Na Asia Mohamed
ADHABU za viboko bado zinaendelea kutumika katika shule nyingi hapa nchini hasa shule za msingi.
HAMISI (12) ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya Msingi (x) (jina siyo halisi). Hamisi amekuwa mtoro kutokana na kukimbia adhabu ya viboko inayotolewa na walimu shuleni kwao.
Yeye hazimudu barabara hesabu, hivyo daftari yake hujaa 'mikasi' mingi na hii husababisha mwalimu kumchapa bakora. Matokeo yake Hamisi anakimbia shule moja kwa moja.
Nakumbuka nilipokuwa shule ya msingi mwalimu wetu wa hesabu alikuwa anatuchapa fimbo moja kwa kila hesabu moja unayokosa, hivyo ukikosa tano fimbo tano.
Mtoto Hamisi akiwa mtoto shuleni ni matokeo ya adhabu za viboko ambazo sio tu humjengea mtoto chuki dhidi ya walimu wake au walezi wake bali pia humnyima haki yake ya elimu na malezi bora.
Walimu na wazazi au walezi wanapaswa kujua kuwa kumfunza adabu mtoto siyo kutumia viboko, bali kumuelimisha lipi la kufanya na lipi la kuacha.
Kwa mfano shuleni, kuna kazi nyingi ambazo unaweza kumpa mtoto kama adhabu. Kazi kama kumwagilia maji bustanini ya mboga au maua, kufagia darasa, kusafisha choo au ofisi za walimu ni adhabu tosha kwa wanafunzi. Hii ni kwa sababu kwanza unakuwa umemwadhibu na hivyo kumuadabisha na pili unamfundisha kufanya kazi.
Hali hii hufamya mwanafunzi kujitahidi kusoma kwa bidii ili kuepuka adhabu toka kwa walimu wake.
Kitu kingine walimu muwe karibu zaidi na watoto/ wanafunzi wenu ili mjue tatizo ni nini hasa ambalo linawafanya watoto au wanafunzi wasingatie masomo yao vizuri.
Huenda tatizo ni la kisaikolojia kutokana na malezi anayoyapata nyumbani, labda kulelewa na mama wa kambo au mtu baki.
Mwalimu upende kurudia yale uliyoyafundisha ili wanafunzi wakuelewe vizuri na ikibidi uwe unauliza maswali kila mara ili ujue ufahamu wao.
Kama matatizo yanatokana na malezi ya nyumbani jaribu kuwasiliana na wazazi/walezi wake ili ujue ni jinsi gani utamsaidia mtoto huyu.
Kwa upande wa nyumbani, wazazi na walezi mjaribu kuwa karibu na watoto wenu. Wanapofanya makosa mjaribu kuwaonya kwanza kwa maneno.
Angalieni madaftari ya watoto wenu na muwaulize leo wamejifunza nini shuleni, somo gani hawajaelewa na kama wewe mzazi unalielewa msaidie.
Uisitangulize viboko, kwani ataona hakuna tofauti kati ya nyumbani na shuleni. Hali hii itamuathiri kisaikolojia.
Baadhi ya wazazi na walimu walikuwa na maoni yafuatayo juu ya mada hii.
Mwalimu Stella Joseph, mwalimu wa shule ya msingi hapa Dar es Salaama anasema haoni sababu ya kumchapa viboko mtoto kama njia ya kumuadabisha. Kwanza mtoto anakuwa sugu, kwa kuwa kila atakapofanya kosa, anajua atachapwa tu na hivyo ataendelea kufanya makosa yale yale.
Vile vile mwalimu huyo, ameendelea kusema kuwa baadhi ya walimu wana hasira, hivyo huweza kumchapa mtoto katika hali ya hasira na hivyo huweza kumsababishia maumivu makali au hata majeraha makubwa.
Anamalizia kwa kusema kuwa, lengo la adhabu ni kumkanya au kumfunza mtoto aone kuwa yale aliyoyafanya siyo mazuri. Hivyo basi anashauri kuwa mtoto apewe adhabu kama za kufagia madarasa, kumwagilia na kadhalika.
Kama amechelewa kufika shule asubuhi, vile vile apewe adahbu ya kubaki shuleni na afanye adhabu aliyopewa. Kesho yake atawahi shuleni na atafanya vizuri zaidi.
Naye mama Maria Massawe muuguzi hospitali ya Rufaa Muhimbili, yeye anasema kwamba kwanza mtoto aambiwe kwa mdomo, kosa lake, asipojirekebisha ndipo viboko vifuate, kwani akipata maumivu mtoto ataacha tabia mbaya.
Mama Fatuma, mama wa nyumbani mkazi wa Kariakoo, anasema yeye bila viboko watoto wake hawamsikii. Anasema kwake yeye adhabu maridhawa ni fimbo. Watoto wake wakipata fimbo mbili tatu wanakuwa watiifu.
Dk. Maridadi, daktari wa magonjwa ya watoto anashauri kwa ksuema kuwa mtoto kwanza apewe mapenzi na malezi bora toka kwa wazazi wake, anapofanya kosa, wazazi waangalie na waupime uzito wa kosa, kabla ya kutoa adhabu kali.
Kwa mfano, badala ya kumchapa viboko, mwambie sitakununulia nguo ya sikukuu, au mwambie ukiwa wa kwanza darasani nitakununulia nguo nzuri,viatu vizuri au hata baiskeli.
Mtoto akishafikiria vitu vyote hivyo vizuri, atajihidi asifanye makosa kuanzia nyumbani mpaka shuleni.
Vile vile daktari huyu mwanamke, anashauri kuwa kama mtoto hamudu masomo au masomo fulani, atafutiwe mwalimu wa kumsaidia, vile vile kuwepo mawasiliano ya mara kwa mara kati ya walimu na wazazi au walezi wa watoto ili kuweza kutatua matatizo ya watoto wetu.
Kwa ufupi fimbo hailei mwana!
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |