USTADH mmoja amechoma moto kadi za Krismasi Njema kwa kile alichokiita kashfa dhidi ya imani yake.
Akieleza, Ustadh Juma Hussein amesema alipokea kadi hizo toka kwa Mashirika kadhaa na kampuni anayofanya nayo biashara.
"Watanitakiaje Krismasi Njema wakati nipo ndani ya swaumu. Kwanini wasinitakie funga njema?" alifoka Ust. Juma huku akimuonesha mwandishi wa habari hizi moja ya kadi iliyotoka katika Shirika moja la Umma.
"Nimezichoma nyingi, kama hawana kadi za funga njema au Eid Mubarak waache, hiyo haitavunja uhusiano wetu wa kibiashara", alisema.
Ustadh Juma ambye alifika katika ofisi za gazeti hili jana, amesema haelewi ni kwanini kila mtu katika nchi hudhaniwa Mkristo.
"Nani kawaambia utamaduni wa Kikristo na taratibu zake ndio kigezo cha kufuatwa na kila mtu?" Alihoji Ustadh Juma na kuongeza kuwa umefika wakati dhana hiyo kukomeshwa.
Amesema ametoa wito kwa Waislamu watakaotumiwa kadi hizo wazirejeshe kwa wenyewe na ujumbe: "Mimi ni Muislamu mtafute Mkristo wa kumpa".
Kwa upande mwingine Ustadh Juma amewanasihi Waislamu wasiziweke kadi hizo majumbani kwao.
Kwa kufanya hivyo amesema ni kuikubali hiyo Krismasi na kugeuza nyumba zao viwanja vya kusambaza dhana hiyo ya Krismasi.
Kadi za Krismasi njema na heri ya mwaka mpya zimekuwa zikisambazwa na watu binafsi, mashirika ya umma na ofisi za serikali.
Usambazaji wa kadi hizo ambao ni maarufu kila
mwaka, umekuwa haubagui. Hupewa kila mtu bila kujali dini yake.
ENEO la Mbagala limekuwa likikabiliwa na ukosefu wa maji kwa muda mrefu, kiasi ambacho wakazi wake wanaona ni jambo la kawaida. Mwandishi wa habari hizi alipotembelea maeneo ya Mbagala Kiburugwa na kuongea na baadhi ya wakazi, wamesema, eneo hilo bado halijasambazwa maboma ya maji na DAWASA bali ni baadhi ya wakazi wenye uwezo wamejivutia mabomba kutoka Nzasa ambayo yanatumia pampu za umeme.
"Umeme ukikatika na maji hayatoki", alisema Mwalimu Mwishehe. Watu wasio na uwezo wa kuvuta mabomba ambao ndio wengi wanatumia maji ya bondeni na wengine kuchimba visima.
Vingi vimeelezwa vipo karibu na vyoo vya watu jambo ambalo ni hatari kwa afya za watu.
"Watu wengine hununua maji ya kwenye mikokoteni ambayo hatujui wanayachota wapi", alisema mama Sikitu.
"Hiyo pesa ya kununua maji ni vigumu kuipata mtu una watoto wengi, maji nayo yanahitajika kwa wingi, haya utanunua madumu mangapi yakutoshe? Kwanza maji yenyewe hujui anayatoa wapi", alisema mama Kidawa ambaye naye ni mkazi wa eneo hilo.
Nao wakazi wa eneo la Mbagala Kizuiani wamepata unafuu kidogo, baada ya mtu mmoja kuchimba kisima karibu na shule ya msingi Mbagala ambacho kinatumia pampu ya umeme na kuyaweka katika matenki kisha kuyauzwa kwa wananchi ndoo moja shilingi 20.
Kwa mujibu wa muuzaji maji hayo ni mazuri na hayana chumvi.
"Hali hiyo imepunguza usumbufu kidogo tu, kwani si wote wenye uwezo wa kupata shilingi 20 ya maji ukizingatia mtu anahitaji kutumia ndoo hata 10 kwa siku, kwa hiyo anatakiwa atenge shilingi 200. Wakazi wengi ni wa kipato cha chini.
Juhudi za kuwapata wahusika wa DAWASA kuhusu suala hili hadi tunakwenda mitamboni hazikuweza kufanikiwa.
Wakati huo huo wakazi wa maeneo ya Tandika Azimio, Tandika Kaburi moja, Mtoni Mashine ya Maji, Mtoni Relini na Mtoni Mtongani wameanza kusahau tabu ya maji waliyokuwanayo zamani baada ya kupatiwa maji kwa mfululizo kwa kipindi kisichopungua mwezi hivi sasa.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia maji yakitokea maeneo hayo.
"Sasa hivi hatuna hata shida ya maji karibu
mwezi mzima sasa maji yanatoka", alisema Sakina Mgaya akiungwa mkono na
mama Kilenga ambao ni wakazi wa Mtoni Mtongani.
SHEIKH Suleiman Amran Kilemile ametoa wito kwa wawekezaji vitega uchumi wa ndani na nje ya nchi katika sekta ya biashara hususan upande wa mabenki kuanzisha mabenki yasiyotoza riba ili kuweza kuinua uchumi wa mwananchi wa kawaida.
Hayo aliyasema hivi karibuni wakati alipokuwa akichambua athari zinazotokana na riba alipokuwa akizungumza na wakazi wa Tandika, wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kusema kuwa kuna baadhi ya watu wa taifa fulani wamekuwa na mawazo kuwa uchumi auwezi kuendeshwa bila riba na kusema hilo si kweli.
Pia alisema kuwa wakati umefika kwa Waislamu kuwa na mabenki yao ambayo hayatozi riba kwa wateja wake na sio kwenda kuweka pesa kwenye mabenki ya watu wa magharibi ambayo hutoza riba.
Pia amekemea kitendo alichokiita kuwapa nguvu maadui wa Uislamu kinachofanywa na baadhi ya mataifa ya Kiarabu yenye utajiri mkubwa wa mafuta kuweka fedha zao kwenye mabenki ya mataifa ya magharibi kama Uingereza na Marekani kwa kufuata faida kubwa itokayo nayo na riba.
Akionesha kuchukizwa na riba, Sheikh Kilemile alisema kuwa athari za riba zimeshaanza kujitokeza duniani kote kwa kuyaweka baadhi ya mataifa kuwa masikini kabisa kiuchumi.
Wakati huo huo, Sheikh Kilemile amewataka waandaji wa hotuba Misikitini zielezee na kuyachambua mambo ambayo yanagusa wakati na mazingira husika ili kuweza kuwapatia Waislamu mwelekeo sahihi wa maisha yao.
Hayo aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Thaqafa uliopo Tandika wilayani Temeke jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Akihutubia umma uliofurika Msikitini hapo alisema kuwa "Hotuba safi ni zile zenye kumuelimisha mlengwa matukio mbalimbali yanayotokea ndani ya nchi na nje yawe ya kisiasa, kiuchumi na utamaduni".
Aidha, alisema kuwa wakati umefika kwa waandaaji na wasomaji hotuba Misikitini kote nchini kuwa wapembuzi katika kutayarisha hotuba zao kwa kusikiliza radio, kuona televisheni, kusoma magzeti na sio kwenda madukani kununua hotuba ambazo zimepitwa na wakati.
|
|