CHAMA cha siasa cha CUF hakipo kuhubiri mambo ya mbinguni, bali kuleta ukombozi kwa Watanzania.
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Lipumba ameeleza kuwa, chama chake kipo kuwakomboa wananchi wasione kuwa shida na umasikini ndio maajaliwa yao.
"Unapokuwa na sera mbovu za uchumi na hali ya maisha ikazidi kuwa duni, wananchi wanaizoea hali hiyo na kuona ni majaaliwa yao", amesema Prof. Lipumba.
Ni kutokana na hali hiyo mbaya inayowakabili wananchi, unapatikana uhalali wa kuwepo CUF ilete ukombozi.
Prof. Lipumba ameeleza kushangazwa kwake na sifa kemkem zinazotolewa kwa ukusanyaji wa kodi wakati hali katika huduma za kijamii na maisha ya wananchi inazidi kuwa duni.
Prof. Lipumba yupo ziarani mikoa ya kusini na amekuwa akifanya mikutano mbalimbali ya hadhara.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wamesema, wanaodai CUF ni chama cha udini wakachunguze kwanza Ikulu wamejaa watu wa dini gani.
"Wasitufanye hatuna akili, Ikulu, kwa Waziri Mkuu, Spika wa Bunge, Majaji na Mwanasheria Mkuu na sehemu zote nyeti nani wamejazana huko? Mbona hawasemi taasisi hizo zina udini", alihoji Mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Said Nachunguru.
Akizunguza katika mazungumzo yaliyoibuka baada ya Prof. Lipumba kusema kuwa wapinzani wa CUF wanadai kina udini, Mzee Nachunguru alisema hizo ni mbinu za watu waovu wanaowadhania wenzao ni waovu kama wao.
Katika mjadala huo uliojumuisha wazee na vijana, suala la udini lilionekana kuwa propaganda ya kudumaza demokrasia.
"Anayedai chama fulani ni cha udini apeleke ushahidi wake kwa Msajili wa vyama asituhubirie mitaani, sisi sio wasajili wa vyama vya siasa", alisema Bw. Wadhifa Nangwanda.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |