Uyoshua hauna mantiki, Nyerere hafanani na Mussa
 
Na S. Hussein

NI wajibu kuwakemea wale wote wanaofanya stihizai ya kumfananisha Nabii Musa na hayati Julius Kambarage Nyerere. Kiitikadi, utani huo una tafsiri ya kufuru hasa ukizingatia kuwa kuna watu wanaomutakidi visiyo Nyerere. Wengine wamekwisharopoka kuwa alikuwa "nabii". Hata yule aliyempachika Nyerere U-Mussa, hatujui, alisukumwa na hisia gani japo aliegamia kigezo cha kifimbo!

HATA kama wahusika wanafanya hivyo kwa tamathali, bado jambo hilo linabeba maana yenye dhambi nzito kwani kufanya hivyo kunamtweza Nabii wa Mungu.

Achilia mbali Nyerere ambaye haendani hata kidogo na Mussa (a.s.), walipita wacha Mungu wa peo za juu katika dunia hii ambao hawakufananishwa na Mtume yeyote yule. Aidha, walipita wapigania haki wa aina kwa aina lakini nao pia "hawakunasibishwa".

Ukiangalia muktadha wa uongozi wa Mussa, kuanzia mwanzo hadi mwisho wa maisha yake, utagundua hatia kubwa wanayoipata wale wafanyao mzaha kumlinganisha Nabii huyu na mwanasiasa yeyote.

Kwanza, Mussa (a.s.) kama sote tujuavyo, alikuwa Mtume, hadhi ambayo ilikwisha kamilishwa na Muhammad (s.a.w.) karibu karne kumi na nne zilizopita. Hadhi hii binadamu hupewa na Mungu pekee. Kwa maana nyingine, hakuna binadamu mwenye haki ya kumpachika hadhi hii mwanadamu mwenziwe.

Pili, kiimani, Mussa hakuwa Mkristo au Mkatoliki, hakuwa muumini wa utatu bali alikuwa mwanatauhidi na kimsingi, alitumwa na Mungu kufuta itikadi ya kishirikina ya kumchanganya au kumfananisha Mungu na kiumbe chake chochote kile.

Na katika nukta ya kisiasa, misingi ya siasa ya Mussa ni tofauti kabisa na ile ya siasa ya Mwalimu Nyerere. Mwalimu alitawala kwa mawazo ya kibinadamu, Mussa aliongoza kwa sheria za Mungu.

Ndani ya misingi ya siasa ya Nyerere ni muhali kutumbukiza sheria za Mungu, vinginevyo dola inaweza kufanya kile alichotaka kufanya Firauni dhidi ya Mussa na wafuasi wake (rejea tukio la Mwembechai).

Kwa sababu hizo, sio tu Nyerere hafanani na Mussa bali hastahili kupewa sifa hiyo.. Laiti binadamu hawa wangetokea kuishi wakati mmoja basi kisiasa na kiimani wangelikuwa wapinzani.

Kwa mantiki hiyo, utani wa mwandishi wa makala ya "sitari ya Musaa na Nyerere" ungepaswa kuandaa ulingo wa kupambanisha wasifu wa Mussa na ule wa Nyerere ili changamoto yake itupatie "Yoshua wa kweli".

Angefanya hivyo, utani wake ungekuwa wa kiucha Mungu mithili ya ule wa Nabii Ibrahimu alipoziita "nyota" (jua na nyota) Mungu kwa lengo la kuwatanabahisha washirikina.

Lakini "kumhusisha" Nyerere au "kumnyereresha" Mussa kunatoa mwanya kwa matapeli wa kisiasa kujipa "Uyoshua" isivyo halali jambo ambalo linapotosha historia ya Mussa na kumdhalilisha Nabii huyu.

Hata hivyo, kama ni mimi ningeingia katika mzaha huo, ningechimbua mantiki hii, je, mrithi wa mkombozi huwakomboa watu kutoka wapi? Je, urithi wa Yoshua ulilenga kuwakomboa Wamisri kutoka katika utumwa wa Mussa?

Je, urithi wa Yoshua ulikusudia kuwatoa watu katika misingi ya Taurati? Kama ni hivyo kwanini aitwe mrithi wa Mussa? Na kama ni kinyume chake, basi Yoshua alikuja kuendeleza ya Mussa.

Sasa nauliza, ni ipi nafasi ya huyo "Yoshua wa Nyerere na upi ni wajibu wa mrithi huyo wa "Mussa-Nyerere". Kama ni ukombozi, anawakomboa Watanzania kutoka wapi? Je, ana anawakomboa kutoka katika sera za Nyerere? Au je anataka kuwatoa watu katika misingi ya Nyerere? Kama ni hivyo kwa nini aitwe mrithi wa Nyerere?

Mantiki ya "Uyoshua" ni muhali kupatikana katika mazingira hayo. Inavyoelekea wananchi wanataka marekebisho ya misingi ya Nyerere kupitia katiba na watu wanaohitaji ukombozi wamegawanyika katika mitizamo tofauti ya kisiasa, wapo wanaoitaka CCM na wapo wanaotaka vyama vingine. Ni dhahiri kundi hili la pili lingependa kuona anatokea "Yoshua" wa Nyerere, na akitokea litampinga kwa sababu ataendeleza yale yanayowafanya watafute ukombozi.
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook