Siku ya sikukuu ni siku ya Ibada

Na Hawra Shamte


 


KRIMASI ya mwaka huu sawa na ya mwaka jana, haikuchangamka kwa sababu Waislamu wamo ndani ya mfungo wa Ramadhani.

Huo ni uoni wa Betty Raphael mkazi wa Mikocheni.

Betty anasema kuwa kuzorota kwa sikukuu hiyo inayosadikiwa kuwa ni ya uzawa wa Yesu Kristo kunatokana na "mapatna" katika ufisadi kujizuilia kwa kutokunywa pombe, kwenda kwenye madisko na starehe nyingine kadhaa wa kadhaa.

Angela Livingstone mkazi wa Kinondoni anasema kwamba hali hiyo ya utulivu inaonesha kuwa wenye fujo ni Waislamu.

Evandensiana Mushi mkazi wa Tabata ambaye ni mmiliki wa "Bar" moja maarufu Tabata Relini anasema biashara yake katika mwezi huu si nzuri kwa sababu wateja wake wengi wako katika swaumu.

Hizo zote si sifa njema kwa mtu anayejiita Muislamu ambaye maana ya jina lenyewe tu inamsuta mtu mwenye matendo maovu.

Uislamu maana yake ni salama, amani na unyenyekevu hivyo Muislamu anapaswa kuzibeba sifa hizo kwa kila hali bila ya kujali huu ni wakati wa Ramadhani, Krismasi au Idd, anapaswa ajipambe na utanashati wa Uislamu kwa kujiepusha na mabaya na maovu.

Si hayo tu wenye tunguli na wapunga mashetani nao wamekwenda likizo wanasubiri tu wale sikukuu na hawatadiriki hata kufunga sita.

Yote tisa kumi Allah (s.w.) husamehe dhambi zote kasoro kushirikishwa.

Huu ni mwezi wa toba, wafungaji hujizuilia kwa mengi ili wapate radhi za Mola mrehemevu. Lakini Allah (s.w.) amesema katika kitabu chake kitukufu kuwa, "Humsamehe dhambi zake yule anayefanya toba ya kweli...".

Toba ya kweli ni ile yenye azma ya kutorudia tena makosa. Waswahili wanasema kuwa 'kufanya kosa si kosa, bali kurudia kosa...'.

Sikukuu inakuja, haikuandikwa pahali kuwa wakati wa sikukuu milango ya pepo inafungwa na ya moto kufunguliwa - la hasha.

Ila tunapaswa kufahamu kwamba kufanya dhambi siku ya Idd ni sawa na kufanya dhambi siku ya kiyama.

Hebu fikiria siku ambayo utakuwa umesimamishwa mbele ya Mola wako na hapo hapo ukatenda dhambi, je unaweza kukadiria ghadhabu za Mwenyezi Mungu juu yako?

Kuna watu wameiwekea nadhiri siku ya sikukuu kuwa watakunywa hadi wagaregare na wengine wamedhamiria kustarehe na vimada wao hadi asubuhi na kuumaliza usongo wa mwezi mzima.

Mtu atakayefanya vitendo hivyo siku ya sikukuu afahamu kwamba atakuwa amepoteza ibada zake zote za siku 29 au 30 za Ramadhani.

Siku ya sikukuu ni siku ya kumshukuru Allah (s.w.) kwa kuwawezesha kufunga kwa siku thelathini na kusali sala za ziada na ni siku ya kumuomba Mungu azipokee funga zetu, sala zetu na maombi yetu hivyo si siku ya kufanya vitendo viovu.

Kufanya maovu siku ya sikukuu ni sawa na yule mwanamke anayefuma nyuzi zake mchana wa kutwa na ikifika usiku akazifumua zote na kuwa amepoteza nguvu zake bure mchana kutwa na usiku anaambuliwa patupu.

Siku ya sikukuu ni siku ya kula vizuri, kuvaa vizuri na kutakiana kheri si siku ya kumkhalifu Mwenyezi Mungu.

Katika siku 30 tumeweza kusema kuzini hapana, kunywa pombe hapana, kumshirikisha Mwenyezi Mungu hapana, kusengenya hapana na kadhalika. Tumeweza kusema hapana mwezi wa Ramadhani vipi tusiweze kusema hapana mwezi wa kula mchana?

Tuchunge tusije tukaharibu ibada zetu za mwezi mzima kwa starehe za siku moja.

Siku ya sikukuu ni siku kubwa kwa Mwenyezi Mungu nasi waja twapaswa kuitukuza kwa kufanya vitendo vyema.


Eid el Fitr njema


Na Maulid Ahmed


NI siku ya sikukuu, nyuso zina furaha na tabasamu isiyo na kifani.

Watoto wamependeza kwa kuvishwa nguo vizuri na kupikiwa vyakula vizuri.

Siku ya sikukuu kama ambavyo ni siku ya furaha kwa watu wazima pia ni siku ya furaha kwa watoto.

Watoto wafundishwe adabu za Uislamu siku ya sikukuu, waambatane na wazazi wao kwenda kusali sala ya Idd, watoe mikono ya kutakiana Idd njema na wakatoe mkono wa Idd kwa ndugu, jamaa, marafiki na majirani.

Furaha ya siku ya sikukuu huwavaa watoto pasipo kiasi. Siku hiyo huwa hawana muda wa kupigana, kugombana au kufanya fujo, ni siku maalumu ya utanashati kwao na hususan kwa sababu wamevaa nguo mpya.

Inapokaribia sikukuu ya Idd mawazo ya watoto wengi yanakuwa juu ya nguo nzuri na mpya, hivyo wazazi wanapaswa wajitahidi kukidhi wawezavyo wasiififishe furaha ya watoto wao.

Siku ya sikukuu ni siku ya mapenzi na huruma na pia ni siku ya unyonge kwa watoto watakaokosa kuifurahia sikukuu ama kwa kula chakula kizuri au kuvaa nguo nzuri au kutembea.

Kadhalika ni siku ya majonzi kwa wazazi walioshindwa kutimiza matarajio ya watoto wao, lakini wanapaswa wajipe moyo kuwa kupata na kukosa ni katika uwezo wake Mungu Muumba na anapaswa ashukuriwe kwa kila hali.

Endapo mzazi atakosa kizuri cha kumvisha mwanawe, basi badala ya kukaa kwa unyonge anapaswa awape moyo wanawe kuwa Mungu anawapenda kwa kuwajaalia uzima katika siku hiyo ya sikukuu ambayo wengine hawajadiriki ama wagonjwa taabani kitandani au wanasubiri kufukiwa udongoni.

Kwa siku ya sikukuu, wenye uwezo wa kimali wanapaswa watoe zakka kwa wasio na uwezo ili nao waifurahie sikukuu.

Wazazi wasisahau kutoa zakkat el-Fitr, wajitolea wao na ahli zao ili sikukuu iwe ni siku ya furaha kwa Waislamu wote.

Aidha, wazazi wanapaswa wajiepushe na vitendo viovu kwa siku ya sikukuu kama vile kupigana, kutukanana au kulewa, kwani kufanya hivyo huwatia simanzi watoto.

"Siku za sikukuu huwa ni siku za matatizo kwetu kwani baba haonekani nyumbani wala hawachi pesa za matumizi na akirudi usiku mkubwa humpiga mama hadi awe taabani".

Asha Salehe (10) anaelezea madhila yanayotokea nyumbani kwao siku za sikukuu.

Wazazi kufanya vitendo kama hivyo ni kuwakosesha amani na furaha watoto na pia huwasababishia matatizo ya kisaikolojia.

Siku ya sikukuu ni siku ya furaha, wazazi wahakikishe kuwa wanawafurahisha watoto wao siku za sikukuu kama si kwa mali basi kwa hali, nyumbani kuwe na mazingira ya amani, utulivu na mapenzi.

Tunawatakia wote sikukuu njema!
 

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji


   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook