NI siri isiyofichika kwamba, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ndani ya serikali mbili, kwa kiasi kikubwa umekokotwa na utawala wa chama kimoja hadi kufika hapo ulipo. Vinginevyo matatizo ambayo yamekuwa yakiusibu Muungano huo yasingefichwa na kudhibitiwa na mtu au watu wachache. Mwandishi S. HUSSEIN anaelezea zaidi.
HISTORIA ya Muungano huo inatutia hofu kuwa, kama migogoro na michafuko ya hali ya hewa vimeweza kutokea ndani ya serikali mbili za chama kimoja, hali ingekuwaje kama zingelikuwa serikali mbili za vyama tofauti?
Ilikuwa bahati njema kwamba, vigogo waliosemekana kuchafua hali ya hewa walikuwa wanachama wa chama tawala na hivyo wakashughulikiwa kichama. Ikabidi wang'olewe kuokoa Muungano. Lakini, kwa uzito wa nyadhifa zao, laiti wangelitokea chama kingine cha upinzani, hapana shaka Muungano wetu ungekwenda na maji ya bahari na kila nchi kushika ustaarabu wake.
Aidha, bahati nzuri nyingine ni kuwa, ili kuepusha kimbunga kilichomfagia Rais wa Awamu ya Pili upande wa pili wa Muungano mrithi wake na mrithi wake na mrithi wake wamebaki kinyonge kuzitweza hadhi zao na kupurura baadhi ya mamlaka ya nchi yao. Wanachama hawa wa chama tawala kwa nyakati tofauti, wameona aheri ya fedheha au udhalili kuliko kuchafua hali ya hewa na kupoteza ulaji.
Sasa swali ni je, Rais wa chama kingine angeukubali udhalili huo? Yaani achaguliwe kwa kura na wananchi wake halafu asiwe na mamlaka kamili ya nchi yake au aisujudie mamlaka ya nchi rafiki ili aweze kufanya mambo muhimu kwa maendeleo ya nchi na wananchi wake.
Iweje mkuu huyu wa nchi awe mnyonge na mdogo mbele ya Rais mwenzie anasuburi amri na huruma ya bwana wake. Ni dhahiri Rais wa kambi ya upinzani hatoridhia unyonge huu hata ikiwa serikali zote mbili ni za chama chake.
Kwa hali hiyo, ndio maana, wapinzani, wanataaluma wa sheria na watu wengine wanaoutakia heri Muungano wetu wamependekeza mapema muundo wa serikali tatu zenye mamlaka kamilifu na tofauti.
Hata hivyo, warithi wa serikali mbili wakisimamia sera za chama chao, wanajaribu kuupinga mfumo huo wa Muungano ingawaje, muelekeo wa upinzani wao ni wa kishabiki zaidi kuliko kimantiki.
Kisingizio chao cha kuheshimu maoni ya wengi na kuenzi mema ya Mwalimu, kihoja, hakina mashiko imara kwa sababu kadhaa, kimsingi, sera ya CCM haishabihiani na mkataba wa Muungano, na hapakuwepo muafaka wa wazi baina ya pande mbili husika juu ya serikali mbili ndio maana Rais wa pili wa Zanzibar akalazimika kuhoji uhalali wa serikali mbili mwaka 1984 na ameandika kitabu kuhusu suala hilo.
Juu ya hivyo, wananchi hawakuwahi kupiga kura ya maoni kuukubali mfumo wa serikali mbili. Imekuwaje mfumo huo utumbukizwe kwenye katiba kienyeji halafu mtu aseme anatekeleza sera ya chama chake kwa kuzingatia katiba?
Pili, hapakuwa na jitihada zozote za kitaifa za kuwaelimisha wananchi mijini na vijijini juu ya maana, umuhimu na manufaa ya serikali tatu. Ni vipi mtu atachagua kitu asichokijua. Upo mfano wa takwimu za watu waliokubali na kukataa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Kilichothibitisha kwamba wananchi wengi waliukataa mfumo wa vyama vingi kwa sababu walikuwa hawajui maana, umuhimu na manufaa yake ni matokeo ya chaguzi za Rais Bara na Visiwani. Idadi ya watu waliopigia kura wapinzani ilikuwa kubwa kuliko ile ya watu waliokubali mfumo wa vyama vingi.
Na papo hapo, mbona maoni ya wengi hayakuheshimiwa?
Ni wazi busara na msukumo wa ndani na nje vilitumika kupitisha mfumo huo kwa kuzingatia kiwango cha ufahamu wa wananchi wengi wakati ule. Hivyo, dai kuwa maoni ya wengi yaheshimiwe linamaanisha kuwavisha kilemba cha ukoka wana maoni kwani wameulizwa kitu wasichokijua. Japo tunaaswa tusiwaone Watanzania wajinga, lakini nina wasiwasi, hao wanaosema hivyo sio tu wanaona bali wanawafanya wananchi wajinga kiasi cha kukubali hata maneno Ujamaa na Kujitegemea yasiyo na maana yoyote katika Katiba.
Tatu, utaratibu wa (White Paper) haukuridhiwa na wengi na hata Rais amesema kuwa zoezi la kukusanya maoni limefanywa huku kukiwa na upinzani. Tukiangalia idadi ya watu waliotoa maoni tunabaini kuwa sehemu kubwa ya jamii haikushiriki katika zoezi hilo.
Mbali ya watu waliosusia utaratibu huo, mazingira ambamo maoni yalikusanywa pia hayakutoa fursa kwa wengi wa wale waliouafiki utaratibu huo.
Nne, inakubalika kuwa watu hukikubali chama kwa sera zake, sasa basi kuna vyama vyenye sera ya serikali tatu na vina wafuasi wengi kuliko idadi ya watu waliotoa maoni sijui huo wingi wa maoni unapimwa kwa mizani gani!
Tano, mtandao mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi hususan kupitia vyombo vya chama na serikali kwa namna moja au nyingine umechangia kuwashawishi wananchi kuchagua kilichotakiwa na CCM.
Sita, ijapokuwa Kamati imejiosha kwa kutoa mapendekezo maridhawa hata hivyo, muundo wake ulikuwa wa kitumwa. Siutii mashakani uadilifu wa waheshimwa Majaji tuna hofu na uhuru wao katika utendaji kazi kwa kigezo cha tume za uchaguzi na kwa hoja kuwa kwa nini serikali ya CCM inahofia tume huru na kwanini haitaki mkutano wa katiba. Ni hasara gani wanayoihofia na ni faida gani wanayoipata katika tume na kamati wanazojiundia wenyewe.
Ndio maana hata tume yenyewe imeona bora iongeze mapendekezo kufidia mapungufu yote hayo ambayo yanakinzana na demokrasia ya sasa. Kwa maana nyingine mapendekezo hayo ni maoni ya kitaaluma ya waheshimiwa waliokusanya maoni.
Kwa kweli hakuna sababu ya kulumbana kwa jambo ambalo hata kimichezo linajiweka bayana lenyewe. Ipo ligi ya soka ya Tanzania Bara (Tanganyika) na ligi ya Zanzibar na kisha ligi kuu ya Muungano. Hizi ni ligi tatu tofauti. Aidha, ipo timu ya taifa ya Zanzibar, timu ya Taifa ya Tanzania Bara (Tanganyika) na timu ya Jamhuri ya Muungano.
Ni muhali kuiua timu ya Taifa ya Tanzania bara ili ibaki timu ya Muungano halafu iwe na majina mawili kwa wakati mmoja yaani Timu ya Tanzania Bara na Muungano! Vivyo hivyo ni makosa kuitoa kafara serikali ya Tanganyika ili ibaki serikali ya Muungano yenye maana mbili. Kama ni hivyo kwa nini ya Zanzibar iwepo? Vile vile si haki kuibana Zanzibar kwa kisingizio cha Muungano.
Muungano wa sasa si wa kweli hata kidogo. Kuukumbatia ni sawa na kuficha maradhi na matokeo yake ni msiba.
Mhe. Rais amebeba jukumu la kuudumisha Muungano
wetu kwa kuyafanyia kazi mapendekezo ya Kamati yake yanayolenga kuepusha
mchafuko wa hali ya hewa baadaye.
--
|
|