SWALA ni nguzo ya pili ya Uislamu na ni nguzo iliyotiliwa msisitizo sana na ikaelezwa kuwa tofauti baina ya Muislamu na kafiri ni swala.
SWALA ni wajibu kwa Muislamu na asiyesali anahesabika kuwa si Muislamu wa kweli.
Watoto wa Kiislamu wanapaswa waelezwe umuhimu wa ibada hiyo na wafundishwe kusali.
Ni lazima mzazi amhimize mtoto kusali ili amzoeze kufanya ibada angali mdogo.
Kumfundisha mtoto kutekeleza maamrisho ya dini yake ni kumfundisha kuwa mwadilifu na mtiifu.
Katika hadithi iliyopokelewa na Ibn Majah imesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu amesema: "Wakirimuni watoto wenu kwa kuwafundisha vizuri".
Wazazi hawana budi kuwapa watoto wao malezi mema, kwa kuwafunza mema na kuwafundisha wafanye ibada kwa kumcha Mwenyezi Mungu aliyewaumba.
Wazazi wataulizwa juu ya amana waliyopewa waichunge, nayo ni watoto.
Watoto ni kama maji katika mto, ambayo hufuata mkondo, endapo mkondo utapotea njia na maji nayo yatapotea na endapo mkondo utaongoza njia na maji nayo yatakwenda sawasawa.
Ni lazima wazazi wachunge tabia zao na wajitahidi kufanya mema ili watoto wawaige.
Umuhimu wa swala
Kama mto utakuwa unapita mbele ya nyumba yako na unakoga kutwa mara tano utabaki na uchafu?
Ili mtu aweze kusali anapaswa atawadhe na kwa kuwa swala hufanyika kutwa mara tano ni lazima atawadhe kutwa mara tano kama matayarisho ya kuingia katika sala, hivyo swala humfundisha mja kuwa muadilifu.
Je, huwa anajisikiaje mtu aliye nadhifu anayechunga udhu na kusali?
Bila shaka anajisikia ni mwenye furaha na mwepesi. Je, si itakuwa vizuri kama furaha hiyo na wepesi tukaigawa mipaka kwa wapenzi wetu?
Hivyo, twapaswa kuwapa watoto mafunzo ya swala ili nao wawe na furaha na wawe wepesi.
Katika Qur'an kila ilipotajwa swala imezungumzwa kuwa "husimamishwa". Hivyo watoto wanapaswa kufundishwa kuisimamisha sala ambayo ni faradhi yenye wakati maalum, ada na taratibu zake.
Swala humfanya mja awe karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kwa sababu huwa ananong'ona naye, ni mawasialiano ya moja kwa moja baina ya mja na Mola wake, vipi basi tusiwafundishe watoto wetu karama hiyo muhimu inayomuwezesha kuzungumza na Mola wake na kumcha?
Taratibu za kujipanga katika swala na kufuata amri ya kurukuu, kusujudu na kuitidali - ni utaratibu wa kijeshi unaomfanya mja awe mwepesi katika kufuata maelekezo.
Je, ni jeshi gani zuri ambalo mja angependa kujiunga zaidi ya jeshi la Mwenyezi Mungu? Muorodheshe mtoto wako katika jeshi hilo linalojipanga mistari tayari kwa gwaride kutwa mara tano. Jeshi ambalo Amiri Jeshi wake mkuu ni Mungu Muumba.
Unampomfundisha mtoto kusali unamfundisha uadilifu, adabu na unyenyekevu.
"Sote ni wachungaji na sote tutaulizwa
juu ya tulivyokuwa tukivichunga".
--
|
|