Utatuzi wa mashauri ya jinai nje ya mahakama Tanzania
 
Dk. Abdallah J. Saffar

KATIKA miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la makosa ya jinai nchini Tanzania Bara. Jambo hili limesababisha kujaa kwa mahabusu na magereza ambayo yameshindwa kuhimili wimbi la watuhumiwa na wafungwa. Matokeo yake kumekuwa na upungufu mkubwa wa huduma za chakula, afya na malazi mambo ambayo yameleta madhila makubwa. Baya zaidi ni kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa mahabusu watoto ambao wamekuwa wakilawitiwa na mahabusu au wafungwa waliokubuhu.

IDADI kubwa ya mahabusu hawana mawakili jambo ambalo huchangia katika kukosa dhamana. Isitoshe aghalabu mashauri ya jinai huchukua muda mrefu kumalizika.

Pia imedhihirika kwamba karibu asilimia hamsini (50%) ya watu hutiwa hatiani kwa makosa (Dakta Abdallah J. Saffari, Human Rights in the Criminal Process with Reference to Tanzania Mainland, DPhil Thesis, University of Sussex, England, 1994). Na bahati mbaya Tanzania haina utamaduni wala sheria inayoilazimu serikali kuwafidia wafungwa ambao walitiwa hatiani kwa makosa.

Azma ya makala haya ni kutafuta namna bora ya kutatua mashauri ya jinai nje ya mfumo wa mahakama ili kuepuka matatizo yaliyoelezwa hapo juu.

Tatito

Jitihada kubwa imefanywa duniani kote na hivi sasa hapa Tanzania kutatua mashauri ya madai nje ya Mahakama (Mfano mzuri ni 'Alternative Dispute Resolution' (ADR), utaratibu unaotumika nchini Marekani. Hivi sasa wataalam kutoka Marekani wanasaidia kuutumia utaratibu huu katika mahakama hapa nchini.). Njia mbalimbali zimetumika kama vile usuluhishi, majadiliano na mapatano. Pia ni dhahiri sheria za Tanzania na taasisi zote za huduma za uwakili kama vile Chama cha Mawakili cha Tanganyika, Kamati ya Msaada ya Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chama cha Mawakili Wanawake Tanzania hutoa huduma kwa wanaohusika na mashauri ya madai.

Kwa bahati mbaya hakuna utaratibu wala jitihada iliyofanywa kutatua mashauri ya jinai nje ya mahakama licha ya athari zinazowakabili mahabusu.

Mambo muhimu

Yako masuala matatu ya kuzingatia kutafuta namna muafaka ya kutatua mashauri ya jinai. Kwanza ni kuainisha makosa ya jinai; pili chanzo cha makosa hayo na tatu misimamo ya pande zinazohusika katika uendeshaji wa mashauri ya jinai.

Aina ya uzito wa makosa ya jinai

Kanuni ya Adhabu ya Tanzania imegawanya makosa ya jinai katika aina mbalimbali. Lakini aina kuu ni makosa dhidi ya serikali kama vile uhaini na ujajusi; makosa yanayohusiana na mali kama vile wizi, makosa yanayokiuka itikeli mathalan kulawiti na kubaka; na makosa dhidi ya mwili kama vile mauaji ya kukusudia na yasiyo ya kukusudia pamoja na ujambazi.

Ukiachilia mbali takwimu za hivi karibuni zinazoonesha ongezeko la makosa ya itikeli, idadi kubwa ya mashauri ya jinai yanahusiana na mali hususan wizi. Mbali na makosa ya wizi kumekuwepo na ongezeko la makosa mengine dhidi ya sheria ndogo na hata kubwa. Mfano ni uzururaji yaani kutokuwa na maskani na ufanyaji biashara bila leseni.

Dhahiri basi kwamba ainisho la makosa ya jinai linaonesha kuwa baadhi yake ni mazito zaidi ya mengine. Hivyo aina ya adhabu inayotolewa hutafautiana kutokana na uzito au wepesi wa kosa lenyewe. Kosa kubwa huwa na adhabu kali zaidi kuliko kosa dogo. Na kwa Muktadha huu huu aina ya kosa pi huathiri utoaji dhamana. Kwa kawaida mahakama huweka masharti magumu zaidi kabla ya kutoa dhamana mintaarafu ya makosa makubwa kuliko yale madogo.

Muhimu vile vile ni kuwa ainisho la makosa madogo na makubwa linasaidia kuamua kuanza kutatua yale ambayo ni rahisi. Sisi tunaamini kwamba hakuna faida inayopatikana kwa kumfunga mzururaji, mchuuzi asiye na leseni au mwizi wa kitu chenye thamani ndogo. Na pengine pia hakuna faida kumfunga mwizi aliyeiba mali ambayo tayari imepatikana. Kinyume chake ni kuwa madhara ya kufanya hivyo ni makubwa sana kwa mkosaji na taifa lake kwa ujumla. Kwa kifupi mkosaji (hususan mtoto) ana uwezekano mkubwa wa kunyanyaswa na kudhalilishwa kifungoni. Pia huweza kugeuka nunda. Yaani kifungo humuandaa kwa uhalifu mkubwa zaidi. Kwa upande mwingine taifa huchangia kumharibu mfungwa mtoto na pia kutumia fedha nyingi kwa huduma za magereza.

Chanzo cha makosa ya jinai

Suala la chanzo cha makosa ya jinai limejadiliwa duniani kote. Ukweli ni kwamba mazingira ya kiuchumi huchangia mno katika suala hili. Makosa kama vile wizi, uzururaji na uporaji na hata aina fulani ya mauaji ni matokeo ya kushindwa kwa serikali tawala na taasisi zake kukidhi mahitaji ya raia wake katika masuala muhimu kama vile chakula, makazi, tiba na elimu. Kwa hiyo basi njia sahihi ya kusaidia kupunguza na pengine kuondoa ongezeko la makosa ya jinai ni kwa dola kutimiza wajibu wake kwa raia.

Misimamo ya pande zinazohusika na shauri

Tafauti moja kubwa katika uendeshaji mashauri ya jinai na yale ya madai ni kwamba aghalabu serikali huendesha mashauri ya jinai. Hufanya hivyo kwa kutumia ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (F.90, Kanuni ya mwenendo wa jinai, Sheria Na. 9, 1985). Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai anasaidiwa na Mawakili wa serikali pamoja na waendesha mashitaka wengine kutoka idara mbalimbali kama vile polisi na uhamiaji. Lakini mashauri mengi katika mahakama ya wilaya huendeshwa na polisi.

Serikali huweza kuamua kumshitaki mtu kutokana na malalamiko kutoka kwa anayehusika au inaweza kufanya hivyo inapoamini kosa la jinai limetendeka hata kama hakuna malalamiko rasmi yaliyopelekwa mbele yake.

Misimamo ya pande zinazoanzisha mashitaka ni muhimu kueleweka katika utatuzi wa mashauri ya jinai nje ya mahakama. Maana yake ni kuwa kwa kiasi gani mlalamikaji au serikali watakuwa tayari kutompeleka mahakakamani mkosaji wa jinai? Hakika hakuna utafiti uliofanywa hapa nchini kujibu swali hili kwa usahihi. Isipokuwa ni dhahiri uamuzi huo utategemea masuala gani kama vile wepesi wa kosa linalohusika, athari iliyopatikana na iwapo mkosaji yuko tayari kufidia athari aliyoipata mlalamikaji.

Mbinu za utatuzi

Kama ilivyogusiwa kabla, kuna namna nyingi za kutatua migogoro ambazo zinaweza kutumika katika utatuzi wa mashauri ya jinai. Baadhi ni usuluhishi, upatanishi na majadiliano. La muhimu ni kutumia mbinu ambayo itasaidia kutatua shauri linalohusika kwa wepesi.

Azma yetu sio kuzama katika mbinu hizo bali kuonesha kwamba pande zinazohusika na shauri zielezwe na kuelewa faida za kutatua shauri lao nje ya mahakama. Ili kuelewa hivyo itafaa kuangalia masuala muhimu kama vile dhamana, ucheleweshaji wa kesi, madhila ya kifungo, fidia na uhusiano wa pande zinazohusika.

Dhamana

Tatizo ambalo linaleta mateso makubwa kwa washitakiwa wengi ni kukosa dhamana (Dk. Abdallah J. Saffari, Human Right in the Criminal Process with Reference to Tanzania Mainland, i.k). Lakini suala la dhamana ni lazima litazuka mtu anaposhitakiwa. Nia yake ni kuhakikisha mahakama yanamwachia mshitakiwa ambaye atarejea kuendelea na shauri lake siku iliyopangwa. Ina maana suala la dhamana haliwezi kuepukwa na mshitakiwa. Njia ya kuliepa ni kutopelekwa mahakamani.

Ucheleweshaji wa mashauri

Kwa miaka mingi kumekuwepo na malalamiko ya ucheleweshaji mashauri ya jinai katika ngazi mbalimbali za mahakama Tanzania (K.h.j). Tatizo hili lipo na mapendekezo kadha wa kadha yametolewa ili kulitatua. Lakini mapendekezo na vitendo ni masuala tafauti kabisa. Hivyo hadi sasa tatizo hili bado lipo (K.h.j).

Athari za ucheleweshaji wa mashauri ni pamoja na kuziweka pande zinazohusika katika wasiwasi; na kuziondolea uhuru wa kusafiri na kufanya kazi ili kusubiri kwenda mahakamani. Namna bora ya kuepuka tatizo hili ni kutohusika na taratibu za mahakama katika jinai.

Madhila ya kifungo

Kuna nadharia nyingi kuhusu adhabu au athari zake. La muhimu hapa ni kuelewa kwamba kifungo, kirefu au kifupi (pamoja na kuwekwa mahabusu) (Nipashe, Dar es Salaam, Februari 10, 1996, uk. 1) kuna athari kubwa kwa mhusika. Watoto wameathirika mno kutokana na jambo hili. Na wakubwa nao wameathirika kwa namna tofauti (Nipashe, Dar es Salaam, Februari 23, 1996 uk. 4).

Tatizo hili linaongeza kwa kutokuwepo na uwiano wa adhabu miongoni mwa maofisa wa mahakama. Isitoshe, serikali haitoi fidia kwa mtu ambaye amefungwa kwa makosa ya mahakama. Hivyo bora kuepuka taratibu za mahakama.

Fidia

Kwa kawaida fidia husikika zaidi katika mashauri ya madai. Lakini suala hili pia liko katika mashauri ya jinai ingawa labda halizungumzwi sana au kupewa kipaumbele (Kanuni ya Mwenendo wa Jinai i.k).

Fidia huweza kuwa ya fedha, mali au hata kuomba radhi au msamaha kwa upande wa mkosaji. Namna ya fidia itategemea aina ya kosa na uzito wake. Mathalan mwizi wa nguo anaweza kutakiwa kuzirejesha au kulipa gharama ya kununua mpya. Na hivyo hivyo kwa mwizi wa aina nyingine ya mali. Pia anaweza kutakiwa kufidia hasara iliyopatikana kutokana na tendo hilo la wizi.

Kwa upande mwingine katika kutafuta suluhu mtu aliyemuumiza mlalamikaji au kumtukana anaweza kutakiwa kugharamia matibabu kisha kulipa fidia ya uchungu na maumivu yaliyotokana na kosa hilo. Na anaweza kutakiwa kuomba radhi.

Yumkini suala la fidia ni muhimu mno kuangaliwa kwa kina katika utafutaji suluhu wa mashauri ya jinai nje ya mahakama.

Watendaji

Kwa mujibu wa makala haya dhahiri watendaji wakuu katika utatuzi wa mashauri ya jinai ni wasimamizi wa utatuzi yaani watatuzi kwa upande mmoja, na pande zinazohusika na mashauri yenyewe, kwa upande mwingine (yaani walalamikaji na watuhumiwa).

Watatuzi

Watatuzi ni watu wenye ujuzi, nia na uwezo wa kutatua mashauri ya aina hii. Watu hawa watapanga mikakati ya kuwasiliana na walalamikaji na watuhumiwa.

Walalamikaji

Kuna aina mbili kubwa za walalamikaji yaani watu binafsi kwa upande mmoja na serikali kwa upande mwingine.

Watu binafsi

Watu binafsi ni wale ambao wameathirika moja kwa moja na tendo la jinai. Kwa kawaida watu hawa huenda kutoa taarifa ya tukio hilo kituo cha polisi ambao hulifuatilia shauri hilo na kuchukua hatua zinazostahili.

Watatuzi wanaweza kuwasiliana na walalamikaji kabla ya kutoa taarifa polisi au mara baada ya kufanya hivyo ili kutafuta suluhu kati yao na watuhumiwa. Katika kufanya hivyo faida na athari za kutatua shauri hilo nje ya mahakama vielezwe vizuri kwa pande zote zinazohusika.

Serikali

Mara nyingi serikali husimamia upelelezi wa makosa ya jinai na kuendesha mashauri hayo mahakamani. Serikali hutumia polisi kufanya upelelezi na waendesha mashitaka kusimamia kesi hizo mahakamani. Watendaji wakuu hapa ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai. Wa kwanza anao wasaidizi wake kama vile Wakuu wa Upelelezi wa mikoa, wilaya na vituo. Na wa pili, yaani Mkurugenzi wa Mashitaka anao wasaidizi wake kama vile mawakili wa serikali na waendesha mashitaka kutoka idara mbalimbali za serikali.

Kuna uhusiano mkubwa baina ya watendaji hao wakuu katika uamuzi wa kufungua au kutofungua mashitaka. Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai anayo kauli ya mwisho katika suala hili. Lakini ni kweli kabisa kuwa uamuzi wa kuendesha mashauri mengi ya jinai (isipokuwa yale mazito kama vile uhaini na mauaji) hufanywa kuwashtaki watuhumiwa bila ya kuwa na ushahidi wa kutosha kufanya hivyo. Jambo hili husababisha mahakama au Mkurugenzi wa Mashitaka kuyatupilia mbali au kuyafuta mashitaka katika hatua za awali au mwisho wa shauri. Tatizo ni kwamba vyovyote vile iwavyo athari kubwa tayari huwa imeshatokea kwa mshitakiwa.

Nyakati nyingine mashitaka hufunguliwa kwa makosa makubwa zaidi kinyume na ushahidi uliopo. Kutokana na hali hii aghalabu mahakama hukataa kutoa dhamana au hufanya hivyo kwa masharti magumu mno kutimizwa. Aidha mara nyingine makosa ya jinai yangeweza kuendeshwa kama ya madai.

Kwa hali hii ni wajibu wa watatuzi kukutana na watendaji hawa wakuu au wasaidizi wao kabla au mara tu watuhumiwa wanapopelekwa mahakamani kutafuta namna ya kutatua shauri linalohusika. Katika kufanya hivyo itakuwa muhimu kuzingatia faida na athari za kufungua mashitaka. Pia ni muhimu kuwahusisha wahusika wakuu katika jinai yaani mtu au watu ambao wameathirika na kosa linalodaiwa kwa upande mmoja, na watuhumiwa kwa upande mwingine. Maana pande hizi mbili ndizo zitakazoweka masharti ya makubaliano ya kutoenda mahakamani. Na serikali itapata wasaa kuona iwapo masharti hayo hayataathiri maslahi yake na raia wote kwa jumla.

Wakati muafaka

Ni vizuri watatuzi kukutana na pande zinazohusika mara baada ya tukio la jinai kama vile wizi mdogo, kuharibu mali kwa makusudi yanaweza kutatuliwa kabla ya kukimbilia vituo vya polisi. Mali iliyoibwa au kuharibiwa inaweza kurejeshwa au kufidiwa pamoja na usumbufu uliotokea. Na mtuhumiwa anaweza pia akamuomba radhi mlalamikaji.

Kama haiwezekani kutatua shauri la jinai katika hatua hiyo ya awali basi watatuzi wakutane na pande zote wakati shauri limefikishwa polisi lakini bado kupelekwa mahakamani. Na hapa napo watatuzi watatumia mbinu kama pale awali.

Na iwapo shauri litakuwa limefikishwa mahakamani bado watatuzi wa pande zinazohusika wanaweza kutumia mbinu zile zile kuliondoa shauri hilo mahakamani. Njia mojawapo ya awali kabisa ni kukubaliana shauri hilo liendeshwe kama shitaka la madai. Jambo hili litaziwezesha pande zinazohusika kukwepa madhara yatokanayo na mashauri ya jinai ili kutafuta muafaka wa kumaliza shauri hilo kama vile la madai.

Hitimisho

Mashauri ya jinai yanayopelelekwa mahakamani ni mengi kuliko mashauri ya madai. Na madhila yatokanayo na mashauri ya jinai pia ni makubwa zaidi kwa pande zote zinazohusika. Hivyo wakati umefika kujaribu kutatua mashauri ya jinai nje ya mahakama kwa njia nyngine kama vile majadiliano na usuluhishi. Jambo hili linaweza kufanyika hasa kwa kuanzia na yale mashauri yanayohusu makosa mepesi ambapo fidia pamoja na kuombana radhi huweza kutumika kuepuka mwenendo wa jinai mahakamani.

Uwezekano wa kutatua makosa makubwa pia upo kutegemea aina ya makosa yenyewe, uzito wake na athari iliyopatikana.

Kwa jumla ufanisi katika utatuzi wa mashauri ya jinai utaondoa madhila ya kifungo na upotezaji muda mahakamani, kudumisha maelewano na pia kupunguza kasma ya serikali katika kuwakimu mahabusu na wafungwa. Kasma hiyo ni ziada inaweza kutumika kwa maendeleo ya jamii. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook