Kinga ni 'hapana' si 'salama'
 
Na Hawra Shamte

KATIKA nchi za Kiafrika kusini mwa jangwa la Sahara, takwimu zinaonesha kuwa wanawake huambikizwa zaidi na virusi vya ukimwi kuliko wanaume.

Sababu kubwa inayojitokeza ni maumbile ambayo hurahisisha kupenya kwa virusi.

Sehemu za siri za mwanamke ni laini na zinazotunza majimaji kwa muda mrefu, majimaji ambayo hurahisisha kupenya kwa virusi vya ukimwi katika mishipa ya damu kama mwanamke huyo atakuwa amepata michubuko.

Takwimu zinasema kwamba takriban watu milioni 1.6 nchini Tanzania wanaishi na virusi vya ukimwi ambapo laki tano tayari wanaumwa na ukimwi na zaidi ya watoto laki tatu ni yatima baada ya wazazi wao kufa na ukimwi.

Nini ukimwi?

Ukimwi ni upungufu wa kinga mwilini hali ambayo inasababisha kupungua kwa chembechembe nyeupe za damu ambazo husaidia kinga dhidi ya maradhi mbalimbali.

Mtu anapoambukizwa virusi vya ukimwi, mwili wake huwa hauna nguvu ya kupambana na maradhi na baada ya muda hutokewa na magonjwa mbalimbali ambayo huweza kutibiwa na kurudia tena.

Mwenye virusi vya ukimwi pia huweza kupata magonjwa yatakayomsumbua kwa muda mrefu kama vile homa za muda mrefu, kuharisha kusikokoma, mkanda wa jeshi (upele), majipu, kifua kisichosikia dawa na kadhalika.

Njia kuu za maambukizo

Uasherati, kuwekwa damu (blood transfusion), kuchangia vyombo vya kunyolea, sindano na kukatia, mama mjamzito humwambukiza mwanawe.

Hata hivyo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 80 ya maambukizo ya ukimwi husababishwa na uasherati.

Suluhisho pekee la tatizo hilo ni watu kuheshimu ndoa zao na wale wasiokuwa nazo kujizuia hadi watakapofunga ndoa.

Kama ambavyo watu hujikinga wasiambukizwe malaria kwa kutumia vyandarua, kinga ya kuambikizwa virusi vya ukimwi ni kutofanya zinaa kabisa.

Suala la kubadili tabia ni jambo linalopigiwa kelele kila siku katika vyombo vya habari na takwimu zinaonesha kuwa asilimia 90 ya Watanzania sasa wanafahamu kuhusu ukimwi yaani wanaelewa ukimwi ni nini na unaambukizwa vipi lakini bado haijafahamika ni kwanini hawajakubali kubadilisha tabia zao katika masuala ya jimai.

Kisingizio kinachotolewa kwa watu kufanya vitendo vya uasherati ni hali ngumu ya uchumi.

Mara nyingi mwanamke huwa na mpenzi zaidi mmoja, kwa matarajio kuwa wapenzi hao watamsaidia mahitaji yake ya kiuchumi. Lakini wangapi wanaonufaika kwa kutumia njia hiyo atagundua kuwa ni wachache sana. Katika kila wanawake 100 wanaofanya biashara ya kuuza mwili ni 10 tu wanaonufaika kiuchumi.

Hali hiyo inaonesha kwamba zinaa siyo njia rahisi ya mkato ya kujinufaisha bali ni nja ya maangamizo.

Aidha, kuna mila na desturi ambazo zinatajwa kusababisha ongezeko la maambukizi ya ukimwi.

Mila hizo ni kama ile ya kuwatahiri wanawake ambayo zana ya kutahiria huwa moja kwa mlolongo wa wasichana.

Mila nyingine ni ile ya kurithi wake . Kaka anapofariki ndugu huweza kumrithi mke wa kaka yake na kama kaka alifariki kutokana na ugonjwa wa ukimwi mtandao huwa mkubwa zaidi.

Pia kuna mila ambazo huruhusu watu wa rika moja kuwatembelea wake wa wenzao kila wapendapo kwa sababu ya kuwa wamekwenda jando pamoja hivyo hawana mwiko kwa wake wa hiramu zao.

Kadhalika kuna makabila ambayo si ajabu kwa mume kutembea na shemeji zake wote wa kike na hapo ndipo hutambulika kuwa ameoa.

Mila kama hizo mbali na kumdhalilisha mwanamke pia huchangia kueneza maambukizo ya ukimwi katika jamii pana.

Tahadhari juu ya ugonjwa huo unaoenea kwa kasi nchini ilitolewa hiiv karibuni na Rais Mkapa ambaye alisema kuwa ukimwi ni janga la kitaifa na ongezeko la kasi ya ugonjwa huo linachangiwa na mila na tamaduni za baadhi ya makabila.

Rais alisema wakati umefika kwa Watanzania kuachana na utamaduni na tabia zinazochangia maambukizo ya kasi ya ugonjwa huo na tatizo hilo limo ndani ya uwezo wetu halihitaji wafadhili waje watuambie tubadili tabia.

Bila ya kujali hali ngumu ya kiuchumi inayomkabili mwanamke, anapaswa kujifunza kusema hapana anapokabiliwa na mtu anayemtaka afanye naye uchafu.

Kinga si "mipira" ni kutokukaribia uasherati.

Dawa si "salama" bali kufuata maagizo ya Muumba.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook