MASHAIRI
 

Aka!!
 

Sijasema ni kwa nini, na wala sijakataa,
Ni sababu sizioni, hunifanya kuduwaa,
Wala sipo ugenini, ni nyumbani Tanzania,
Cha kuenzi kitu gani, nabaki ninashangaa!!

Nasikia redioni, na kwenye hotuba pia,
Huko Dodoma bungeni, mwito wanatutolea,
Haya shime muenzini, mengi alotutendea,
Aka! Haya mageni, naachwa kwenye mataa.

Ni kipi kikubwa kwani, kwa macho katukazia,
Vibwebwe vikiunoni, kuenzi kututishia,
Shime nielewesheni, debe nitampigia,
Wataenzi walopwani, bara wataitikia.

Wasomi wa Mlimani, mwauenzi ujamaa?
Mbona haupo nchini, zamani ulijifia!!
Ulijikwaa doleni, ukaangukia pua,
Pameshaota majani, lipozikwa ujamaa.

Tulikuwa misibani, vijiji vya ujamaa,
Si wakimbizi vitani, makazi kuyakimbia,
Simba kala themanini, nani asiyeyajua!!
Kipo wapi nambieni, kijiji cha ujamaa?

Mimi ndiye mjivuni, kwa kuenzi ni shujaa,
Kwa hili nipo pembeni, aibu naichelea,
Elimu yetu ni duni, takwimu zinatwambia,
Aliyeasisi nani, Azimio la Musoma?

Eti shule anzisheni, elimu kuwagawia,
Walimu akina nani, hawa walojishindwia!!!
Wangetufundisha nini, yale wasiyoyajua?
Tusingekwenda London, homa tukijisikia!

Kiswahili ni utani, hayo mnotuimbia,
Kilikuwepo nchini, tangu kale asilia,
TUKI kweli isemeni, sitaki kukodolea,
Uongo ulo sheheni, kama rushwa Tanzania.

Tumemtoa Amini, Uganda amekimbia,
Kwa ubavu namba wani, twaogopwa Tanzania,
Siku mbili jifungeni, hali ngumu meingia,
Makatambuga vaeni, na mikoba ya gunia!!

Uganda tembeleeni, linganisha Tanzania,
Avinjari Museveni, Uganda yaendelea,
Huku tuso na udini, hali mbaya yatishia,
Amefaidika nani, naachwa kwenye mataa.

Muungano dumisheni, na vitisho wavitoa,
Wakishuka jukwaani, tembo maji hulitia,
Sasa magari ya nini, ya Zanzibar mwakataa,
Fumbomwamfumbiani, Nolo nimeshitukiaaaa!!!

Aka! Sasa nambieni, kabla sijakataa,
Kuenzi kisicho mboni, ni shubir si halua,
Hasa mlo ufukweni, jipu hili lipasua,
Nolo nitaenzi nini, kalamu naiachia.

Luanda K.S. (Nolo), Dar es Salaam.
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook