Mke wa Spika wa Bunge la Sudan asema nguvu ya Waislamu ni umoja
 

MKE wa Spika wa Bunge la Sudan, Bi Rahmani Mahdi amewahimiza Waislamu ulimwenguni kote kuuungana ili kuweza kukabiliana na nguvu mpya ya mataifa makubwa. Amesema kuwa hivi sasa Ulaya imeungana na halikadhalika Madola ya Amerika. Nasi Waislamu hatuna budi kutambua kuwa nguvu yetu ipo katika umoja.

MWANAMAMA huyo alitamka maneno hayo wakati akihojiwa na jarida la Mahjubah la Iran wakati alipokuwa ziarani nchini humo.

Mwishoni mwa mahojiano hayo, Bi Rahmani aliutanabaisha ulimwengu wa Waislamu kuwa, vita kusini mwa Sudan, vinachochewa na Marekani, Israel na Vatican kwa lengo la kudhoofisha nguvu za Uislamu nchini humo.

Yafuatayo ni mahojiano hayo:

Mahjubah: Tafadhali jitambulishe kwa wasomaji wetu.

Bi Rahmani: Kwanza kabisa nalishukuru jarida lenu kwa kufanya nami mahojiano haya. Mimi natokea Sudan na jina langu ni Rahmani Mahdi. Mimi ni msomi wa sheria niliyehitimu katika Chuo Kikuu cha Khartoum (Sudan). Mume wangu ni Dk. Hassan Al- Turabi, Spika wa Bunge la Sudan. Babu yangu mkubwa alikuwa kiongozi wa mapinduzi ya Waislamu dhidi ya serikali ya kikoloni ya Uingereza nchini Sudan mwaka 1885.

Nina familia ya watoto sita, wanaume na wanawake. Umri wangu ni miaka 57, na ninafanya kazi katika shirika la kimataifa la wanawake nchini Sudan. Pia ninatumikia jeshi la ulinzi la umma. Sisi huwa tunaandaa chakula kwa ajili ya askari wa jeshi hilo.

Vile vile, ninafanyakazi katika kitengo cha uandishi wa vitabu kuhusu wanawake nchini Sudan. Tumebobea katika uandishi wa vitabu juu ya nafasi ya wanawake katika Uislamu. Tunawahamasisha wanawake wawe waandishi kwa sababu tunawataka watopee katika taaluma ya sheria za Kiislamu ili akina mama wazijue nafasi zao ndani ya Uislamu.

Mahjubah: Hivi, hii ni ziara yako ya kwanza hapa Iran?

Bi Rahmani: Hapana, hii ni ziara yangu ya tatu. Awali nilikuja hapa kwa mwaliko wa mke wa Rafsanjani. Alinialika mimi pamoja na mke wa Rais wa Sudan. Tukakaa hapa takriban siku sita. Baadaye, nilialikwa tena na Fatma Rafsanjani kuja kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa wanawake wa Kiislamu kabla ya mkutano wa OIC uliofanyika mjini Tehran, mwezi Desemba 1997. Tulikaa hapa kwa kipindi cha juma moja.

Kwa hiyo basi, hii ni ziara yangu ya tatu. Nimekuja hapa na mume wangu kuhudhuria mkutano wa Bunge la Muungano la nchi za Kiislamu (IPU) ambalo, nahisi, hivi sasa linaanza kufanana na kijiji kidogo kutokana na usafiri, mawasiliano na mikutano. Na kama watu wasemavyo kwa Kiingereza, "Birds of the same feather flock together" yaani "Ndege wanaofanana manyoya huruka pamoja".

Hivyo, na sisi Waislamu hatunabudi kuungana ili kuweza kukabiliana na nguvu mpya ya mataifa makubwa. Ulaya imeungana na halikadhalika madola ya Amerika. Waislamu lazima tutambue kwamba nguvu yetu ipo katika umoja wetu.

Tuungane katika kila kipengele cha maisha - kisiasa, kijamii na kiuchumi na mabunge yetu yafungamane, ni umoja huu utakaoleta mashikamano katika ulimwengu wa Waislamu.

Mahjubah: Umezungumzia umoja katika wakati ambao wanawake wa Kiislamu wapo katika hali ngumu ya kukandamizwa hasa hasa wale wa Kossovo, Bosnia na Palestina. Sasa, sisi wanawake wa Kiislamu tufanye nini kuwasaidia wenzetu hao.

Bi Rahmani: Twaweza kufanya mambo mengi tu kuwasaidia wenzetu. Kwa kweli tunasikia vilio, tunawaona katika runinga (televisheni) na tunapata habari zao kupitia vyombo vinginevyo vya habari. Tunafahamu kuwa Waislamu wameuliwa katika pande nyingi za dunia, zikiwemo Palestina, Somalia, Kashmir, Bosnia na Kossovo.

Hii ni vita kubwa dhidi ya Waislamu na kwa hakika, anayeathirika zaidi ni mwanamke. Yeye ndiye mzazi wa familia, mlezi wa familia, na katika vita hivi, hupoteza mume, watoto na makazi na mzigo mzito humuelemea yeye, ndio maana sisi kule Sudan tunajitahidi kuwasaidia wanawake.

Akinamama wa Kiislamu wana hali ngumu kule Kossovo kwa sababu ya vita dhidi ya Uislamu na Waislamu. Sisi tunawasaidia kifedha, tunawapelekea chakula, tunawaombea dua nyakati zote na katika kila sala, na kufanya hivi ni muhimu sana - InshaAllah.

Mahjubah: Najua umesomea sheria na hivyo u-mwanasheria, na unazijua haki za watoto na jinsi zinavyopuuzwa duniani. Uislamu umewapa watoto haki kwa maana yake halisi. Je sisi wanawake tufanyeje kuwasaidia watoto kupata haki zao.

Bi Rahmani: Tunaweza kufanya mengi tu. Kwanza kabisa, nadhani, ili kuwapatia watoto haki zao, wanawake wazazi wakae nyumbani kunyonyesha watoto, japo najua kuwa jambo hili linapingana na utaratibu wa sasa wa maisha duniani. Katika pande zote mbili, mashariki na magharibi, ni ada kwa wanawake kutoka majumbani kwenda nje kutafuta pesa.

Sidhani kama utaratibu huu ni mzuri kwa watoto kwa sababu watoto muda wote wanahitaji maziwa ya mama. Maziwa ya kopo si ya asili na hayafai kwa watoto, pia watoto wanahitaji mama wanapoumwa, wanapokuwa na matatizo ya kula, na wanapolowana.

Qur'an imeweka wazi kuwa, lazima tuwape matunzo watoto, tuwape haki ya urithi, tuwape elimu bora na mafunzo (ya maadili) ya Uislamu. Kisha tuendelee kuwaangalia. Tusiwaondoe majumbani mwetu kama wafanyavyo watu wa magharibi.

Huko, mtoto anapofikia umri wa miaka 18, wanasema amekwishakuwa mtu mzima. Wanawahamisha watoto hao wadogo majumbani, wakiwaambia nendeni mkajitegemee. Jambo hili lisifanywe na Waislamu. Sisi tuwajali watoto wetu ili nao watujali uzeeni kwetu, na hivi ndivyo tutakavyoweza kujumuisha familia.

Hivyo, nafikiri nafasi ya mwanamke katika malezi ya watoto ni muhimu sana. Mwanamke asikimbilie kutafuta pesa bali aangalie watoto wake mpaka wakuwe.

Mahjubah: Kwa ajili ya ushirikiano bora wa nchi za Kiislamu, unapendelea nini kingine kifanyike zaidi ya hii mikutano.

Bi Rahmani: Mkutano ni hatua ya kwanza tu. Baada ya mkutano yanakuja maazimio na uandaaji wa sera. Katika uwekaji wa sera, lazima tushirikiane katika masuala ya fedha, masuala ya elimu na tushirikiane rasilimali zetu.

Tusaidiane kifedha, kielimu na hata kwa kuombeana dua. Tunapaswa kufikiriana, kufikiria kila taifa lenye Waislamu hususan wale wanaodhalilishwa na wanaouawa na wanaonyanyaswa kama vile Kossovo, Kashmir, Palestina na Bosnia.

Mahjubah: Ulisema, unaandika vitabu na makala kuhusu wanawake wa Kiislamu. Ni mdahalo gani mnaoweza kuuanzisha ili kuchambua matatizo katika umma wa Kiislamu.

Bi Rahmani: Wanawake wa Kiislamu kwanza kabisa yawapasa wazijue haki zetu katika Uislamu. Haki zetu zote zinapatikana ndani ya Qur'an na katika mafundisho ya Mtume (s.a.w.). Hata hivyo, wanawake wakati mwingine wanaweza kuwa na hiyana dhidi yetu. Ndio sababu tunaandika vitabu, akinamama tuijue nafasi yetu, hili likiwa ni jambo la awali kabisa. Vile vile tuweze kuona umoja wa mataifa unakusudia nini kwetu.

Unajua, umoja wa mataifa unajishirikisha sana katika masuala ya haki za wanawake duniani. Mkutano wa kwanza uliowakutanisha wanawake kule Beijing China, kwa ujumla ulizungumzia haki za wanawake na haki za binadamu katika mataifa mbalimbali.

Umoja huo una azma ya kuingilia kati mambo hayo na kulazimisha mawazo yake juu ya mambo yepi wanawake wafuate na yepi wasifuate. Nionavyo mimi, jambo hili ni la hatari sana kwa sababu watu hawa wana mikataba kama vile nchini Sudan. Wanataka kutumia mkataba ulio kinyume na umbile la mwanamke kwa ajili ya ulimwengu mzima.

Mathalan, wanataka sheria moja ya mirathi, mtoto wa kiume na wa kike wagawane urithi sawa. Sasa hii ni kwenda kinyume na Uislamu ambao huwagawia mali wanawake chini ya kiwango wanachopata kaka zao. Sisi tunafuata sheria za Kiislamu kwa hiyo hatuwezi kusaini mkataba wowote utakaotupeleka kwenye sheria nyingine.

Mimi nafikiri tufanye mdahalo na Wakristo ili kuwafundisha Uislamu na kuwabainishia ukweli kuhusu Uislamu ambao upo kwa ajili ya wanawake na si dhidi yao. Hawa watu wana mawazo potofu kuhusu Uislamu kwamba unawanyima wanawake haki zao.

Kwa upotofu huo, naona tunahitajika kufanya nao mdahalo kuwasaidia kuelewa Uislamu unasemaje kuhusu nafasi ya mwanamke katika vipengele mbalimbali vya maisha.

Mahjubah: Nataka kukuuliza kuhusu hijab (vazi la Kiislamu) una maoni gani juu ya vazi hili. Kwa kuwa umekwishaeleza kuwa watu wasio Waislamu wanamtazamo potofu juu ya wanawake wa Kiislamu na haki zao ndani ya Uislamu, hasa kuhusiana na vazi hilo, una wazo gani kuhusu hili?

Bi Rahmani: Sipaswi kuwa na wazo langu binafsi kwa sababu, nisomapo Qur'an, inaniambia niwe na Hijab na jinsi gani niivae. Na kwa kuwa mimi ni mwanamke wa Kiislamu basi napaswa kufuata kile kinachosemwa na Qur'an. Sihitajiki kuwa na wazo lolote kuhusu hili.

Hijab ni vazi bora kwa mwanamke katika jamii kwa sababu asipokuwa na vazi hili atadhalilika, jambo ambalo yeye mwenyewe hatolipenda. Na naona vazi la stara la Kiislamu ndilo zuri kwa mwanamke yeyote, hata aweje, awe Muislamu au Mkristo.

Kwa kiasi fulani watawa wa Kikristo huvaa vile vile kama tuvaavyo sisi. Wanawake wengine wasijihisi aibu kuvaa Hijab kama sisi. Tulipende vazi hili na tulieneze kwa wanawake wote duniani iwapo wana imani na vazi hili. Mimi binafsi nina imani na vazi hili na nasema napaswa hasa kulivaa.

Najua hawa watu wana mawazo mabovu sana kuhusu vazi hili. Walituchokoza katika mkutano wa Beijing ati walisema, nyie (wanawake wa Kiislamu) hebu oneni haya. Ninyi hamjui sisi tunaufikiria vipi huo uvaaji wenu. Nami nikasema, hata nyinyi hamjui sisi tunawafikirieni vipi kuhusu huo uvaaji wenu. Kwa hiyo sisi vile vile tuna wazo kama hilo mlilonalo nyie, kwa sababu hiyo lazima tuwe na mdahalo kuweka mambo sawa.

Mahjubah: Kwa kumalizia, sijui unataka kutoa ujumbe wowote kwa wasomaji wetu.

Bi Rahmani: Ndio ninao. Nataka kuufahamisha ulimwengu kuhusu vita vinavyoanzishwa dhidi ya Uislamu na Waislamu. Kule Sudan tuna vita kati ya kusini na kaskazini ambavyo sasa inaelekea mashariki ya nchi.

Katika vita hii, waasi wa serikali ya Sudan wanasaidiwa na Marekani, Israel na Vatican ili kuushinda Uislamu nchini Sudan, jambo hili lazima lieleweke vema na ulimwengu wa Waislamu.

Waislamu pande zote za dunia wafahamu kuwa, hawa watu wanapigana vita vya msalaba (Crusade) kusini mwa Sudan, lakini, naamini, sisi ndio tutakaoshinda kwani tunamuamini Allah na tunaamini kuwa ushindi (siku zote) ni wa Mwenyezi Mungu na wale walioamini. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook