MASHAIRI

Joka limekasirika!

Joka limekasirika, li shimoni limetuna,
Tena limekasirika, hasira zenye kununa,
Tena linababaika, shimoni kwa kujikuna,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka.

Shimoni litaondoka, siafu wakiungana,
Nguvu zitaongezeka, joka la kufanya hana,
Na kamwe halitafoka, tuli litatulizana,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka.

Wananchi kamba shika, na siafu fananeni,
Nyinyi ni wengi hakika, joka mliondoeni,
Joka litaweweseka, shimoni lifukieni,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka.

Tatu nane ni yakini, joka lipo darakani,
Sasa basi lipasheni, nduli lile la kijani,
Mkiani lianzeni, mitani serikalini,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka.

Mwakani elfu mbili, kichwani limalizeni,
Kosa sio mara mbili, mbali lifutilieni,
Dhila iliyowadhili, sasa basi iageni,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka.

Tazameni hali zenu, mtaamini yakini,
Hamjui nchi yenu, yaongozwa njia gani,
Na vile vinono vyenu, vinaliwa hamuoni,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka.

Wale waliodhulumiwa, walikosa kosa gani,
Nao waloadhinwa, na kufukuzwa mjini,
Nao walohukumiwa, sheria ziso imani,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka.

Wengi walidhulumiwa, hata uhai jamani,
Damu yao kufukiwa, Mwembechai kumbukeni,
Wapo walobomolewa, nyumba zao hadharani,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka.

Wapo walochomelewa, ?vidunda? vyao jamani,
Wazee wadhulumiwa, mafao yao jamani,
Wapo wanaobaguliwa, kwa dini zao jamani,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka.

Vitani tukaingizwa, dhidi ya ?nduli? Amini,
Nchi imevamiwa, twende tukamtoeni,
Kumbe fumbo twafumbiwa, kama wajinga majnuni,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka.

Faida yake ni nini, tupo hoi taabani,
Uganda ipo hewani, sisi tupo majangwani,
Hivi twalipendeani, joka nduli la kijani,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka.

Mbali tuliacheni, lijifie taabani,
Kwa salama liageni, kura zenu linyimeni,
Nguvu ziimarisheni, dhuluma muifuteni,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka.

Hapa ninakuageni, nyinyi sio masikini,
Uchumi ulo shakani, joka kakuleteeni,
Yatieni akilini, niliyoyanena kinywani,
Joka limekasirika, siafu wamezinduka

Mwapwani M.
Dar es Salaam.



Takibiiir Mbukuzi

Wako wengi na majoho, tele kichwani ujuzi
Mafisadi na waroho, vibaraka wachafuzi
Kiko wanikosha roho, Amiri Sheikh Mbukuzi
Ndiyo ndiyo mwana kwetu, Takibiiir !

Ni Allahu Akbaru!!,twende mbele mtetezi
Kuapa kwa yake nuru, Kitabu chake Mwenyezi
Kisha wanazikufuru, seraze kuto kuenzi
Ndiyo ndiyo mwana kwetu, Takibiiir !

Wewe ndiye Ulamaa, madhubuti kiongozi
Wahoji yanotufaa, na kupinga ubaguzi
Sikama walopumbaa, kwa futari na michuzi
Ndiyo ndiyo mwana kwetu, Takibiiir !

Tatizo ni Utwaghuti, ni wa kweli upembuzi
Haki zetu mahututi, njaa iko waziwazi
Kura zinatusaliti, na tufanye uamuzi
Ndiyo ndiyo mwana kwetu, Takibiiir !

Hasa haya matabaka, yamezusha kiangazi
Yameibua vibaka, na kufunza majambazi
Balaa na hekaheka, kichochoro humalizi
Ndiyo ndiyo mwana kwetu, Takibiiir !

Ni Allahu Akibaru!!, tuwang?oe walowezi
Kura iwe ni sururu, kuchimbulia mizizi
Wanyonge tujinusuru, ziondoke shida hizi
Ndiyo ndiyo mwana kwetu, Takibiiir !

Takbiiir!! Takbiiir!!, haya umebaki mwezi
Takbiiir!! Takbiiir!!, yataka maandalizi
Takbiiir!! Takibiiir!!, Kiko nimewapa kazi
Ndiyo ndiyo mwanakwetu, Takibiiir!!

Ila mwisho tahadhari, hodi hodi kwa wakubwa
Watakulisha futari, na vipesa vya ubwabwa
Utaacha mstari, hiyo ni dhuluma  kubwa
Ndiyo ndiyo mwanakwetu, Takibiiir!!

Idi Kikong'ona
Morogoro

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook