Iking'oka CCM tutanusurika na njaa
 
Na Mujahid Mwinyimvua

AWALI ya yote napenda kuwakumbusha wasomaji wa makala haya ya chakula na lishe kuwa chanzo kikubwa cha matatizo yanayomkabili mwanadamu leo (kama vile njaa na vita) duniani ni uongozi mbaya. Yaani sera mbaya za siasa na roho mbaya waliyonayo viongozi wa nchi mbalimbali duniani.

Kwa mtazamo wa watu wa dini, chanzo cha matatizo hayo ni mwanadamu kuacha kuongoza maisha yake (siasa, uchumi, jamii na kadhalika) kwa kufuata mwongozo kutoka kwa Muumba wake.

Nakumbuka siku moja Amir wa Shura ya Maimamu mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Juma Mbukuzi alisema kuwa, viongozi wa kijamii (wanasiasa) kila wanapoingia madarakani wanaapa kwa kutumia misahafu (Qur'an, Biblia, na kadhalika) lakini hawako tayari kufuata yale yaliyomo katika vitabu hivyo.

Matokeo yake ni zinaa inaonekana ndiyo maendeleo, kinga ya ukimwi ni kondomu, konyagi halali lakini gongo haramu, mtu kwenda uchi kwa vile tu anamwiga mzungu hakuna taabu.

Vile vile, nakumbuka siku hiyo Sheikh Mbukuzi alikuwa akihimiza waumini kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji, kwa kuwaambia "wanaosema tusichanganye dini na siasa hawajuwi maana ya dini wala siasa, Msikitini hakuna dini, dini iko mtaani ambako watu wanadhulumiana, watu hawalali kwa kelele za walevi walioko katika baa na 'grosaries'.

Kwa hiyo, lazima viongozi wa dini tuingie katika jamii (siyo tu kuishia Misikitini) ili kuwaokoa wananchi.

Tukizingatia haya yote, tuna kila sababu ya kukubali (vinginevyo tutakuwa mataahira) kuwa wananchi wa Tanzania hawataweza kuwa na chakula na lishe bora kama hakutakuwa na siasa (sera) safi na uongozi bora.

Wananchi wajue kwamba umaskini wao unaofikia kilele cha kuwaua baadhi yao kwa njaa, chanzo chake siyo "kapenda Mungu" bali ni sera mbovu na uongozi mbaya wa nchi.

Kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) (na wazee wake wa TANU na ASP) kipo madarakani kwa zaidi ya miaka 38, umri wa mtu kuwa na mjukuu, tuna kila sababu na ushahidi wa kisayansi kuamini kuwa CCM (na serikali yake) iking'oka madarakani kidemokrasia, walalahoi watanusurika na baa la njaa na dhiki ya maisha kwa ujumla.

Ndiyo kusema nakubaliana na waliyoyasema viongozi wa kambi ya upinzani kuwa wananchi kama wanataka kuondoakana na kero za rushwa, mazingira duni, huduma duni za elimu, afya, maji na pia wanataka kupata maendeleo na ustawi mzuri lazima wainyime kura CCM.

Kama CCM itanyimwa kura na walalahoi (wananchi wa kawaida) ambao ndiyo wengi, hakutakuwa na kitu kinachoitwa serikali ya CCM. Bali kutakuwa na serikali ya chama fulani cha upinzani au serikali ya mseto inayoundwa na vyama kadhaa vya upinzani.

Uchaguzi uliofanyika hivi karibuni wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji katika baadhi ya sehemu hapa Tanzania na matokeo waliyoyapata wapinzani japo si makubwa ni ishara kwa kila mtu makini kuwa, sasa wananchi wameanza kuiaga CCM na serikali yake kwa amani na utulivu.

Kama nchi sasa ni ya tatu kutoka chini kwa kero ya rushwa licha ya kelele nyingi za serikali ya awamu ya tatu ya CCM, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, ambaye pia ndie Mwenyekiti wa chama hicho, wananchi wanahoja zote zinazokubalika kisayansi kuwa wakati ni huu wa kuing'oa CCM kwa njia ya kidemokrasia. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook