"USO umeumbwa na aibu, ni aibu kwangu na ni kinyume cha mila na desturi zetu za Kiafrika kukaa na watoto wangu kuzungumza kuhusu mambo ya zinaa ambayo ndio mzizi mkuu wa ugonjwa wa ukimwi", anasema Mwanamtumu Shaurimoyo mzazi wa watoto watano.
Kosa kubwa linalofanywa wahamasishaji wa kampeni za kujiepusha na ukimwi ni kule kuchukua ukimwi kama tatizo la msingi. Na kujaribu kumjaza mtoto habari za ukimwi.
Suala hapa ni malezi na maadili mema kwa ujumla.
Mtoto alelewe awe na murua mzuri, amjue Muumba wake, ajue lipo anatakiwa afanye na lipi asilikaribie.
Mzazi anayetarajiwa kuwa mwalimu wa mtoto, kuwa kama bubu hasemi lolote kwa mtoto wake, kwa namna hiyo mzazi anachangia kwa kiasi fulani mtoto kupata ugonjwa wa ukimwi.
Mtoto huyo anapokuja kuathirika na ugonjwa wa ukimwi, mzazi ndiye anayekuwa wa kwanza kumlaumu mtoto na kumsema kwa maneno mabaya. Je, angemfundisha na kumpa malezi mema mapema yangetokea hayo?
Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na kitengo cha mradi wa kudhibiti ukimwi cha Umoja wa Mataifa (UNAIDS) zinaonesha kuwa nusu ya watu wote duniani ambao wanaambukizwa virusi vya ukimwi ni vijana na watoto kati ya miaka 14-24 na kila baada ya dakika moja vijana watano wanapata maambukizo.
Watoto na vijana milioni tatu kwa mwaka jana peke yake waliambukizwa ugonjwa wa ukimwi. Vijana wapatao 7,000 wanapata maambukizo ya ugonjwa huo kila siku.
Ni wazi kuwa idadi kubwa ya wanaopata maambukizo ya ugonjwa wa ukimwi ni vijana na watoto ambao wengine hupata kwa bahati mbaya au kwa kujisababishia wenyewe.
Watoto na vijana hao wamekuwa wakipata maambukizo ya ukimwi katika mazingira mbalimbli kama watoto wa mitaani na wale wazazi ambao hawajali malezi ya watoto wao.
Umasikini unaonekana ni sababu nyingine, watoto wasiolelewa huhadaiwa na vitu kama pesa, mavazi, chakula kama vile chipsi na kuku ambavyo kutokana na umaskini wa wazazi wao huwa hawavipati.
Wanaume wenye umri mkubwa wanadhani wasichana wenye umri mdogo ndio wako salama na hawana ugonjwa na bila kujali kwamba kufanya hivyo ndio kuwaambukiza wasichana wadogo ukimwi.
Kuwahamasisha watu "kuelezana wazi wazi bila ya aibu" juu ya kujikinga na ukimwi hakutaleta nafuu yoyote pasi na kuzingatia suala la maadili mema kwa jamii.
Watu wakielimishwa kwanza kuepuka zinaa,
kujikinga na ukimwi kufuate baadaye.
--
|
|