Kaeni chonjo msitoswe Rwanda
HIKI ni kipindi cha Waislamu kutumia vyema akili, busara na kuchukua maamuzi muafaka.
Hali inayowakabili ni ya kutisha. Hakuna kinachoashiria mtazamo wa kheri bali ishara ya shari.
Bila kutafakari kwa makini, wanaweza kujikuta wametoswa Burundi, Rwanda au Kossovo.
Wanaambiwa wavae magwanda ya ukachero wamdhibiti Sheikh Mbukuzi, utadhani ndiye aliyewaua Waislamu pale Mwembechai. Wamdhibiti Sheikh Mbukuzi utadhani ndiye aliyempiga risasi na kumtia kilema Chuki Athumani na kuamrisha wanawake Waislamu wavamiwe Msikitini na kudhalilishwa.
Wanaambiwa waidhibiti Shura ya Maimamu utadhani ndiyo iliyounda mfumo usio rasmi wa kibaguzi uliowanyima watoto wao elimu na vyeo!
Padri Lwambano na viongozi wa serikali walio katika mtandao wa Kanisa waliochochea mauaji ya Mwembechai, hao hawaambiwi wawadhibiti!
Wanapewa muhadhara juu ya katiba, sheria na utawala wa kisheria. Huku bila hatia Mzee wao maskini Mzee Chatta kateswa jela, akanyimwa dhamana! Naye Muhammad Omar bila ya hatia anawekwa rumande na kukosa matibabu hadi akafia huko na ile tu haki ya kufanyiwa 'inquest' ananyimwa! Kina Simbaulanga wanaingizwa rumande mlango wa mbele wanatolewa wa nyuma!
Waislamu washukuru tu kuwa watu wa mtandao wamewasambazia majibu ya madai yao.
Lakini wazingatie hatari iliyopo katika majibu hayo.
Hapa kuna mbinu ya serikali kukwepa lawama. Waislamu wanatoa ushahidi kwamba matatizo yanayotokana na serikali kuendesha mambo kwa upendeleo, yapo hata kama mambo hayo yanafanywa na watendaji pasipo kuwepo mfumo rasmi unaoruhusu ubaguzi.
Serikali inadai yenyewe ni refa wa kuhakiki uhuru na haki sawa kwa kila upande.
Mbinu hii inaweza kujenga hoja ya kuwagombanisha Waislamu na Wakristo, Serikali inataka ionekane Waislamu wanaghadhabu ya ujinga na umaskini wao baada ya kuwaona Wakristo wameendelea hivyo wanajenga chuki zisizo na msingi na hivyo madai yao ni sawa na kutaka serikali iwadhibiti Wakristo au iwapendelee wao ili wafike walipo Wakristo, jambo ambao ni la kipuuzi.
Mbinu hii pia ni sawa na ile ya kuhimiza Interfaith dialogue. Inajengwa hoja ya kutaka Waislamu watatue matatizo yao kwanza kwa kukiri kuwa wana moyo wa husuda dhidi ya Wakristo na ndiyo maana wana endesha hata mahubiri ya "kashfa" dhidi yao, jambo ambalo linadaiwa ndilo litakalo vunja amani ya nchi na siyo dhulma inayodaiwa kufanywa na serikali dhidi ya Waislamu. Hivyo inahimizwa kuwepo na "interfaith dialogue".
Zimwi hili la Interfaith dialoque lazima lifichuliwe na kuwatahadharisha Waislamu waepukane nalo. Interfaith Dialogue inayohimizwa huenda ni ile inayolenga kuwaweka Wakristo, Wahindu na makundi mengine yasiyo kuwa Waislamu upande mmoja na Waislamu upande mwingine. Kisha ijengwe hoja ya kuonesha makundi mengine yote yanawaelewa na kuwakubalia Wakristo isipokuwa Waislamu ambao watahukumiwa kuwa ni wabishi, jeuri na wenye "jazba" za chuki!
Kama kweli hawa wanataka Interfaith Dialogue mbona walikataa ile aliyoiandaa aliyekuwa Rais, Alhaj Ali Hassan Mwinyi ili Wakristo waeleze maana ya Mihadhara ya kashfa wanayoilalamikia.
Hivyo katika mazingira haya ya serikali kukandamiza Waislamu kisha kutumia mbinu ya kubadilisha shutuma na kuzifanya ni za chuki na jazba dhidi ya Wakristo, serikali haiwezi kuwa refa!
Serikali kama chombo hakiwezi kuacha Wakristo wanakitumia kwa manufaa yao dhidi ya wengine hususan Waislamu halafu kikwepe jukumu la kujirekebisha badala yake kiwaambie Waislamu wakazungumze na Wakristo na yenyewe (serikali) itakuwa refa!
Hawezi kuwa refa mtu anaevaa jezi ya upande mmoja wa timu zinazopambana. Hawezi kuwa refa yule anaechezesha katika kiwanja kisicho kuwa sawa, upande mmoja uko juu kuelekea upande mwingine ulio chini katika mchezo ambao "half time" timu hazibadilishani upande wa magoli.
Hawezi kuwa refa mtu anaeruhusu upande mmoja kuvunja sheria za mchezo na kufunga magoli ya kuotea (off-side), magoli ya mkono na kadhalika.
Hawezi kuwa refa yule anaeteua wajumbe wa kamati ya majaji wa rufaa toka timu anayoipendelea kisha kuwataka walioonewa waende kulalamika kwa majaji hao!
Ipo hoja kwamba hakuna mfumo rasmi wa kibaguzi hivyo hakuna sababu ya kuunda chombo cha kuzuia ubaguzi. Mantiki hii mbona haisimami. Kwa mfano, hatuna mfumo rasmi unaoruhusu rushwa. Lakini tunakiri kuwa rushwa ipo. Wala Rais hasemi tusimsumbue kwa malalamiko ya kuenea rushwa serikalini na kwamba tukiiona twende kushitaki mahakamani tu! Mbona tunakiri rushwa ipo pasipo kuwepo mfumo rasmi? Mbona kikosi na tume na vyombo vya uchunguzi mbalimbali vimeundwa licha ya kuwepo utaratibu wa kupeleka kesi za rushwa mahakamani?
Imekuwa ikiletwa hoja ya "Kihistoria" kama sababu ya Waislamu kuwa nyuma kimaendeleo katika elimu na hivyo kukosa kazi za madaraka. Lakini hapo hapo inatolewa changamoto ya kuonesha Waislmu wengi mabalozi. Sisi tunasema kuwa huo ni ushahidi kuwa wapo Waislamu wenye ujuzi ambao wakipewa fursa wanaonesha umahiri wao na hivyo "Human resourcebank" iwatafute Waislamu wengine na kuwapa fursa pasipo ubaguzi. Vinginevyo tuambiwe basi, ni sababu zipi za "kihistoria" zilizofanya Waislamu wawe wengi kwenye ubalozi lakini wasionekane au wawe wachache kwenye sekta nyingine!
Mauji ya Mwembechai yalichochewa na hatua zilizochukuliwa na serikali kuitikia fitna za uchochezi huo zilizotolewa na Padri Camillus Lwambano.
Hoja inatolewa kuwa mauaji yale hayahitaji uchunguzi, kwani kila kitu kinajulikana. Pili, halikuwa suala la kidini kwani hata Wakristo walikuwepo. Tatu, serikali haijaona sababu ya kuunda Tume.
Tunafahamu kuwa baada ya Fitna za Paroko Lwambano, msako ulianza Msikiti kwa Msikiti hadi uvamizi ulipofanywa pale Mwembechai na wanawake kudhalilishwa ndani ya Msikiti.
Sasa kama polisi walipovamia Msikiti Wakristo walikuwepo, basi hiyo ndiyo sababu yenyewe ya kuunda Tume. Msikitini walifuata nini? Kwanini wao hawakuuliwa? Mauaji yale hayakutokana na risasi zilizopigwa ovyo. Watu walilengwa shabaha baada ya kuchaguliwa, nani apigwe. "Piga yule, mwongeze .. mtakoma, yote haya sababu ya Ruksa..."
Kama kilichotokea kinajulikana, tuelezwe kilitumika kigezo gani kumchagua wa kumlenga shabaha na sheria gani ilitoa ruhusa hiyo. Kwanini waliochaguliwa kupigwa risasi wakawa Waislamu watupu! Kinajulikana nini? Kwamba wauaji walitumwa, walipewa maelekezo?
Kinajulikana nini, mbona baada ya mauaji visingizio vilielekezwa kwa watu mbalimbali na baadaye serikali yenyewe kukanusha yale yale iliyotangulia kuyasema!
Waliomuua marehemu Imran Kombe walijulikana hali kadhalika sababu. Lakini Tume iliundwa na kesi ilipelekwa mahakamani. Katika mauaji ya Mwembechai uzito watoka wapi kama siyo dhulma dhidi ya Waislamu?
Waislamu miongoni mwa Wamakonde na Wayao, waliwahi kuikabili serikali ya kikoloni kwa udhalimu wake iliyokuwa ikiufanya ikiwatoza kodi halafu inawapa fedha Wakristo pekee waliokuwa wachache wajenge na kuendesha mashule yao.
AMNUT ilianzishwa kuukabili udhalimu huo huo.
Baada ya uhuru baadhi ya maeneo ya Waislamu katika wilaya ya Pare (sasa Mwanga) walikataa kulipa kodi kwa sababu serikali iliwadhulumu. Walitozwa kodi lakini fedha za misaada ya elimu wakapewa Wakristo pekee.
Akina Abdillah Plantan na Khamis J. Abeid waliwekwa kizuizini na Mwalimu Nyerere waliposimama kidete kutaka dhulma dhidi ya Waislamu iondoke.
Awali ya yote katika wote hawa hayupo aliyedai kuwa nchi haina katiba au sheria. Hakuna aliyedai kuwa nchi ina sera rasmi za kuwabagua baadhi ya watu.
Lakini suala ni kuwa yanayosemwa kwenye majukwaa ni mengine na yanayotekelezwa kisirisiri ni mengine. Isitoshe, vifungu vya katiba na sheria havikuwekwa ili viwe vikitajwa tu. Vipo ili vitekelezwe na ionekane vinatekelezwa na wale waliokula kiapo kuilinda na kuitetea katiba ya nchi.
Kama tulivyosema hapo juu, hatuna mfumo rasmi unaokubali rushwa. Mbona tunapambana nayo na tumeunda Tume ya kushughulikia rushwa. Mbona hatuleti hoja kuwa kuunda Tume ni kukiri kuwa rushwa ipo! Kama ubaguzi upo, basi upo tu. Kutokuwepo kwa mfumo rasmi wa kibaguzi haufanyi usiwepo. Wala ubaguzi hauwezi kuwepo kwa sababu ya kuundia mbinu za kuuondoa na kuuzuia. Na hivyo ndivyo ilivyoonekana pale ilipoamuliwa haja ya kuchukua hatua dhidi ya rushwa.
Pili, haki kuu ya msingi ni haki ya uhai. Mtu huwa hai kwanza ndipo akadai haki nyingine. Anaekunyima haki hii kakusudia kukunyima zote.
Raia wanapouliwa na vyombo vya dola na dola inasema haioni sababu ya kuchunguza vifo hivyo, basi angalau raia hawa waelezwe wajihesabu kama wao ni watu sawa na wengine au la!
Waafrika, Afrika Kusini walielezwa hadhi yao mbele ya Makaburu, walijua namna ya kuishi na hali hiyo. Na walipoamua kuing'oa walijua namna ya kuishughulikia.
Uhai wa mtu ni kitu kitakatifu. Anayeua mtu mmoja pasi na haki ni sawa na kuua watu wote. Waliouliwa Mwembechai ni Waislamu. Damu iliyomwagwa ni ya Waislamu. Ndio maana Waislamu wote hatukubali mauaji yale ya Mwembechai yapuuzwe pasipo kuwachukulia hatua wahusika wote.
Kama tulivyotangulia kusema ndugu Waislamu, hiki ni kipindi kizito. Ni kipindi kinachoashiria kuwa Waislamu wasitegemee kitu.
Waislamu wakipeleka hoja ya Kadhi, huletewa agenda ya kumdhibiti Sheikh Mbukuzi, la Kadhi haliguswi.
Wakihoji OIC, huambiwa maoni ya Wakristo hayawezi kupuuzwa na kwamba suala hilo litahitaji ridhaa ya wote kitaifa. Lakini wahusika hawasemi kwa nini upo Ubalozi wa Vatican na nani aliulizwa kabla ya kuruhusiwa, kuwepo nchini.
Waislamu hawana budi kutafakari kwa makini sana uchochezi wa Padri wa Kikatoliki Paroko Lwambano na mchango wake katika mauaji ya Mwembechai kutokana na kauli yake iliyoitikiwa na serikali.
Kisha wafanye rejea aina ya mahusiano yaliyokuwepo kati ya Maaskofu na wauaji wa mauaji ya maangamizi kule Rwanda.
Waislamu vile vile waipime kauli ya kiongozi mmoja wa juu wa Kanisa nchini kuhusu mauaji ya Mwembechai halafu walinganishe na hali ilivyokuwa Bosnia, Kossovo na sasa Chechnya ambako Maaskofu wa Kirusi wanamshangilia Putin na kumsifia anavyowaangamiza Waislamu.
Waislamu yatafakarini kwa makini mazingira haya mpate kuyaelewa vizuri.
Tumuombeni Allah (s.w.) atupe subra na atukinge na shari ya wale wenye nia mbaya na sisi.