Kinanuka!
Kuna udini udini lo! kinchi
kinanuka,
Kuuawa waumini, tena bila
mashitaka,
Kupigwa Misikitini, na
kejeli kadhalika,
Mhu! kinanuka kinchi, chuki
udini udini.
Inanuka nuka, mbaya harufu
nchini,
Raia tunavyongeka, kama
vile wahaini,
Vipigo tunapigika, na kusweka
gerezani,
Mhu! kinanuka kinchi, chuki
udini udini.
Kuna udini udini lo! kinchi
kinanuka,
Katiba ni matendoni, nadharia
ni dhihaka,
Twauawa masikini, sheria
wazifunika,
Mhu! kinanuka kinchi, chuki
udini udini.
Paroko alitamka, bado ushahidi
gani,
Kamanda alohusika, amri
kampa nani,
Na bunduki wakashika, wakalenga
vifuani,
Mhu! kinanuka kinchi, chuki
udini udini.
Kuna udini udini, lo! kinchi
kinanuka,
Walouwa kulikoni, washindwe
kushitakika,
Sirikali muna nini, uzito
kuwajibika,
Mhu! kinanuka kinchi, chuki
udini udini.
Huku kudharaulika, Ikulu
hadi bungeni,
Kutuona takataka, wachochezi
na wahuni,
Ndipo tunanung’unika, haki
mtatupa lini,
Mhu! kinanuka kinchi, chuki
udini udini.
Hebu nanyi tazameni, usukani
muloshika,
Iweje sawa kwa nini, wale
walokizika,
Walouwa hadharani, sheria
walokizika,
Mhu! kinanuka kinchi, chuki
udini udini.
Idd Kikong’oa,
Morogoro.
Fikira nazikusanya, kujibu
hili shairi,
Yarabi hisani fanya, uishushe
yako nuri,
Jamii niweze onya, kwa
haya yaloshamiri,
Ni vita vya kifikra, lazima
tuviepuke.
Lazima tuwe makini, laa
sivyo tutapotea,
Kwa vita vilo nchini, ni
mtihani tambua,
Makusudi wamebuni, wale
wenye chafu nia,
Ni vita vya kifikra, lazima
tuviepuke.
Huwezi kuiepuka, siasa
ndani ya dini,
Ni Rabi aloviweka, viwe
pamoja yakini,
Vipi leo tunataka, kuvigawa
twepukeni,
Ni vita vya kifikra, lazima
tuviepuke.
Fikra hizi jamani, kweli
zimepandikizwa,
Kuivunja yetu dini, ni
mila yetu kuchakazwa,
Sijui wafanye nini, hali
wao washawezwa,
Ni vita vya kifikra, lazima
tuviepuke.
Hii ni njama jamani, ilokaliwa
vikao,
Ni lazima tujueni, watu
wayataka yao,
Tutakuwa matatani, tukiwafuata
wao,
Ni vita vya kifikra, lazima
tuviepuke.
Hao wanaotangaza, tukiwa
Misikitini,
Siasa haitoweza, kuchanganyika
na dini,
Lengo ni kutupambaza, tusitoke
utumwani,
Ni vita vya kifikra, lazima
tuviepuke.
Kila kiumbe jamani, lazima
kiwe na dini,
Na humo ndani ya dini,
siasa haikosekani,
Yatwambia Qurani, kitabu
chake Manani,
Ni vita vya kifikra, lazima
tuviepuke.
Tamati naishilia, tufuate
ya Jalia,
Tupuuze yanongia, yanopotosha
jamia,
Fikira za kupotoa, tusije
zifuatia,
Ni vita vya kifikra, lazima
tuviepuke.
Rukia Othman,
Dar es Salaam.
|
|