HABARI


Imamu akatwa mapanga na kuporwa milioni tatu


IMAMU wa Masjid Nurania Modeco mjini hapa Ahmad Juma Bagule amevamiwa na kukatwa mapanga pamoja na kuporwa shilingi milioni tatu ambazo zilikuwa za kulimia shamba lake.

Akielezea tukio hilo mapema wiki hii, Imamu huyo alisema kuwa alifanyiwa vitendo hivyo vya kinyama na vijana wawili wa Kimasai katika eneo la Mwanzo Mgumu katika kijiji cha Kambala tarafa ya Mvomero Morogoro vijijini.

"Vijana wawili wa Kimasai siku ya Desemba 24, 1999 wakiwa na sime na marungu majira ya mchana walifika kwenye eneo la shamba langu na kudai nimewaibia ng'ombe wao, walipokagua kwenye nyumba yangu na kukosa, wakanifunga kamba na kuanza kunicharaza bakora", alisema huku akionesha majeraha kwenye vitanga vyake vya mikono.

Aliendelea kusema kwamba baada ya kumfunga kamba na kumpiga sana wakaingiza mikono yao kwenye mifuko ya suruali ya Imamu huyo na kuibuka na kitita cha fedha shilingi milioni tatu ambapo walimuambia, "Sisi shida yetu siyo ng'ombe tulitaka fedha kutoka kwako", alisema na kuongeza kwamba Wamasai hao pia walichukua radio yake kubwa (bendi nne).

Imamu huyo wa Msikiti mpya wa Nurania alisema kuwa baada ya muda alitokea mtu mwingine aitwaye Ally ambaye alitaka kumsaidia Imamu huyo, ndipo mvua za fimbo zilipomnyeshea na hatmaye kukatwa na sime kichwani na mgongoni na kupelekea kushonwa nyuzi kadhaa na kulazwa katika hospitali ya mkoa.

Baada ya tukio hilo alisema kuwa wakaenda katika ofisi ya Afisa Mtendaji wa kijiji hicho ambaye aliwapa barua ya kwenda polisi Kituo Kikuu cha Polisi Mjini Morogoro ili wahusika ambao afisa huyo alisema ni tishio kijijini hapo waweze kuchukuliwa hatua zinazostahili.

Aliongeza kusema kwamba walifika kituo kikuu cha polisi ambapo aliambiwa kwamba magari pamoja na polisi wa kwenda kuwakamata watu hao yapo isipokuwa (magari) hayana mafuta. Ndipo ikamlazimu Imamu huyo kutoa shilingi 15,000 kujaza mafuta kwenye gari la polisi.

Alisema kuwa polisi walipofika kijijini hapo hawakuwakuta watuhumiwa hao na kuamua kuwachukua ndugu wawili wa majambazi hao na kuwaweka rumande ambapo baada ya siku mbili walitoka kituoni hapo kwa dhamana.

Aidha, Imam Bagule aliyefungua kesi yenye Namba Mo/BB/12529/99 kutokana na kukatwa viganja vya mkono hawezi kujitafutia mahitaji yake muhimu yeye na familia yake ukiachilia usumbufu anaopata wa kufuatilia kesi hiyo polisi ambapo wameonesha ushirikiano mdogo katika kulifuatilia suala hilo.

Katika toleo lake la Septemba 17-23, 1999 gazeti hili (AN-NUUR) liliandika juu ya wakulima wa mkoa wa Morogoro kumlilia mkuu wao wa mkoa Bw. Lawrance Ntazama Gama juu ya vurugu na uharibifu unaofanywa na jamii ya wafugaji wa Kimasai katika mashamba ya Mgongola - Mvomero.

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Bw. Christopher Shekihondo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.


Dodoma wawaombea dua Chechnya


MAMIA ya Waislamu mjini Dodoma walijumuika eneo la Majengo (Masjid Ghazal) kuwaombea wapiganaji wa Chechnya.

Dua hiyo ambayo ilianza kutangazwa katika Misikiti yote ya mjini Dodoma ilipokelewa kwa ari kubwa na waumini.

Wakitoa nasaha zao fupi kabla ya kuanza kwa dua hiyo, viongozi wa AL-MALLID mkoani walisema sababu kuu ya vita hivyo ni chuki ya makafiri dhidi ya Uislamu.

Ustadh Kabutali alisema kuwa vita hivyo si vya Wachechen peke yao, ni vya Waislamu wote duniani. Aidha, alisema misaada ya hali na mali inahitajika kuwafikishia Wachechnya na ikibidi kusaidia katika mapambano hayo kinadharia.

Naye Ustadh Mohammed Kiwipa toka Masjid Mugadamati aliwaambia Waislamu kuwa Wachechnya kama Waislamu wengine duniani, wameyapata matatizo pale walipoamua kuitekeleza nguzo ya kwanza ya Uislamu, ambayo inaashiria kumpwekesha Allah (s.w.) na kuuweka utawala wake.

"Sala, saumu, zaka na hijja ni nguzo ambazo haziwatishi makafiri lakini ikigusa nguzo ya kwanza utachukiwa na makafiri na hata baahi ya Waislamu nao watakuangalia vibaya", alisema Ustadh Kiwipa.

Wazee mbalimbali wameonesha kufurahishwa kwao kwa kufanyika kwa dua hiyo, Mzee Alhaj Hamis Lubuva alisema; "Hakika kuhudhuria kwa vijana wengi katika dua kunaashiria ushindi kwa Waislamu uko karibu kwani vijana ni chachu za harakati duniani kote.

Bi Mwanahamisi Abdallah naye alitoa wito kwa Waislamu wote nchini kuwaombea dua ndugu zao Wachechnya, siku ya Ijumaa ya mwisho ya Ramadhani kwa kusoma kunuti.

"Hatuna uwezo kwa kwenda huko kuungana nao bega kwa bega, basi tushindwe hata kwa dua tu", alimalizia mama huyo.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook