BARUA
 
Sasa tuambiwe nchi hii haina dini

Ndugu Mhariri

IMEKUWA ni kawaida ya viongozi wa nchi hii kusimama katika majukwaa ya hafla mbalimbali na kusema "Tanzania hakuna udini".

Kauli hii sasa imekuwa kama wimbo kwa viongozi wetu. Lakini kwa muda mrefu sasa jamii ya Kiislamu hapa nchini imekuwa ikisisitiza kuwa Tanzania kuna udini tena uliojikita kila sekta ya jamii.

Na kila aliyetamka kauli hii aliitwa mchochezi, siasa kali au anataka kuhatarisha amani ya nchi.

Lakini hatimaye ukweli umedhihirika katika tukio hili la kupiga marufuku kongamano la Waislamu lililokuwa lifanyike katika viwanja vya Jangwani. Kongamano hili pamoja na maandalizi mengine lilikua na kibali cha polisi.

Katika hatua za kushangaza polisi walikibatilisha kibali hicho kwa madai ya kuhofu kuvurugika kwa amani! Sababu nyingine waliyoitoa ni kuwa Sheikh Mbukuzi alialika Waislamu wote badala ya taasisi za Kiislamu tu.

Sasa kiini macho kipo hapa, yaani taasisi za Kiislamu tano tu zifanyie mkutano Jangwani? Ni wazi walimuelewa vizuri alipokwenda kuomba kibali cha kufanya kongamano Jangwani alimaanisha ni mkusanyiko wa Waislamu.

Sasa hii ya kusema amewaalika Waislamu wote maana yake nini? Ina maana wapo wanaofaa kuhudhuria na wapo wasiofaa? Wakristo kila kukicha mikutano haiishi pale Jangwani na wanakwenda wote, lakini amani haivunjiki. Ila Waislamu ni hatari watavuruga amani.

Tunashuhudia Wakristo wanapiga kambi pale hata mwezi mzima bila wasiwasi wowote. Lakini siku nne za Waislamu imeonekana hatari na balaa kuwaruhusu!

Sasa tunasubiri kiongozi mwingine aibuke kuwa hakuna upendeleo katika dini, kuna uhuru wa kuabudu na kuitangaza dini!

Maulidi Japhary,
S.L.P. 31999,
Dar es Salaam.



Mchezo wa Tausi una athari mbaya

Ndugu Mhariri

NAPENDA kuelezea mtazamo wangu juu ya mchezo wa kuigiza uitwao TAUSI unaorushwa hewani na kituo cha televisheni cha ITV.

Maoni kwamba, mchezo huo una mafunzo kwa mabinti wa Kiislamu wanaobahatika kuendelea na masomo ya juu, kwa kweli, yana mapungufu.

Katika utafiti nilioufanya mitaani, nimebaini athari mbaya za mchezo huo kwa wasichana hususan wale wa shule za msingi na sekondari.

Badala ya kuiga yale matendo mema katika tamthiliya hiyo, watoto wa kike ambao ndiyo wametokea kuupenda sana mchezo huo wanajifunza na kuyafanyia kazi mambo mabaya yanayodhaniwa kuwa yanayasaidia kuiasa jamii. Na hivyo ndivyo ilivyo nguvu ya shetani.

Kimaumbile, watoto wadogo huwa hawana uwezo wa kiakili wa kupambanua na kuchuja mema na maovu. Wao wanaweza kuiga chochote wakionacho au wakisikiacho, ndio maana kwa utamaduni wetu sisi Waafrika, watu wazima na hupaswa kuwa makini wanapotamka au kutenda jambo la siri au faragha.

Kinyume na utamaduni huo, katika mchezo wa TAUSI kuna mambo nyeti ambayo labda kwa watu wazima yangeweza kuchujwa ingawa hilo linategemea akili ya mtu na mwelekeo wake wa kimaadili.

Mathalan mahusiano na mazungumzo ya kihuni kati ya wanaume na wanawake ambayo yanamfundisha na kumshawishi mtoto kuingia katika ulimwengu wa ngono.

Huwezi kumuadilisha mtoto kwa kumuonesha jinsi mwizi anavyoiba, au jambazi anavyokaba watu na kupora mali zao. Vivyo hivyo huwezi kumfundisha mtoto ubaya wa uasherati kwa kumonesha namna waasherati wanavyoendeana na kusemeshana hata kufikia muafaka.

Utaratibu huo mbaya wa kurekebisha maadili ya jamii twaweza kuulinganisha na mtindo wa baadhi ya majarida kuandika maovu kwa lengo la kuondoa maovu. Matokeo yake yanachangia kwa kiasi kikubwa kuhamasisha watu watende maovu.

Nakataa kabisa kuwa jamii zinaweza kuadilika kwa njia hizo. Nasema hivyo kwa sababu kabla ya televisheni na magazeti ya aina hiyo hali ya jamii yetu kimaadili haikuwa mbaya sana kama ilivyo sasa.

Hata hivyo, hatuwezi kukipongeza wala kukienzi kitendo cha kuzuia televisheni kwani ni teknolojia muhimu katika maisha, bali tunachopiga kelele ni kuoneshwa kwa mambo yaliyo kinyume na maadili yetu.

Kwa kuwa ni vigumu kuwadhibiti watoto kuyaangalia mambo hayo basi ninapendekeza wasanii na wahariri wa vipindi vya tamthiliya wazingatie maadili yetu.

Mama Akili,
S.L.P. 1876,
Morogoro.



E'e Allah wanusuru ndugu zetu

Ndugu Mhariri

NAOMBA nafasi katika gazeti letu ili nitoe machungu yanayotusibu kila Muislamu anayetarajia radhi za Allah (s.w).

Uadui uliopo dhidi ya Uislamu na Waislamu ulimwenguni. Kila mmoja wetu yampasa kuelewa kuwa zipo mbinu mbalimbali zinazotumiwa na maadui kuudhoofisha Uislamu kiimani, kimaadili, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni kwa hali na mali, hata sasa imefikia kuuliwa kwa Muislamu au Waislamu siyo kosa.

Hivi sasa Waislamu wenzetu wa Chechnya wanaangamizwa na Mrusi bila sababu yoyote ile, ila kosa lao kubwa ni kule kuwa Waislamu.

Nchi pamoja na jumuiya za kimataifa zinazotetea haki za binadamu zimenyamaza kimya kuonesha dhahiri hujuma wanazofanyiwa Waislamu Chechnya ni halali.

Waislamu wote duniani ni ndugu moja na linalomfika Muislamu mmoja linatusibu sote bila ya kujali rangi, kabila, nchi, utajiri, umaskini na kadhalika.

Allah (s.w.) anatoa ruhusa kupigana na wale wote wanaotupiga kwa ajili yake (2:190-193), (2:216). Hivyo sisi Waislamu yatupasa tushirikiane na ndugu zetu wa Chechnya kwa mali na nafsi zetu, na kumuomba Allah (s.w.) katika kila swala zetu awanusuru na kuwaangamiza maadui wote wa Waislamu na Uislamu. Na awajaalie Waislamu kuwa na subira, uvumilivu, upendo, mshikamano na ushindi mkubwa.

Abdul-Rawph Bushiri,
Dar es Salaam.



Hongera wapinzani, wananchi tukazane

Ndugu Mhariri

KUPITIA gazeti letu, napenda kuwapa pongezi za dhati wabunge wa upinzani kwa kuonesha muelekeo mwema wa kuwasaidia wananchi.

Uwakilishi wao mzuri unaoongozwa na Mama Fatma akishirikiana na Bwana John Cheyo umetoa changamoto kubwa kwa wapiga kura.

Pamoja na kuwashukuru wenzetu waliotumia vizuri kura zao kwa kuwachagua wabunge hao wa vyama vya upinzani katika majimbo yao, sisi wengine lazima tujute kwa kuwapa kura za bure wabunge wa CCM ambao kwa shinikizo na kwa maslahi ya chama chao wanashindwa kutetea wapiga kura bungeni.

Lakini kujuta kwetu kusiishie moyoni na mdomoni tu bali kuthibitike kwa vitendo katika haguzi za usoni. Tuhakikishe tunatumia kura zetu kuongeza nguvu ya wapinzani bungeni.

Nawaomba viongozi wa upinzani, kwa ushirikiano, wafanye chini juu kupambana hadi kuondosha vikwazo tunavyowekewa na CCM ili tusiweze kutekeleza azma yetu ya kuleta mabadiliko ya kisiasa hapa nchini.

Kwa mfano watu wengi tumesikia tu redioni na kusoma magazetini habari za uchaguzi wa serikali za mitaa. Hatukuwaona hao wanaosemekana kupita majumbani nyakati za kazi kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura.

Wengi tumekuwa watazamaji kwa kutoandikishwa na hivyo kukoseshwa kwa makusudi haki yetu ya kuchagua viongozi tunaowataka.

Naunga mkono kauli ya Mama Fatma Maghimbi kuwa, wananchi tujitoe muhanga kweli kweli tuweze kujikomboa. Tusichoke kwani Waswahili husema aliyechoka kapata na aliyepata kahangaika.

Dotto Shaaban,
S.L.P 30124,
Kibaha,
Pwani.



Waislamu tusikubali kudhulumiwa

Ndugu Mhariri

NAOMBA unipatie nafasi hii katika gazeti lako ili niweze kutoa wito wangu kwa Waislamu wenzangu.

Kwa kweli kitendo cha serikali ya CCM kupitia jeshi la polisi na kamanda wa polisi mkoa kuwazuia waumini wa dini ya Kiislamu kufanya makaribisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kitendo cha ukiukaji wa sheria ya nchi.

Hebu tujiulize sisi Waislamu mbona hawa Wakristo wenzao wanaruhusiwa kufanya mikutano na mahubiri katika hivyo viwanja vya Jangwani tena kwa muda mrefu hata mwezi mmoja na kuendelea na kwa nini sisi Waislamu tunyimwe haki hii.

Hatua hii ya sasa kuzuiliwa kongamano imewadhihirishia wale wote waliokuwa wakipinga madai ya Waislamu kuwa wanadhulumiwa hapa nchini.

Vyombo vya dola vinadiriki kuvunja katiba ya nchi kwa kiwango hiki halafu bado wako viongozi wanaosimama kusema wanaongoza kwa mujibu wa katiba na sheria.

Umefika wakati ndugu Waislamu wa kutanabahi kuwa sisi hatuthaminiki hapa nchini kwa hivyo tutafakari njia gani itakayotusaidia kuondokana na madhila haya.

Viongozi wamepania kuvuruga amani kwa hiyo hatuna budi kushikamana na kusimama imara kutetea dini yetu na Taifa kwa ujumla.

Maududi Mussamry,
S.L.P. 4308,
Dar es Salaam.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook