IWAPO nguzo za Zakka ikisimamishwa, matatizo ya jamii kiuchumi yataondoka.
Kusimamisha nguzo hiyo, ni kujenga taasisi na mtandao imara wa ukusanyaji na ugawaji Zakkah kinchi.
Sheikh Suleiman Kilemile ametoa ufafanuzi huo hivi karibuni katika hafla ya ugawaji Zakka.
Hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Starlight iliandaliwa na The Dar es Salaam Yemen Community for Charity and Culture (D.Y.C.C.C.), kitengo cha Zakaat na Sadaqa.
Akielezea falsafa ya Zakaat, Sheikh Kilemile alisema kuwa, Zakaat ni mhimili wa uchumi.
Imekusudiwa kustawisha jamii na kutatua matatizo ya jamii kiuchumi.
Kwa mtazamo huo, amesema Zakat si nguzo ya kutekelezwa mtu mmoja mmoja na bila ya utaratibu.
Katika hafla hiyo ilielezwa kuwa kitengo cha Zakaat cha D.Y.C.C.C., kimekuwa kikiwasaidia wananchi katika elimu, afya na uchumi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Said Abri, ameeleza; wanafunzi watapatao 500 wamepatiwa misaada ya elimu, na 800 wenye matatizo ya afya, walipatiwa misaada ya matibabu.
Aidha, alieleza akina mama kadhaa wameshapatiwa mitaji, ikiwa ni fedha taslimu au vitendea kazi kama majokofu (friza) na vyerehani.
Misaada mingine iliyokwisha kutolewa na D.Y.C.C.C ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa shule na madrasa.
Katika hafla ya Novemba 28, mwaka huu misaada ya thamani ya mamilioni ya fedha ilitolewa kwa wenye shida.
Misaada hiyo ilijumuisha majokofu 15, cherehani 30, baiskeli 20, vifaa vya kuwekea vitu baridi (cooler box) 5 na nguo marobota 10.
Waliohudhuria hafla hiyo walikuwa ni
pamoja na Mwenyekiti wa D.Y.C.C. Sheikh Abdallah Albaity, Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam Yusuf Makamba na mamia ya Waislamu waalikwa.
--
|
|