Nisingekubali kuwa kibaraka
Hivi UN inaridhika kuona
dola bilioni 1,485 zikiteketezwa ?
MAHITAJI ya lishe na afya kwa watoto wote ulimwenguni ni dola 13 bilioni za Kimarekani kwa mwaka, inafichua ripoti ya muda si mrefu ya fuko la kimataifa la watoto ulimwenguni (UNICEF) ambalo ni shirika tanzu la Umoja wa Mataifa (UN) unaoongozwa na Dk. Kofi Annan kama Katibu Mkuu wake.
MAHITAJI ya jumla ya kuokoa maisha ya watoto hawa kila mwaka ni dola bilioni 34 tu, ambapo mbali na lishe na afya, taaluma ya msingi ya watoto hawa inahitaji dola bilioni sita tu kwa mwaka. Na bilioni 15 zilihitajika kuwapatia watoto hawa maji safi na salama pamoja na mipango imara ya maisha yao kijamii. Hata hivyo wanasiasa wa ulimwengu wamelifumbia macho suala hilo tete.
Hivyo, watoto hawa waliotelekezwa kama si kutupwa nje kabisa ya bajeti za kila mwaka za serikali zetu nyingi duniani, hivi sasa wanateketea kwa ukosefu wa lishe bora, afya iliyotengemaa na ukosefu wa elimu sahihi ya kuwaonesha japo mwangaza hafifu wa matumaini mwishoni mwa pango lenye kiza kinene cha ujinga.
Aidha, watoto hawa wasiojua mustakabali wa maisha yao ya mbeleni wanaangamizwa kwa kunyimwa maji safi na salama, na kwa ujumla kutopangiwa kabisa mipango thabiti au kupangiwa mipango duni (chini ya sera zisizotekelezeka) ya kuboresha mazingira yaliyowazunguka na miundo mbinu ya maendeleo yao binafsi kama si ya jamii wanazoishi.
"Bila shaka watoto wote ulimwenguni wanaweza kubisa kuokolewa katika janga hilo baya la maangamizi iwapo dunia itawapa kipaumbele na kupunguza matumizi yake yasiyo ya lazima", inasema sehemu ya ripoti hiyo ya shirika hilo tanzu la UN bila kueleza Umoja huo umefanya nini kuishinikiza dunia iokoe jahazi hilo liendalo mrama.
Sambamba na hilo, imeelezwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wote wa dunia hususan kwenye nchi zinazoendelea wanaishi katika hali ya umasikini wa kupindukia, hali ambayo imezaa ongezeko kubwa la vitendo vya uhalifu, watoto wa mitaani na maradhi yanayoweza kuzuilika.
Kwa mujibu wa shirika lingine tangu la UN linalohusiana na masuala ya fedha (World Bank) wanachi wa nchi husika wanaishi kwa kati ya dola tatu hadi chini ya dola moja kwa siku. Hali ambayo inapelekea baadhi yao kuponea mlo mmoja kwa siku.
Wakati hayo yakijiri, wanasiasa wa dunia wanapoteza zaidi ya dola bilioni 800 za Kimarekani kwa mwaka kugharimia majeshi yenye malengo ya kiwazimu, bilioni 400 kununulia Segereti! Bilioni nyingine 245 kununulia bia na na mvinyo na bilioni zaidi ya 40 kugharimu kile wakiitacho Game of rich yaani mchezo wa gofu, jumla ikiwa ni dola za Kimarekani 1,485 kwa mwaka, inaanika juani ripoti ya UNICEF.
Wananchi kadhaa waliohojiwa na mwandishi wa makala hii kwa nyakati tofauti hivi karibuni wanasema kwamba, chanzo kikuu cha tatizo hilo sugu la kuteketeza pesa za walipa kodi kwa matumizi ya kihayawani huku jamii husika ikiangamia kikatili ni kwa viongozi waliopewa dhamana ya mamlaka na madaraka katika jamii hizo kukosa uadilifu, na kuwa wabinafsi pamoja na mipango butu ya maendeleo kiujumla.
Chanzo kingine ni kwa wananchi wenyewe kukubali kuhujumiwa kiakili kama si kutekwa kifikra na watu wasio na sifa za uongozi, kwa kuwapa mamlaka hali ambazo ni sawa na kujikaanga kwa mafuta yako mwenyewe.
Na kwa upande wa Umoja wa Mataifa na jumuiya zake, nitakuwa nawanyima haki na heshima stahiki endapo sitawaita wanafiki.
Unafiki huo unatokana na ripoti zao za kusisimua wazitoazo kila mwaka kwa ulimwengu bila kuweka wazi mipango yao thabiti ya kudhibiti pale penye tatizo na kutia nguvu pale penye matumaini.
Mtu mwenye dhamana kubwa ya kadhia zote chafu zinazoigubika dunia hivi leo ni Katibu Mkuu wa Umoja huo Dk. Kofi Annan na vigogo wenzake waandamizi ambao wamepewa rungu na ulimwengu kuzilinda jamii zao, lakini sasa 'vigogo' hawa wa UN wamelewe madaraka kiasi cha kuutukanisha ulimwengu kwa kuruhusu umoja huo uwekwe mfukoni mwa baadhi ya nchi zilizojipa 'upolisi wa dunia'.
Mimi binafsi kama ningekuwa Dk. Annan au ' kigogo' mwandamizi wa UN singekubali kuendeshwa puta na taifa lolote lile duniani kinyume na katiba ya UN kiasi cha kupoteza haiba yangu binafsi na umoja wa Mataifa kiujumla.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |