TAHARIRI
 
Waislamu waangamizwa Chechnya tuwasaidiaje
 

WAISLAMU kwa maelfu wameuliwa Chechnya. Nyumba zao, miji yao, viwanda vyao na mashamba yao, yanaangamizwa kwa mabomu na mizinga ya Warusi.

Wengi wamekimbilia misituni na milimani na vitoto vyao vichanga, huku wakikabiliwa na baridi kali iliyoandamana na theluji. Chakula hakuna na majeruhi hawana dawa.

Urusi inatenda yote haya kwa kisingizio kwamba inapambana na magaidi. Lakini haya hayakuanzia kwa Warusi.

Clinton, aliipiga Afghanstan na Sudan, akidai ni magaidi.

Iraq inapigwa kila leo kwa kisingizio cha kuwalinda Wakurdi.

Waislamu walipouliwa Mwembechai, ilidaiwa ni kupambana na wanaovuruga amani ya nchi.

Waislamu wa Chechnya wanaodai haki yao ya kujitawala wamefanywa magaidi na hivyo kuwa uwanja wa kujaribia silaha za maangamizi za Kremlin..

Kinyume kabisa na kanuni zote za kimataifa raia wanauliwa, na mashirika ya misaada yanazuiliwa kuwahudumia waathirika.

Baada ya majumba kubomolewa, ndugu zetu, kaka zetu na dada zetu, wameachwa bila makazi, chakula, nguo na madawa. Aidha, hawana pakwenda mbele wala nyuma.

Taarifa za hivi karibuni za shirika la kimataifa la wakimbizi (UNHCR) zimeeleza kuwa wapo wakimbizi wapatao 217,000 katika Ingushetia, Ossetia, Dagestan na Stavropol. Maelfu wengine hawajulikani walikokimbilia baada ya makazi yao kuangamizwa.

Taarifa hiyo imezidi kueleza kuwa Wachechnya wapatao 200,000 wamekwama mipakani wasijue pa kwenda.

Hayapo maneno ya kutosheleza, kuelezea ukatili na unyama wanaofanyiwa Waislamu wa Chechnya.

Ikutoshe peke yako kutafakari, ikoje hali kwa wanawake na watoto wanaotolewa katika makazi yao kwa mashambulizi ya mabomu, mizinga na maroketi!

Ikoje hali ya watoto hao Waislamu, wanaolazimishwa kuishi milimani kwenye baridi kali ambapo hata majani hayaoti.

Ulimwengu leo unashuhudia umwagaji wa damu na ukatili uliopea kama ule uliofanywa wakati wa Czarist, Bolshevic na zama za Stalin.

Takriban Waislamu wa Chechnya wapatao 4000 washauliwa na Warusi.

Kwa muda mrefu sasa Waislamu wa Chechnya wamekuwa wakifanya juhudi ya kujinasua kutoka ukoloni wa kikomunisti wa Urusi.

Ni jambo la kusikitisha kuwa kilio cha Waislamu wa Chechnya, kimekuwa kikiangukia sikio la uziwi la walimwengu.

Tulishuhudia huko Timor ya Mashariki ulimwengu mzima ukija juu kuwahami Wakatoliki wapewe haki yao ya kujitawala. Lakini Chechnya imekuwa Mwembechai. Maadhali wanaouliwa ni Waislamu sheria, mikataba na kanuni zote za kimataifa haziangaliwi.

Tutakuwa tumefanya kosa kubwa iwapo hatutaguswa na unyama huu wanaofanyiwa Waislamu wenzetu.

Tumkabili Mola wetu kwa dua. Tuielewe vyema hali ya udhalimu, uadui na ukandamizaji, unaowakabili Waislamu duniani.

Lakini muhimu zaidi, uovu huu uzungumzwe wazi wazi Misikitini, mitaani na popote walipo Waislamu.

Khotuba za Ijumaa zisikose kuelezea hali ya Waislamu huko Chechnya, Nigeria, Kossovo, Bosnia, Mwembechai na kwingineko.

Pamoja na hayo, tuandike barua kwa balozi na taasisi mbalimbali za kimataifa kusajili hisia zetu juu ya udhalimu wanaofanyiwa Waislamu.

Kumbuka, jana Mwembechai, leo Chechnya, kesho yaweza kuwa zamu yako.

Mtume (s.a.w.) amesema Waislamu katika kupendana na kuhurumiana kwao ni kama mwili mmoja. Sehemu moja ikiathirika mwili wote hushtadi kwa homa na maumivu.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook