Ndugu Waislamu,
MWENYEZI Mungu (s.w.) baada ya kuumba ulimwengu na vilivyomo akamteua mwanaadamu kuwa khalifa na mtawala katika ardhi (dunia). Pia akamtayarishia mwongozo wa namna ya kuitawala dunia hii ipatikane amani, baraka na mafanikio leo na kesho akhera. Bahati mbaya wanaadamu tumepuuza mwongozo huo na kufuata utashi wa matamanio ya nafsi zetu.
VIONGOZI wa jamii ulimwenguni wapo tayari kushika mikononi mwao vitabu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu, vyenye miongozo sahihi wa maisha, kuvishika kwa ajili ya viapo tu wakati kushika nyadhifa zao za utawala na ukubwa, lakini kamwe hawako tayari kusimamia utekelezaji wa maagizo yaliyomo ndani ya maandiko ya vitabu hivyo.
Kiburi kilioje cha viongozi hao kumpuuza Mwenyezi Mungu na sisi raia tulio wafuasi wa viongozi hao tuko radhi, hatuhoji wala kukemea hilo. Matokeo yake ni hasira za Mwenyezi Mungu kutuelekea, baraka na rehema kutoweka na badili yake kushamiri dhulma, uhasama, kuhusudiana, kuuana, kunyanyasana, kukashifiana, kutukanana na maovu mengineyo.
Viongozi wengi wa jamii, hawataki kabisa dini ihusishwe katika uongozi wa jamii. Kauli za usichanganye dini na siasa ni ushahidi wa hilo. Ikiwa wote tunaamini kwamba ulimwengu ni wa Mwenyezi Mungu na muongozo wa Mwenyezi Mungu juu ya kuendesha ulimwengu wake umo katika vitabu vya dini, sijui tunapopinga dini isiwemo katika uongozi wa jamii kama tunaitakia mema jamii.
Viongozi wa jamii hawako tayari kusimamia sera za uhakika za Muumba wa ulimwengu kama zilivyo katika vitabu vya dini, badala yake wanasimamia sera za dhana na fikra potofu. Mwenyezi Mungu anaagiza ulevi una madhara, upigwe marufuku katika jamii, viongozi wanasema kinyume kwamba ulevi ni uchumi na burudani. Mpaka ulevi ni urithi wa taifa.
Mwenyezi Mungu anaagiza watu wajiheshimu kwa kuvaa mavazi ya stara, viongozi wanapinga kwamba kuvaa ni hiari ya mtu atavaa apendavyo na pale apendapo. Mwenyezi Mungu anaagiza uzinifu ni uchafu na hatari, usiwepo katika jamii, wanasiasa wanaona uzinifu sio tatizo mradi mtu hapati ukimwi au mimba. Yapo mengi ambayo ni maagizo ya Muumba kwa ushahidi wa maandiko matakatifu, lakini yanapuuzwa na viongozi wa jamii na hawataki kusimamia utekezaji wake.
Wakati umewadia wa kuwahimiza na kuwashawishi viongozi katika jamii zetu, wairuhusu dini katika uongozi wa jamii na wasimamie utekezaji wa sera za Mwenyezi Mungu za kuamrisha mema na kukataza maovu kwa mujibu wa maandiko ili upatikane uwiano wa kiroho na kimwili. Wakianza wao na sisi tutafuatia bila woga kwani watu huwaiga viongozi wao. Mungu atuwezeshe Insha-Allah.
Enyi waja wa Mwenyezi Mungu imepofuka mioyo yenu kwa mghafala wa kumsahau Mwenyezi Mungu wetu. Mmebadilisha mema kwa maovu, mmekuwa wavivu kufuata twaa ya Mwenyezi Mungu. Mmeisahau siku ya kiyama na mazito ya siku hiyo ya hisabau na adhabu. Mmeamua kumtii na kumfuata Shaitaan na matamanio maovu ya nafsi badala ya Mwenyezi Mungu kuyaparamia maasi na kuacha twaa ya Mwenyezi Mungu.
Mmepuuza na kujiweka mbali na mafunzo ya dini yenu na kuzitupa adabu na sheria, nidhamu na murua wa Kiislamu nyuma ya migongo yenu. Mkaupendelea ulimwengu huu wa kupita kuliko akhera ya kudumu. Mkajishughulisha sana na dunia na mapambo yake mkaacha kujifunza dini yenu na kuifuata. Mkaacha utamaduni na mwenendo mzuri wa Kiislamu, mkashabikia tamaduni na mienendo mibaya ya kimagharibi inayozivuruga jamii zetu kwa mmomonyoko wa maadili.
Ndugu zangu Waislamu tunatakiwa tuzindukane na usingizi huu mzito na mghafala mkubwa wa kufuata na kutii dhana potofu, tukaziacha sera za uhakika za Mwenyezi Mungu za kuiongoza jamii. Wapotofu kwa kutumia dhana ya fikra zao zisizo sahihi wametuonesha maadui bandia tukashughulika nao kwa muda mrefu na gharama kubwa tukimcha adui halisi akiiharibu na kuivuruga jamii bila upinzani kama hatupo na mara nyingi tukimsaidia adui huyo kutuvuruga tukidhani kwamba yeye siye adui.
Dhana tuliyoilea muda mrefu ya kwamba maadui wetu ni watatu: Ujinga, Umaskini na maradhi ni dhana potofu iliyotuzuia kumtambua na kumshughulikia adui wa kweli ambaye ni sheitaan (twaghuut) kama tunavyoambiwa na Mwenyezi Mungu (s.w.) Muumba wa vyote na Muumba wa vyote.
Ndugu Waislamu adui tunaetahadharishwa naye na Muumba wetu ni sheitaani wala sio ujinga, maradhi na umaskini, kwa sababu huo ujinga maradhi na umaskini ni matokeo tu ya kumtii sheitaani. Kwa fikra sahihi za mzamo-ujinga sio kutokujua kusoma na kuandika tu kwa sababu wapo wengi ambao wanajua kusoma na kuandika na wengine wana shahada za juu lakini bado ni wajinga. Ujinga ni mtu kutojua asili yake, chanzo chake na vile alivyopatikana.
Ukweli huu haupatikani mahali pengine zaida ya kutoka kwa yule mtengenezaji (manufaturer) wa ulimwengu na vyote vilivyomo katika huo ulimwengu.
Kuna wengi wa hao wanaojua kusoma na kuandika na wenye shahada ambao wamejingikiwa na ukweli huu, wakafikia hata kumkataa Muumba na kwamba ulimwengu haukuumbwa umejitokeza tu wenyewe. Huu ni ujinga usio na mfano na tukimfuata mtu wa aina hii ndipo tunapojiingiza katika matatizo na majanga makubwa ya kijamii.
Maradhi nayo ni matokeo ya kumfuata huyu adui wetu mkubwa sheitaan tuliyetahadharishwa naye. Leo kuna gonjwa lisilo na tiba "UKIMWI" ambalo chanzo chake ni kwenda kinyume na amri ya Muumba ya kuacha uzinifu, tukatii vishawishi vya kitwaghuti, tukafanya uzinifu ni burudani. Watoto wa mitaani, watoto wanatupwa vyooni, kuvunjika kwa ndoa na kukosekana ustawi wa jamii, ni sababu ya kumtii sheitani adui mkubwa badala ya kumpiga vita.
Umasikini nalo pia ni tatizo linalojitokeza baada ya kumuasi Muumba na kumtii sheitani. The world economic order and the distribution of wealth (uchumi wa dunia na mgawanyo wa mali) umo katika sera na mikono ya matwaghuti - uchumi wa riba wenye uwezo limbikiza bila kujali wanyonge, wakati hao wanyonge ndio sababu ya kuneemeka hao wenye uwezo kwa dhulma zao.
Nchi za ulimwengu wa tatu leo zina madeni yasiyolipika, kwa sababu ya uchumi wa riba. Zikikopa zinatakiwa zirudishe mikopo na ziada ya riba. Kwa unyonge wa vinchi hivyo vinashindwa kurudisha mikopo hiyo kwa wakati, riba inajilimbikiza na kukua deni lisilolipika kuzifanya nchi hizi siku zote ni maskini zenye uchumi tegemezi. Mwenyezi Mungu katika kujua ubaya wa riba kwa jamii ameikataza isitendeke.
Kwa ushahidi huu adui yetu kwa yakini sio ujinga wa kutojua kusoma na kuandika wala maradhi wala umaskini. Adui yetu ni twaghuut shetani anayetuhadaa tusimjue, kumkubali na kumtii Mwenyezi Mungu ambapo matokeo yake ni matatizo mengi tu ya kijamii. Hivyo kama viongozi wa jamii wangekuwa wanazifahamu sera za Muumba wa jamii, wakazikubali na kuzifanyia kazi katika utekelezaji badala ya kupoteza muda na gharama katika sera za dhana na fikra potofu, wangeweza kuinusuru jamii yetu na matatizo mengi sana.
Ikiwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo bila shaka yeye ndiye mjuzi zaidi na namna ya kuendesha ulimwengu wake.
Ndugu zanguni kuna haja kubwa ya kubadili
mwelekeo wa jamii kufuata fikra na dhana fikra na dhana zisizokuwa sahihi
za wanadamu wenzetu na kuacha fikra za Allah (s.w.) Muumba wa jamii. Sisi
ni viumbe wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.
--
|
|