akili zetu sisi Waislamu.
Kama inavyodaiwa kwamba Mwalimu J.K. Nyerere ameleta amani, mshikamano, utulivu, uvumilivu, uelewano na si utengano na udini. Ikiwa hivyo ndivyo, sasa nauliza jina la mji mkuu wa Tanganyika kabla Mwalimu Nyerere hajajiunga na TAA lilikuwa ni lipi?
Maana neno Dar es Salaam ni lugha ya Kiarabu wala si la Kiingereza au Kijerumani lenye maana ya nyumba ya amani. Kwa maana Dar-nyumba, 'es' ya na 'salaam' - amani. Kama ilivyo St. Francis-Mtakatifu Francis kwa Wakatoliki pamoja na St. Thomas - Mtakatifu Tomasi.
Hata hivyo waumini tuongezeni juhudi kubwa katika dua zetu, itikafu, tawasul, twayibal asmaau na kadhalika ili wale wote wanaoichukia dini ya Allah na kuwafanyia mabaya waja wake, basi yeye Allah ajue cha kuwafanya. Kuna dalili kubwa za kupokelewa dua zetu.
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi kupitia gazeti letu la AN-NUUR nipate kukumbushia.
Nikiwa na majonzi, pamoja na huzuni kuhusu ndugu zetu waliouliwa Mwembechai bado tunazidi kuikumbushia serikali kuhusu kuunda tume huru ya kuchunguza mauaji ya Mwembechai, ikizingatiwa kuwa serikali hii ni ya uwazi na ukweli kama inavyotangaza kufanya hivi ni kuimarisha amani katika nchi yetu kwani damu za Waislamu hazimwagiki bure bure.
Ndugu Mhariri,
NACHUKUA fursa hii ili kuaomba Maimamu wote Tanzania bara na visiwani watizame uwezekano wa kuanzisha mpango wa kuhamasisha Waislamu kuchangia na kugharamia elimu kwa vijana wetu ambao wengi wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na wazazi au walezi wao kushindwa kumudu gharama za masomo.
Tatatizo hili linazidi kukua na kuelemea maendeleo ya Waislamu hasa tukizingatia hali ya maisha inavyozidi kuwa mbaya siku hadi siku.
Wazo ninalolileta kwenu ili mlitafakari na kuliendeleza ni la Misikiti kujipa wajibu wa kutafuta fedha na kuwadhamini vijana wa Kiislamu kwa masomo na mafunzo, kwa kuwatafutia nafasi za shule na vyuo na kuwagharamia.
Mawazo yangu ni kuwa zikiunganishwa nguvu za Misikiti na za wazazi kasi ya kuwainua vijana wa Kiislamu kielimu, kiujuzi na kimaendeleo itaongezeaka sana.
Pili, kwa vile Misikiti ndiyo mahali wanapokutana Waislamu kwa wingi mara kwa mara na kutoa sadaka kwa ajili ya Uislamu, basi Misikiti ibuni kasma maalum ya kusomesha na kufunza vijana itakaochangiwa na sadaka za kawaida za kila siku za waumini wanaofika Misikitini na pia kwa vile Maimamu majukumu yao hayaishii Misikitini tu, kasma hizo za masomo na mafunzo wazitangaze na nje ya Misikiti ili Waislamu wengi na wahisani wachangie.
Wazo hili si geni katika jamii yetu. Iko baadhi ya Misikiti nchini ambayo tayari inatekeleza suala hili kivitendo na kwa ufanisi. Kwa mfano Msikiti Mkuu wa Ijumaa -Boma Road, Morogoro umeanza na unaendelea na zoezi hili vizuri. Kwa rekodi za miaka mitatu tu iliyopita (1996-98) Msikiti umesomesha vijana 8 katika shule za sekondari na vyuo. (Mzumbe , Tambaza , Morogoro , Kigurunyembe na Chuo cha Ualimu Morogoro ).
Japo itaonekana kuwa ni idadi ndogo lakini ni wazi kuwa ikiwa Misikiti 1,000 nchini kila mmoja ungegharimia idada kama hiyo kwa kipindi hicho taasisi ya Msikiti peke yake ingekuwa imetoa mchango wa kufunza vijana 8000.
Hivi sasa uongozi wa Msikiti huo unatafuta fedha na unachambua na kupima sifa za vijana walioomba kudhaminiwa masomo yao na Msikiti ili uwalipie kwa mwaka huu wa masomo unaoendelea. Msikiti huu hivi sasa umepata uzoefu ambao Misikiti mingine ambayo haijaanza utaratibu huu ingeweza kujifunza na hata kuiga kwa nia ya kuupa Uislamu maendeleo ya haraka.
Natumaini kuwa wazo hili mtaliona la kufaa na mtawawasilishia waumini na kwa uwezo wenu wa uongozi na uchu wa maendeleo ya Waislamu mtahimiza kwa nguvu zote utekelezaji.
Mwisho kabisa naomba wito huu kwa ninyi viongozi wetu uwe umefungua mawasiliano baina ya Misikiti, Maimamu na Waislamu kwa ujumla kuungana kuchangia maendeleo ya elimu kwa faida ya Uislamu na Taifa kwa jumla.
Sheikh Sleyum Ali,
S.L.P. 444, Morogoro.
|
|