Hakuna haki pasipo fidia
 
Na Dkt. Abdallah J. Saffari
 

HAKUNA haki pasipo fidia. Maana yake ni kuwa haitoshi kuwa na sheria zinazozingatia na kulinda haki za binadamu ambazo hazitoi fidia zinapokiukwa. Himaya ya haki za binadamu inaweza kulindwa katika ngazi kuu tatu. Kwanza kabisa kitaifa, pili, kibara (continental) na tatu kimataifa.

Kitaifa

Kimsingi ni rahisi na vyema kufidia ukiukaji wa haki za binadamu katika ngazi ya kitaifa. Hii inawezekana tu kwanza iwapo katiba na sheria zinahifadhi haki za binadamu. Pili, iwapo kuna taasisi ambako mtu anayelalamika kuvunjiwa haki zake za binadamu anaweza kupeleka madai yake na kufidiwa.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inahifadhi haki za binadamu kadhaa wa kadhaa kama ilivyotajwa hapo awali (I.h.j). Fidia kutokana na ukiukaji wa haki hizo inaweza kutolewa na Mahakama Kuu (Ibara ya 30(3) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, i.h.j). Lakini katiba haielezi aina gani za fidia zinazoweza kutolewa na mahakama hiyo.

Kwa bahati mbaya kutokana na Watanzania wengi kutoijua sheria hakuna madai mengi ya fidia kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu yanayopelekwa Mahakama Kuu. Shauri la Kasisi Mtikila kuishitaki serikali kwa kukiuka haki yake ya kugombea Urais ni la kipekee katika historia ya haki za binadamu nchini (Rev. Mtikila v. Registrar of Political Parties and Attorney General, Civil Case No. 1985, High Court, Dodoma). Mahakama yaliafiki hoja ya mlalamikaji.

Mara moja moja Mahakama Kuu huombwa kutoa amri chini ya maombi ya habeas corpus ili kupinga kuwekwa ndani mlalamikaji bila ya kufikishwa mahakamani.

Hali hii inatia wasiwasi mkubwa kwa vile kuna ushahidi dhahiri wa ukiukaji wa haki za binadamu katika mwenendo wa mashauri ya jinai kama vile ucheleweshaji wa kesi (Angalia tasnifu ya Udaktari wa Falsafa ya Dr. Abdallah J. Saffari, "Human Rights in the Criminal Process with Reference to Tanzania Mainland", University of Sussex, England, 1994), kukataa dhamana bila ya sababu za maana (K.h.j) na kutotoa msaada wa kisheria katika makosa makubwa ya jinai (K.h.j).

Kibara

Mabara ya Ulaya na Marekani yana vyombo viwili vikuu vya utoaji fidia kutokana na ukiukaji haki za binadamu. Bara la Ulaya lina Kamati ya Haki za Binadamu na Mahakama ya Haki za Binadamu. Raia wa Ulaya ambao wameshindwa kupatiwa fidia na taasisi za nchi zao hupeleka madai yao kwenye taasisi hizo. Taasisi zote hizi mbili zimefanya kazi nzuri sana ingawa kumekuwa na msisitizo katika utekelezaji wa haki za kiraia na kisiasa kuliko za kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Pia kumekuwa na tatizo kuhusu kasma ya fidia.

Bara la Marekani nalo lina Kamati ya Haki za Binadamu na Mahakama ya Haki za Binadamu. Taasisi hizo nazo zimefanya kazi kwa ufanisi ingawa sio kama zile za Bara la Ulaya.

Bara la Afrika halina Mahakama ya Haki za Binadamu bali lina Kamati ya Haki za Binadamu.

Tanzania ni muanzilishi wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika. Iliafiki Makubaliano Kuhusu Haki za Binadamu Barani Afrika (African Charter on Human and Peoples Rights) miaka minne baada ya makubaliano hayo kutiwa saini na nchi nyingine za Kiafrika. Ilikuwa nchi ya kumi na moja kufanya hivyo.

Pengine ni vyema kuelezea hapa kwamba taasisi zote za kimataifa zinazosimamia utekelezaji haki za binadamu hutoa fidia kwa ukiukaji haki za binadamu. Lakini inasikitisha kuona kwamba fidia kama hiyo haiwezi kutolewa na Kamati ya Afrika ya Haki za Binadamu.

Usimamizi wa haki za binadamu chini ya makubaliano hayo ya Afrika uko mikononi mwa Tume ya Afrika kuhusu Haki za Binadamu. Hapa kuna matatizo mawili. La kwanza, ni kuwa utendaji wa Tume hiyo unakabiliwa na matatizo mengi kimuundo na kiutendaji (Rembe, N.S., System on Protection of Human Rights under the African Charter on Human and Peoples Rights: Problems and Prospects, Institute of Sourthern African Studies, Rome, 1991).

Kwa maneno machache tu, Tume hiyo ipo kama haipo. Pili, serikali ya Tanzania, hadi hivi karibuni tu, ilikuwa imewasilisha taarifa mara mbili tu mbele ya Tume hiyo kuonesha namna inavyotekeleza haki za binadamu Tanzania (Angalia Dr. J. Saffari, "Human Rights in the Criminal Process with Reference to Tanzania Mainland" i.h.j). Yafaa hitilafu hii ya kiutendaji nayo irekebishwe na serikali ya Tanzania.

Kimataifa

Kwa bahati mbaya hakuna mahakama ya Dunia ya Haki za Binadamu. Badala yake kuna Kamati ya Dunia ya Haki za Binadamu chini ya Sheria ya Kimataifa ya Haki za Kiraia na Kisiasa (I.h.j). Tanzania iliafiki sheria hiyo ya Kimataifa ingawa haijatambua rasmi mamlaka ya Tume ya Dunia ya Haki za Binadamu. Inaweza kufanya hivyo tu kwa kutia saini Nyongeza ya Kwanza ya Sheria ya Kimataifa ya Haki za Binadamu na Kisiasa (First Optional Protocol to the International Covenant on Civil and Political Rights).

Raia wa nchi nyingi wamepeleka madai yao mbele ya Tume ya Haki za Binadamu (Mathalan raia katika Marekani ya Kusini na nchi nyingine za Kiafrika kama vile Zaire). Tume hiyo haina uwezo wa kimahakama lakini hutoa maoni kupendekeza namna ya kufidia ukiukaji haki za binadamu. Kwa bahati mbaya raia wa Tanzania hawajapatiwa fursa hiyo. Serikali haijaeleza kwa nini hadi sasa haijayatambua mamlaka ya Tume hiyo ya Haki za Binadamu. Tafsiri ya kutofanya hivyo ni kwamba serikali haitilii maanani suala la utekelezaji wa haki za binadamu katika ngazi hii.

Aidha, nchi zote ambazo zimetia saini sheria ya Kimataifa ya Haki za Kiraia na Kisiasa zinatakiwa kuwasilisha mbele ya Tume ya Haki za Binadamu, kila baada ya miaka miwili, taarifa kuhusu namna inavyolinda na kutekeleza haki za binadamu. Na hapa napo Tanzania imeshindwa kufanya hivyo kama ipasavyo, kwani baina ya 1980-1992 waliwasilisha taarifa mbili fupi mno mbele ya Tume hiyo (angalia tasnifu ya Dakta Saffari, i.h.j). Yafaa kasoro hizi zirekebishwe mara moja. Kamati hii inao wajibu wa kuishinikiza serikali kufanya hivyo.

Kasma ya fidia

Suala la namna na kiwango gani kinakidhi fidia ya ukiukaji haki za binadamu dhidi ya mlalamikaji ni muhimu sana.

Makusudi ya fidia ni kumrejesha mlalamikaji katika hali aliyokuwa nayo kabla ya kosa kutendeka (Kanuni hiyo, maarufu kama restitution in integrum ilianza kutumika zamani katika kesi kama vile Hadlay v. Baxandale (1984) 9 Exh. 34, na bado inaendelea kutumika katika mahakama zote za kimataifa).

Malipo ya fedha ndiyo njia kuu ya kulipa fidia. Daima kumekuwa na matatizo ya kukasimu kiwango hasa cha fidia ambacho mlalamikaji anastahili kulipwa kwa fedha. Na hatupendi kuzama katika mjadala huo kwa sasa. Isipokuwa ni vyema kusema kwamba fedha haiwezi daima ikafidia barabara madai ya mlalamikaji. Aghalabu madhara ambayo hutokea kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu hayawezi kufidia kwa fedha. Mathalan hakuna idadi ya fedha ambayo itaweza kufidia mateso na madhila aliyoyapata mlalamikaji kutokana na kuwekwa rumande kinyume cha sheria. Jambo bora zaidi ni kuepuka ukiukaji haki za binadamu kwa kuing'oa mizizi yake.

Hitimisho

Kwa miaka mingi Tanzania imepata sifa nje kwa kutokiuka haki za binadamu. Lakini ni kweli pia kwamba hapa nchini kuna watu wengi ambao haki zao za binadamu zinakiukwa. Bunge lilichangia katika ukiukaji wa haki hizo kwa kupitisha sheria kadha wa kadha ambazo zilihalalisha jambo hilo. Kwa hivyo sasa ni wajibu wa Bunge kuihakikishia jumuiya ya kimataifa na hasa raia wa Tanzania kwamba sheria zote zinazopingana na haki za binadamu zinabatilishwa mara moja. Na kuanzia sasa Bunge liwe macho na makini kuhakikisha halipitishi sheria mpya ambayo itakiuka haki za binadamu. Na endapo haki za binadamu zitakiukwa kuwe na taasisi imara za kufidia ukiukaji huo kwa malipo.

Vile vile Bunge linao wajibu wa kuitaka serikali iafiki Nyongeza ya Kwanza ya Sheria ya Kimataifa ya Haki za Kiraia na Kisiasa (First Optional Protocol to the International Covenant on Civil and Political Rights) jambo ambalo litawawezesha Watanzania kuwakilisha madai yao ya haki za binadamu endapo hawaridhika na maamuzi ya taasisi za kitaifa kuhusiana na suala hilo.

Aidha, ni wajibu wa raia kuishinikiza serikali iwasilishe katika Kamati ya Haki za Binadamu ya Afrika na ile Kamati ya Haki za Binadamu ya Kimataifa, katika muda unaotakiwa, taarifa kuhusu utekelezaji wa haki za binadamu nchini Tanzania. Jambo hili lina manufaa kwa Watanzania wenyewe vile vile kwa mataifa mengine ambayo yataelewa dhamira ya Tanzania katika utekelezaji wa haki za binadamu.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook