Waislamu kuamua hatima yao
MAELFU ya Waislamu wanatazamiwa kuhudhuria Baraza la Idd Mosi litakalofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini.
Katika Baraza hilo ambalo huenda likawa la aina yake katika miaka ya karibuni, kutajadiliwa hatima ya Waislamu hapa nchini kufuatia majibu ya Rais Mkapa kuhusu malalamiko yao.
Ili kulifanikisha Baraza hilo lililoandaliwa na Halmashauri Kuu ya Waislamu, viongozi wa jumuiya zote wameafikiana kutokuwa na Baraza au hafla nyingine yoyote siku hiyo.
Kwa mujibu wa wasemaji wa Jumuiya mbalimbali za Kiislamu jijini, kikao cha pamoja kiliazimia Waislamu waume kwa wake, wazee kwa vijana wamiminike katika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Hata hivyo, wasemaji hao hawakuwa tayari kueleza chochote kuhusu agenda kuu iliyopelekea muafaka huu wakihistoria ambao utawakutanisha mahali pamoja Waislamu wa madhehebu zote nchini.
Gazeti hili limefahamishwa kuwa ili kuwawezesha Waislamu kufika mapema eneo la tukio umeandaliwa usafiri maalum utakaowachukua waumini kutokea Msikiti wa Mtambani kwa upande wa Kinondoni na Msikiti wa Tungi kwa wakazi wa Temeke ambapo wale wa Ilala wametakiwa waelekee ukumbini moja kwa moja.
Katika Baraza la Idd mwaka wa jana, Kamati iliyoundwa na Halmashauri Kuu ya Waislamu iliitaka serikali ichunguze na kuchukua hatua juu ya madai ya kukandamizwa kwa Waislamu kidini na kijamii hapa nchini.
Risala ya Kamati hiyo iliyosomwa mbele ya Rais Benjamin Mkapa ilituhumu uadilifu wa serikali, Bunge na Mahakama kuhusiana masuala kadhaa ambapo Waislamu wametokea kuwa waathirika wakuu.
Risala hiyo ilitaja eneo la elimu kuwa mojawapo ya yale yanayohusika na tuhuma hizo ambapo idadi kubwa ya vijana wa Kiislamu ilielezwa huishia mitaani huku wenzao Wakristo wakifurika katika taasisi mbalimbali.
Aidha, Kamati hiyo ilieleza kuwepo kwa mkakati maalum serikalini wa kuwazuia Waislamu katika eneo hilo.
Maeneo mengine ni pamoja na mgao wa madaraka makazini, magereza mengi nchini kujaa vijana wa Kiislamu, suala la OIC na mauaji yaliyofanywa na polisi Msikiti wa Mwembechai mwezi Februari mwaka wa juzi.
Rais Benjamin Mkapa alikiri uzito wa madai hayo na kuahidi kuyashughulikia baada ya "uchunguzi wa kisayansi" kufanyika.
Baada ya kupita kimya kirefu inasemekana Rais ameyatupilia mbali madai ya Waislamu.
Imedaiwa kuwa Rais ametoa majibu yanayohalalisha mauaji ya Mwembechai kwa kusema kwake kuwa hajaona sababu ya kuundwa Tume kuchunguza mauaji hayo.
Aidha, imeelezwa kuwa amedai kuwa yeye ni Rais pia wa wanywapombe na wala nguruwe, hivyo kuyaweka kando malalamiko dhidi ya wanaofuga nguruwe na wanaouza ulevi karibu na Misikiti.
Kufuatia majibu hayo, wito umetolewa kila Muislamu aliye na chembe ya imani asikose kuhudhuria Baraza la Idd Diamond ili kujadili kwa pamoja hatma ya Waislamu nchini Tanzania.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |