Hijaab ni faraja kwa mwanamke
 

WAKATI wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, taswira ya wanawake mitaani waliovaa hijaabu iliwastua wasiokuwa Waislamu duniani kote. Kuanzia hapo vazi la hijab likawa ni alama ya ukereketwa na msimamo mkali. Mwandishi HAWRA SHAMTE analielezea zaidi vazi hilo.

KILICHOWAPUMBAZA watu wa magharibi ni fikra za kuwa mwanamke anayejifunika anaonyesha alama ya kutengwa na kukandamizwa.

Katika fikra hizo wanadhani kwamba utawala wa Kiislamu haumpi uhuru mwanamke, lakini wasichojua kuwa Uislamu umemkomboa mwanamke kutokana na udhalilishaji wa Kimagharibi ambao umemfanya mwanamke kuwa ni bidhaa itembezwayo.

Kwa hakika hijab si ishara ya kumtenga mwanamke bali ni alama ya kumfanya mwanamke awe huru zaidi katika jamii staarabu.

Uislamu ulipomtaka mwanamke avae hijab haukumuagiza ajifungie nyumbani kwake bali ulimtayarisha kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii akiwa amechunga sitara yake.

Baadhi ya watafiti waliojaribu kuchunguza jinsi hali ya maisha ya kijamii na kiuchumi inavyokuwa kwa mwanamke wa Kiislamu anayevaa hijab, walisema kuwa wanawake wa Kiislamu wanaitumia hijab kama kinga ya kuhifadhi ustaarabu wao dhidi ya unyonyaji wa nchi za magharibi na uharibifu wa tamaduni za kistaarabu.

Na wapo waliosema kwamba wanawake wa Kiislamu wamekubali kuvaa hijab si kwa sababu za kidini bali ni kutaka wakubalike katika jamii pana ambayo kiasili ipo kwa ajili ya wanaume.

Waliotoa mawazo haya wanadhani kwamba wanawake wanaovaa hijab wana lengo la kuwaonyesha wanaume kuwa hawana nia ya kuvamia maeneo yao na wao si tishio kwao kwa namna yoyote ile.

Kwa muda mrefu suala la uvaaji hijabu litaendelea kuwa kitendawili kwa wale wasioamini na wasioelewa umuhimu wa sitara ya mwanamke katika jamii.

Bibi Habiba Nakata Kaori (31) ni mwanamke wa Kijapan aliyeingia katika Uislamu miaka 8 iliyopita na anasema kuwa kilichomvutia ni uvaaji wa hijab.

"Nimezaliwa Japan nchi ambayo ina tamaduni nyingi za kimagharibi na nilifurahia maisha ya Kijapan ya kiada na kiitikadi. Natoka katika dunia ambayo Uislamu ni suala la kufikirika, halipo wala haliingii katika nadharia za watu", alisimulia Bibi Habiba.

"Niliingia katika Uislamu mwaka 1990 nilipokuwa Paris Ufaransa. Nilikuwa nikisoma fasihi ya Kifaransa.

Kwa wakati huo suala la uvaaji wa hijabu mashuleni lilikuwa ni suala lililopamba moto katika mijadala ya wasomi.

Katika mazingira hayo niliwaona wanawake wachache tu wakivaa hijab na wengi wao walitoka bara Arabu, nilikuwa nikiwaheshimu sana.

Nikavutika na kuamua kuwa Muislamu. Nikaanza kuvaa hijabu, hapo ndipo nilipoona faida ya kuvaa hijabu. Nilijiona nimekuwa mtu mwingine kabisa niliyetakasika na kuhifadhika. Mbali na hayo niliona fahari kubeba alama ya Uislamu. Popote ninapokwenda vazi langu hufanya kazi ya kulingania bila ya kufungua mdomo wangu. Natambulika kuwa mimi ni Muislamu na ninauhubiri Uislamu kivitendo.

Watafiti waliwasaili wanawake wanaovaa hijabu waligundua kuwa wengi wao wanaelezea hisia za amani lakin watafiti hao wamezitafsiri hisia hizo kuwa zinatokana na kukubaliana tu na mtindo huo wa maisha wa kihafidhina (conservature). Anaeleza Habiba.

Lakini mimi pia ninahisi amani ninapovaa hijabu ingawa ninatoka katika jamii isiyo na ustaarabu huo.

Nadhani hisia hizo zinatokana na ukweli kwamba sasa nafuata dini ya kimaumbile na namtambua Mungu Muumba. Akielezea zaidi Bibi Habiba anasema: " Kabla sijawa Muislamu, nilikuwa nikichukia kuona mwanamke akiwa mtupu katika magazeti au televisheni. Nilikuwa nahisi vibaya kuzaliwa mwanamke. Jinsia ambayo imegeuzwa kuwa ni chombo cha mwanaume cha kujistarehesha na kumalizia matamanio yake. Lakini sasa Uislamu umenirudishia heshima yangu ya kuwa mwanamke.

"Sihisi kwamba kuvaa hijabu ni lazima kwangu bali ni furaha yangu", anasisitiza Bibi Habiba.

Bi Habiba ni mmoja tu kati ya wanawake wengi wanaohisi kwamba hijabu ni kimbilio la madhila ya unyanyasaji wa kijinsia, ni vazi ambalo humfanya mwanamke ajihisi kuwa yuko salama, mwenye furaha na amani.

Nilikutana pia na Bi Gabriel Francisco kutoka Uruguay Amerika ya Kusini aliyesema kwamba anavutiwa sana na mwanamke wa Kiislamu anayevaa hijab na hilo ndilo linalomhamasisha kuingia katika Uislamu.

Alisema amebaini kuwa Uislamu ni dini inayomthamini na kumpa hifadhi mwanamke na anajisikia kuwa ni mwenye furaha kuondokana na itikadi ambazo nafasi ya mwanamke haiainishwi kuwa ni muhimu katika jamii bali aliletwa kama wazo la unyonge la kumuondolea Adamu upweke.

Inashangaza kuona kuwa hisia kama hizo zinatokana na watu ambao hawakuzaliwa katika jamii za Kiislamu na walipoamua kuingia katika Uislamu waliona kuwa mafundisho yake yana mantiki ya hali ya juu.

Inashangaza kuona kuwa Asha, Fatuma na Halima waliofumbua macho wakijijua kuwa ni Waislamu hawana hata chembe ya fikira ya kuuangalia Uilamu katika mtazamo wanaouangalia Habiba na Gabriela. Kwa akina Asha kuvaa hijab ni bughudha wakati kwa akina Gabriela ni furaha.

Tuiangalie Hijabu katika misingi ya heshima kwa jamii na kwamba Mungu Muumba hakututakia mabaya sisi wanawake wa Kiislamu bali alikusudia tuhifadhike kutokana na wale wenye maradhi miongoni mwao.

Vipi tuone ni mateso kuvaa hijabu baada ya kuichukulia kuwa ni faraja?

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook