KATIKA hali iliyotafsiriwa na wengi kuwa ni chuki za kidini zilizotawala watendaji wa vyombo vya dola, polisi jijini imepiga marufuku kongamano la Waislamu la kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani lililokuwa limepangwa kufanyika katika viwanja vya Jangwani kuanzia Desemba 1 hadi 4, 1999.
Amri hiyo ya polisi ambayo haikuwa ya maandishi ilitolewa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ilala SP G.M Nzowa.
Katika taarifa yake hiyo aliyoitoa mbele ya umati wa waumini wa din ya Kiislamu majira ya saa nane za mchana katika viwanja vya Jangwani, mkuu huyo wa polisi alisema kuwa taratibu zilikuwa zimekiukwa.
Akizitaja taratibu hizo kuwa ni taarifa za kongamano hilo kutiwa saini na Amir wa Shura ya Maimamu Sheikh Juma Mbukuzi badala ya Katibu Mkuu wa Khidmat Dawaat Islamiyat, Shaaban Magezi.
Waumini wa dini ya Kiislamu waliokuwepo katika eneo hilo walichukizwa na hatua hiyo ya polisi ambayo waliita kuwa ni ya kibaguzi na inayodhihirisha chuki ya serikali na vyombo vya dola dhidi ya jamii ya Waislamu hapa nchini.
Akielezea dhulma iliyofanyika Bwana Hassan Jai alisema kuwa barua ya kuomba kutumika kwa viwanja hivyo iliyoandikwa kwa Afisa Utamaduni wa Jiji Kanda ya Ilala inaonesha kuwa Khidmat kwa kushirikiana na Shura ya Maimamu ndizo zilipaswa kwa pamoja kuendesha shughuli hiyo.
Aidha, barua ya Tume ya Jiji yenye kumbukumbu DCC/UTV/V.8/Vol.I/27 iliyoiandikia polisi wilaya ya Ilala inathibitisha kuwa waandaaji wa kongamano hilo ni Khidmat Dawat Islamiyat na Shura ya Maimamu.
Barua iliyoandikwa na Khidmat yenye kumbukumbu KDHIC/P/W/IC/26/99 yenye kuomba kibali cha kongamano hilo ilijibiwa kwa barua yenye kumbukumbu nambari 11/A.24/31/Vol. VII/203 iliyoruhusu kutolewa kwa kibali hicho.
Swali wanalojiuliza Waislamu ni kuwa iweje polisi waende ghafla kutoa amri ya kulipiga marufuku kongamano kwa kisingizio cha barua za mwaliko kusainiwa na Amir wa Shura Sheikh Mbukuzi ilhali kwenye barua waliyoandikiwa na Tume ya Jiji inaonesha kuwa jumuiya hizo mbili kwa pamoja ndizo zinazoandaa na kuendesha kongamano hilo.
Baadhi ya waumini walionyesha masikitiko yao kuona serikali ikiwadhulumu kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa visingizio mbalimbali siku hadi siku.
"Tukitaka kuandamana kwa amani tunajibiwa kuwa taratibu hazikufuatwa, tukitaka kukutana hapa Jangwani hadithi ni hiyo hiyo, sasa ndugu mwandishi sisi tufanye nini? Kwanini tunaonewa katika ardhi yetu wenyewe, tukimbilie wapi?" alilalamika muumini mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Zuberi.
Baadhi ya wananchi waliokuwa wamemzunguka kamanda huyo wa polisi wa wilaya walimweleza kuwa ijapokuwa yeye anatimiza matakwa ya wakubwa zake lakini anatakiwa awe mwangalifu na asichochee chuki miongoni mwa raia.
"Itafikia wakati ndugu kamanda ambapo tutachoka na upuuzi huu mnaotufanyia. Jitahidini kutowajenga wananchi kuamini kuwa wakati wote wao ni raia daraja la tatu katika nchi yao", mmoja wa wananchi hao alimweleza Kamanda huyo wa polisi.
Mpaka mwandishi wetu anaondoka katika viwanja hivyo vya Jangwani, gari la polisi aina ya Land Rover Defender iliyokuwa na askari polisi takriban wanane akiwemo kamanda wa wilaya lilikuwa bado limeegeshwa katika viwanja hivyo.
Katika hotuba yake aliyoitoa Jumamosi ya Desemba 30, 1995 katika hoteli ya White Sands iliyoko nje kidogo ya Jiji, Rais Benjamin Mkapa aliahidi kupiga vita udini katika serikali yake.
Rais Mkapa aliwaambia Watanzania kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 19(1) na (2) ya Katiba ya Tanzania, raia yeyote yuko huru kuabudu na kuwa mfuasi wa dini au dhehebu lolote.
Hata hivyo, Waislamu wamekuwa wakiilalamikia serikali ya awamu ya tatu kuwa imekuwa ikichukua hatua zinazoashiria kuwabagua na kuwakandamiza Waislamu.
Rais Mkapa ambaye ni muumini wa madhehebu ya Kikatoliki alitoa hutuba hiyo kuwashukuru wananchi kufuatia kuchaguliwa kwake kuwa Rais.
Hafla hiyo iliandaliwa na BAKWATA kwa ajili ya kumpongeza na kumuaga Rais mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Katika uchaguzi huo wa mwaka 1995 kura
nyingi za ndiyo kwa Rais Mkapa zilitoka Pwani, Tanga na mikoa ya Kusini
maeneo ambayo wakazi wengi ni Waislamu.
--
|
|