MFUMO wa demokrasia nchini umeelezwa kuingia mashakani baada ya wafuasi kadhaa wa vyama vya upinzani kutiwa mbaroni kufuatia kuonesha hisia za kutoridhishwa na zoezi zima la uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mapema wiki hii.
Idadi ya waliotiwa mbaroni katika kile kilichodaiwa na vyombo vya dola kuwa ni kudhibiti vurugu hadi sasa imefikia 18 ambapo wawili kati yao walikamatwa katika kituo cha kupigia kura eneo la Mwananyamala.
Wakizungumza na gazeti hili watu mbalimbali walioshiriki uchaguzi huo wameuelezea kutokuwa wa haki na demokrasia.
Walisema dosari zilianza kujitokeza tangu zoezi la uandikishaji ambapo watu wengi walikoseshwa haki hiyo ya kikatiba "kimaarifa".
Uandikishaji wa wapiga kura jijini Dar es Salaam ulikuwa wa "nyumba kwa nyuma" chini ya ofisi ya Tume ya Jiji badala ya vituo maalum kama ilivyozoeleka katika chaguzi nyingi.
Uandikishaji huo umeelezwa kufanyika baadhi ya nyuma na nyakati za mchana ambapo watu wengi wakiwa katika mishughuliko.
" Kama mbinu ya kukwepa wapinzani kwa nini uandikishaji ufanywe kwa maelekezo ya viongozi wa serikali ya CCM na watu
wa kupiga kura wachujwe namna hiyo", mzee Rashid wa Ubungo Darajani amedai.
Aidha, amedai usimamizi wa wapiga kura ulikuwa na dalili za kukipendelea chama tawala.
"Wagombea wa vyama vya upinzani wamezuiwa kusimama katika maeneo mengi kwa sababu zisizo na msingi, hii maana yake nini, ni kuiwezesha CCM ishinde", alisema mgombea wa chama cha CUF Kariakoo Kaskazini Bi Tatu Hamza.
Amelaumu utaratibu mzima wa uchaguzi kwa kusema ulikuwa wa "kihuni" na akaongeza kwamba hapakuwa na sababu ya kufanya uchaguzi kama hapakutakiwa kuwepo upinzani.
"Wangeamua tu na kwa vile serikali ni yao, mitaa yote iongozwe na wanachama wa CCM, Watanzania tungenyamaza tu kuliko kutudanganya kufanya uchaguzi wa namna hii", Bi Tatu alimweleza mwandishi wetu nje ya ukumbi wa Diamond Jubilee juzi.
Akitolea mfano wa uvurugaji wa uchaguzi katika eneo lake, bibi huyo maarufu Kariakoo alisema kura zilizuiliwa kupigwa hadi waliokwenda makanisani waliporejea.
"Upigaji wa kura ulianza saa tano na uliendeshwa masaa mawili tu, mimi nilipofika kituoni milango ya saa saba nikaambiwa uchaguzi umekwisha, lakini cha kustaajabisha wapiga kura walikuwa nje tele wakisubiri", alisema.
Matukio kadhaa ya uvurugaji wa demokrasia yaliripotiwa kutoka vituo mbalimbali vya upigaji wa kura.
Eneo la Tabata vurugu zilizuka baada ya wagombea wa CCM kutangazwa washindi katika hali ya kutatanisha.
Mwananyamala hali ilikuwa mbaya zaidi kufuatia wagombea wa CCM kupata ushindi uliowashangaza wapiga kura wengi.
Imeripotiwa baadhi ya watu waliohoji hali hiyo walikamatwa na kupelekwa vituo vya polisi ambapo baadaye ilitangazwa kuwa walihusika na usababishaji wa vurugu katika vituo vya kura.
Katika maeneo ya Mabibo uchaguzi ulivurugika baada ya wagombea wa CCM "kushindwa vibaya".
Hata hivyo, msimamizi wa kituo kimoja alidai kuwa uchaguzi haukufanyika kufuata kutokubaliana kwa wagombea wa vyama shiriki.
Eneo la Mabibo upinzani mkubwa ulikuwa kati ya CCM na CUF.
Uchaguzi wa uenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wao ulifanyika Jumapili iliyopita sehemu mbalimbali nchini.
Siku moja kabla ya uchaguzi huo Kamanda wa polisi mkoa wa Dar es Salaam Bw. Alfred Gewe alikaririwa na vyombo vya habari akiwaonya waliodaiwa kutaka kuleta fujo katika uchaguzi huo.
Kauli hiyo ya Bwana Gewe ilikuja wakati kukiwa na malalamiko upande wa vyama vya upinzani kuwa kulikuwa na njama za kuwabana wagombea wao.
Wagombea wa CUF na TLP katika moja ya vituo eneo la Ubungo waliwekewa pingamizi mbalimbali hali iliyompa fursa mgombea wa CCM kusimama peke yake.
Hali ilikuwa hiyo hiyo maeneo ya Manzese, Mwembechai, Magomeni, Kigogo na baadhi ya sehemu wilaya ya Ilala na Temeke.
Akiwa kituo cha Sea View eneo la Upanga Mwenyekiti wa CCM Rais Benjamin Mkapa alikuelezea kushindwa kwa wapinzani katika uchaguzi kuwa ni dalili ya kutoeleweka vyema kwa sera zao na kwamba vina kazi kubwa ya kujinadi kwa wananchi.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameielezea kauli hiyo kuwa ni propaganda ya kufunika ukiukaji wa demokrasia unaofanywa na chama tawala.
Wameziomba jumuiya za kimataifa na balozi zilizopo nchini zisaidie kushinikiza kutekelezwa haki hiyo ya kibinadamu hapa nchini.
|
|