Talaka
 

WIZARA ya Kazi na Maendeleo ya Vijana imepokea kesi za ndoa 275 jijini Dar es Salaam zinazoomba zivunjwe kutokana na matatizo mbalimbali. Takwimu hizo ni za miezi mitatu tu kuanzia Juni hadi Septemba 1999.

KWA mujibu wa takwimu hizo kwa wastani Wizara hupokea kiasi cha kesi 1,000 kwa mwaka ambazo wanandoa wamechoka kuvumiliana.

Hizo ni kesi zinazopokelewa Wizarani tu, hivyo ni wazi kwamba haijulikani idadi ya ndoa zinazovunjika bila ya kufikishwa kwa Pilato.

Kwa kawaida talaka hupatikana panapo ndoa na ndoa ni mkataba wa hiari baina ya mke na mume pale wanapokubaliana kuishi kama mke na mume kwa sheria ama za kidini au za nchi.

Haiingii akilini pahali ambapo sheria inawaruhusu kukubaliana kufangamana katika ndoa na halafu sheria hiyo hiyo inawakataza kuachana.

Kuoana na kuachana ni miongoni mwa mambo ambayo binadamu wana uhuru nayo na ndiyo maana huoana kwa kuandikiana mkataba na wanapotakiwa kuachana huwabidi pia waandike kama mkataba waliouweka wameamua kuuvunja.

Hali hiyo ndiyo msingu mkuu unaomtofautisha binadamu na mnyama katika maingialino ya kimwili kwani kitabia wanyama huamua kuwa na wandani kwa muda fulani na hakuna tatizo lolote kumuacha mwandani huyo na kwenda kwa mwengine.

Endapo binadamu hataona umuhimu wa kuwa na mikataba maalum katika masuala ya ndoa na talaka, tofauti yake na mnyama itakuwa ni ndogo sana kwani atakuwa hana mipaka katika mahusiano yake na binadamu wenzake.

Kwa mujibu wa takwimu zilizonakiliwa mwanzo wa makala haya ni wazi kuwa jamii itake isitake talaka zipo na zitaendelea kuwepo. Je, vipi wale wanaolazimishwa katika mikataba yao ya ndoa kuwa "utaishi milele, kwa raha au kwa shida mpaka kifo kiwatenganishe?"

Je, inakuwaje watu waliokula kiapo kama hicho wanaposhindwa kuvumiliana katika unyumba wao?

Leo hii tunashuhudia ndoa nyingi zilizoundwa kwa msingi huo zinaporomoka na mwishowe kauli tunayoisikia ni kuwa "wametengana".
 

Nini maana ya kutengana?

Ni kuwa mke na mume hawana tena mahusiano ya kindoa lakini bado wamo katika ndoa. Mke anaweza kuishi kwake na akaendelea kutambulika kuwa ni mke wa mtu na mume anaweza akaishi kwake na akaendelea kutambulika kuwa ni mume na mtu hata mume akaendelea kutoa matunzo kwa mke na watoto.

Kitendo cha "kutengana" husababisha wana ndoa kufanya uzinifu na kuuendeleza kwa sababu tu mkataba wao wa ndoa hauwaruhusu kuachana wala mume kuoa mke mwingine - ni ndoa ya mke mmoja, mume mmoja wamefunga pingu za maisha hadi kifo kitakapowatenganisha!

Mkataba wa aina hiyo huwazuilia wana ndoa haki yao ya kuachana pale wanapochokana na huigawa familia katika misingi ya chuki.
 

Talaka katika Uislamu

Katika Uislamu, lengo la ndoa ni kuleta upendo na huruma kati ya mume na mke. Endapo mwanamke ataona sababu za msingi ambazo zinaifanya ndoa yake isifikie lengo, anao uhuru wa kudai talaka.

Mume akikataa kutoa talaka, mke anaruhusiwa kwenda mbele ya vyombo vya sheria kudai talaka.

Itabidi mume alazimishwe kutoa talaka iwapo vyombo hivyo vitashindwa kuwasuluhisha.

Wakati mwingine, mwanamke anaweza kumtaliki mumewe bila hata ya kukubaliana naye au kupitia katika vyombo vya sheria. Inawezekana kwa namna mbili:

Kama tangu mwanzo, katika kufunga mkataba wa ndoa mume alikubaliana na mkewe kuwa atakuwa na uhuru wa kuvunja ndoa endapo mume atamfanyia au atafanya jambo fulani asilolipenda. Mume atakapovunja ahadi hiyo, mke atakuwa na uhuru wa kumwacha bila ya kudai talaka kwake au mahakamani.

Kama katika mkataba wa ndoa mwanamme alitoa haki yake ya 'kutamka' talaka na haki hiyo alimpa mkewe ili kumpa uhuru na uwezo zaidi wa kuvunja mkataba wa ndoa endapo ataona haifikii lengo lililokusudiwa.

Wakati mwingine mume na mke huamua kwa pamoja kuachana baada ya kuona hawaishi kwa maelewano kama ilivyotarajiwa.
 

Sababu za talaka

Kuchukiana au kutompenda mume.

Bibi Khamsa bint Khadam alimshtakia Bwana Mtume (s.a.w.) kwa kuozeshwa mtu asiyemtaka na alipoulizwa kwanini hamtaki alisema kuwa haipendi sura yake.

Mwanamke mwingine aliyekuwa mke wa Bwana Thabit bin Qais alikwenda kwa Mtume (s.a.w.) kudai talaka na alisema: " Simtaki kwa sababu ya kasoro katika kufuata dini wala tabia bali simpendi nahofia kutomtekelezea haki zake".

Kushindwa kumhudumia mwanamke

Mwanamke hana lazima ya kuchangia katika mastakimu yake ya kila siku ingawa hakatazwi kufanya hivyo. Endapo mume atashindwa kumkimu mkewe kwa mahitaji ya lazima na mke akakerwa na jambo hilo, ana haki ya kudai talaka.

Mwanamme kukosa uwezo wa kujamiiana na mkewe

Mume anapokosa nguvu za ijimai kwa zaidi ya miezi minne mfululizo, mke ana haki ya kudai talaka.

Kundoka mume kwa muda mrefu wa zaidi ya miezi sita bila ya sababu za msingi.

Mume anapoondoka kwa sababu ambazo hazieleweki na mkewe, na mke akahisi kuwa ametelekezwa ana haki ya kudai talaka.

Wazimu

Ndoa ni muungano wa watu wenye akili timamu, mmojawapo anapokumbwa na ugonjwa wa wazimu talaka huwa ni sahihi kutuka.

Ukatili

Mume anapokuwa katili dhidi ya mkewe kwa kumpiga, kumtesa, kumdhalilisha na hata kumfanyia vitendo kinyume na maumbile, mke ana haki ya kudai talaka.

Hakuna lazima ya kuishi katika nyumba isiyo na amani, kumlazimisha kudumu katika ndoa isiyoheshimu mkataba ni kumuweka kitanzini.

"Oaneni kwa wema na achaneni kwa ihsani". (Qur. 2:229).
  


Kuvunjika kwa ndoa chanzo cha matatizo ya watoto
 

SALMA Said (28) alikuwa na miaka minane tu wakati wazazi wake walipoachana. Kuanzia hapo alichukuliwa na mama yake Saida Salum na baba yake wa kambo Zuberi Khamisi ambaye alimuoa mama yake alipokuwa na miaka kumi.

LEO katika ukubwa alio nao hataki kabisa kuolewa na kusema kuwa hamuamini mwanamme yeyote hasa akikumbuka mateso aliyoyapata mama yake kutoka kwa mwanamme. Kwa kujituliza huwa anakunywa pombe na ukahaba.

Siku hizi kuna Salma wengi ambao maisha yao yamekuwa hayafai na ni kinyume cha maadili ya kidini na ya jamii kutokana na kuathiriwa kisaikolojia na kuvunjika ndoa za wazazi wao.

Wengi wao wanadhani kuwa na wao watakapoolewa watapata mateso na ndoa zao zitaishia kama wazazi wao.

Wazazi wanapoachana watoto ndio wanaoathirika zaidi.

Inasemekana watoto wengi hudhani maisha yao yatakuwa afadhali baada ya mzazi kuoa au kuolewa na mtu mwingine lakini badala yake inakuwa kinyume, matatizo mengine hujitokeza.

Ndoa unapovunjika wazazi huangalia maslahi yao zaidi ya watoto, mwanamume huoa na mwanamke huolewa, huwa hawajali mapenzi na maisha ya watoto wao.

Mtoto anatakiwa apate mapenzi ya wazazi wote wawili, aonyeshwe kuwa anajaliwa na mtoto anapoyapata hayo huwa na furaha, uchangamfu na huweza kukua vizuri.

Mtoto huona njia pekee ya kujikwamua na mateso ya mzazi wa kambo ni kukimbia na kwenda kuishi mitaani kwa kuomba au hata wengine hujiingiza katika wizi.

Matatizo hayo hayaishii hapo, kwani anapokuwa kama mtoto wa mitaani anakuwa hapati ulinzi kwa usalama wake kama haki ya mtoto ya msingi, wengi hubakwa hasa wa kike na huweza kuambukizwa magonjwa ya zinaa.

Wazazi wa kambo katika familia nyingi wanaonekana kutotumia muda wao na mali zao kwa watoto wa kambo kama kwa watoto wao binafsi, wanajishughulisha kidogo mno au kutojishughulisha kabisa katika mambo ya shule au au chochote kinachowahusu watoto hao.

Mwanasaikolojia Judith Wallestein anasema kuvunjika kwa ndoa kunasababisha migongano ya mahitaji ya wazazi na watoto. Pia kiu ya wazazi kujitawala inasababisha kuvunjika kwa maendeleo mazuri ya watoto katika furaha na vile vile elimu.

Wataalamu wanasema kiwango cha elimu ya mtoto kinapungua pale tu ndoa inapoanza kulegalega na hupungua zaidi pale ndoa inapovunjika.

Kuvunjika kwa ndoa kunawabadilisha watoto. Katika miongo miwili ya kwanza ya uhuru asilimia 80 ya watoto wengi walikuwa kwenye familia za wazazi wawili na talaka zilikuwa nadra, lakini sasa nusu yake tu wanaishi humo.

Kiwango cha elimu cha watoto kwa wakati huo kilikuwa kizuri ukilinganisha na matokeo ya elimu ya sasa.

Kwa mujibu wa Monica Gutta, mwalimu wa shule ya msingi Mnazi Mmoja, watoto wanaoishi na wazazi wawili wanachukua asilimia 75 ya wanaofanya vizuri kimasomo shuleni ukilinganisha na watoto ambao wazazi wao wameachana au katika familia ya mzazi mmoja (waliozaliwa nje ya ndoa).

Hali hii inaonesha kuwa mtoto kuwepo katika familia ya wazazi wote wawili inamfanya awe na furaha aweze kujisomea akiwa ametulia akili yake.

Wazazi wawili wanasaidia mtoto awe na furaha kwa kumpa upendo na ndio maana mara nyingi watoto wanaoishi katika familia za kambo wanakuwa wapweke na waliojaa huzuni.

Kuvunjika kwa ndoa kunasababisha madhara gani katika maendeleo ya jamii ya watoto?

Uchunguzi uliofanywa na Mwanasaikolojia wa Kimarekani Nicolas Zill unaonesha kuwa wasichana wanaotoka katika ndoa zilizovunjika wako katika hatari ya kupata mimba wadogo, kuolewa wadogo na pia kuachana kwa muda mfupi baada ya kuolewa kuliko watoto kutoka katika familia ambazo wazazi hawajaachana.

Vile vile watoto wengi katika familia zilizoachana wanaongoza kwa vitendo vya wizi na utoaji mimba.

Hali hiyo inaonesha jinsi wazazi walivyo na umuhimu kukaa na watoto wao na kuwafunza mema ya jamii na pia kuwachunga ili wasiharibike.

Migogoro yote ya kifamilia inayosababisha kuvunjika ndoa italaumiwa kwa kuwa ndio chanzo kikubwa cha matatizo ya watoto. Italaumiwa kwa kuongeza umaskini kwa watoto na pia watoto wa mitaani zaidi ya nusu ya watoto wa mitaani mzizi wake ni kuvunjika kwa ndoa.

Ni vema kwa wazazi kufikiria sana maisha ya watoto wao kabla ya kuachana, pia wanapoachana wasijali maslahi yao tu bali pia na ya watoto yapewe kipaumbele kwani kuharibika kwa watoto ni kuharibika kwa taifa.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook