Muungano wa khofu hautadumu

MTAALAMU wa mambo ya siasa Profesa Mwesiga Baregu ameonya juu ya hatima ya muungano wa khofu badala ya matarajio.

Amesema, kuwa na aina hiyo ya muungano inazifanya serikali ziwe legelege zikitawaliwa zaidi na unafiki.

Prof. Baregu aliyasema hayo wiki hii katika mahojiano maarufu yanayorushwa na kituo kimoja cha televisheni Jijini kila jumatatu.

"Dola zijenge misingi ya kuwawezesha raia kudhibiti serikali badala serikali kudhibiti raia", alisisitiza Profesa huyo wa sayansi ya siasa.

Aidha alitahadharisha juu ya hatari ya kuendelea kuukumbatia mshikamano uliojengwa kwa msingi wa mchanga badala ya zege.

Kuhusu viongozi wa serikali kutokuwa wavumilivu wanapokosolewa, alisema kwa muda mrefu hapa nchini ulijengwa utamaduni wa "uwenzetu" ambapo wananchi na viongozi walidumu kupongezana na kusifiana.

"Kutoka kwa mwenzako hujifunzi, mnadumaa wote", alisisitiza Prof. Baregu.

Aidha alikosoa utaratibu uliokuwepo enzi za awamu ya kwanza ambapo ilisisitizwa kudumishwa fikra za mtu mmoja.

"Zidumu fikra za mtu fulani maana yake zidumae fikra za jamii", alionya

Kuhusu marekebisho ya katiba Prof. Baregu alisema Tanzania haijawa na katiba kama mkataba kati ya watawala na watawaliwa hivyo inahitaji Katiba ya aina hiyo.

Maelezo ya Profesa Baregu yamekuja wakati wananchi wakiibana serikali ya Rais Mkapa katika masuala kadhaa ya kisiasa.

Miongoni mwa mambo yanayoendelea kuhojiwa na wananchi wengi hivi sasa ni aina ya muungano iliyorithishwa kwao na marais waasisi wa Tanganyika na Zanzibar.

Masuala mengine ni pamoja na kutokuwepo tume huru ya uchaguzi, kuporwa kwa mamlaka ya raia kuwajibisha serikali halikadhalika viongozi wa juu wa serikali kutokuwa tayari kukosolewa au kusikiliza malalamiko ya wananchi.

Hata hivyo serikali ya Rais Mkapa kwa upande wake imeendelea kudai kuwa itaendelea kuyaenzi kwa nguvu zote yale iliyorithi kutoka kwa waasisi wa Taifa hasa hayati Mwalimu Nyerere.


Serikali inachangia kuua maadili

MAOVU yanayostawi nchini na kupelekea kumomonyoka kwa maadili katika jamii yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na serikali.

Hayo yalisemwa na Ustadh Ilunga Kapungu katika kongamano la Waislamu wa mji wa Mwanza lililoandaliwa na Umoja wa Vijana wa Misikiti ya Mwanza katika Msikiti wa Arafa Mabatini siku ya Jumamosi Januari 1, mwaka huu.

Ustadh Ilunga alisema serikali ina uwezo wa kukomesha maovu yanayotendwa katika jamii, lakini imekuwa ikifanya unafiki wa kisiasa. Inakemea maovu kwa upande mmoja na kwa upande mwingine kutoa leseni za maovu hayo na kukusanya kodi.

Akifoa mfano alisema ni serikali inayoruhusu na kuhimiza ufuska kwa kutoa leseni kwa madanguro.

Alisema huko nyuma serikali iliweza kuzuia uvaaji wa nguo fupi na ikasimamia utekelezaji wa amri hiyo.

Huo ni ushahidi kuwa serikali ikitaka kukomesha uovu inaweza, alisema.

Akizungumzia mtizamo wa serikali juu ya wale wanaokemea maovu alisema; "inashangaza kuona wale wanalitakia mema Taifa kwa kukemea maovu ndio huandamwa badala ya kupongezwa".

Alionya kuwa iwapo Waislamu hawataisafisha jamii kutokana na maovu wajue athari yake itawakumba pia.

Naye Ustadh Issa Rashid wa Madrasatu Thaqib aliwapa nasaha Waislamu wadumu katika lengo la swaumu ambalo ni kumuabudu Allah (s.w.).


Utalii usitumike kuvurugua maadili - Sheikh Mbukuzi

IMAMU Masjid Mujahiduun Sheikh Juma Mbukuzi Salim ambaye pia ni Amir wa Waislamu Dar es Salaam ametahadharisha juu ya kuvurugwa maadili kunakotokana na biashara ya utalii Tanzania visiwani.

Akizungumza Msikiti hapo hivi karibuni, Sheikh Mbukuzi amesema biashara ya utalii imekuwa ndio njia rahisi inayotumika kuingiza maovu Zanzibar na hatimaye kuvuruga kabisa maadili mema katika jamii. Ulevi, uzinifu ni miongoni mwa maovu yanayoelekea kushamiri kwa kasi Zanzibar kupitia biashara ya utalii.

Katika taarifa hiyo Sheikh Mbukuzi amesema serikali inajua fika nini madhara ya ulevi, nini madhara ya uzinifu kama hivi ndivyo, Sheikh Mbukzi amesema hapana budi hatua zichukuliwe kudhibiti maovu hayo kwa kuangalia uwezekano wa kufanya biashara hiyo ya utalii bila kuruhusu maovu.

"Kwani biashara ya utalii haiwezi kufanyika bila kuruhusu pombe, uzinifu...?" Amehoji Sheikh Mbukuzi.

"Kuna nchi katika dunia hii zinafanya biashara ya utalii bila kuruhusu maovu", amesisitiza.

Wakati huo huo, shule ya msingi Masjid Mujahiduun inatarajiwa kufunguliwa mwezi huu. Akitoa taarifa hiyo, Sheikh Mbukuzi amesema masomo yote ya shule ya msingi yatafundishwa pamoaj na masomo ya dini ya Kiislamu.

Amewataka wazazi kuitumia fursa hii kuwaandikisha watoto wao shuleni hapo ili wapate elimu iliyokamilika.

Aidha, Sheikh Mbukuzi amesema kuna fursa kwa wale wanaotaka kuchangia ukamilishaji wa ujenzi wa shule hiyo kutoa michango yao.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook